SHERIA YA MAGAZETI YAWA GUMZO BUNGENI

MBUNGE wa Viti Maalum (CCM), Dk Pindi Chana amewaomba wabunge, wahariri na wadau wa masuala ya habari nchini kumpa majibu nini kifanyike pale magazeti yanapotumika kuchochea mambo kwa kuandika habari za kupendelea upande mmoja, au za kuvuruga amani.
Dk Pindi alisema hayo jana bungeni wakati akichangia mjadala wa Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa mwaka 2013, uliowasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Frederick Werema, ambao ndani yake kuna sheria tofauti 14 zinazofanyiwa marekebisho, ikiwemo Sheria ya Magazeti ya 1976.
Katika mchango wake huo, Dk Pindi ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala,iliyoshughulikia muswada huo, alitoa ombi hilo kwa maelezo kuwa yeye hana majibu.
“Wametuambia lengo la marekebisho ya Sheria hii ya magazeti ni kuongeza adhabu, ili kulinda matumizi ya lugha ya matusi yanayoweza kusababisha ukosefu wa amani, sasa nauliza pale ambapo magazeti yanatumika kuchochea mambo na kuvunja amani, ndio uhuru wa habari, nauliza na sina majibu, wahariri , wabunge niambieni," alihoji Dk Pindi.
Alisema hana matatizo na vyombo vya habari, wala waandishi au wahariri, lakini wapo baadhi yao wananunuliwa na kikundi cha watu kupotosha ukweli au kupendelea upande fulani, na kuhoji wachache hao wafanyweje?
“Wale wanaotumika ndivyo sivyo, leo Bunge hili liseme nini kifanyike, Watanzania wenzangu tusaidiane pale ambapo kikundi cha watu kinatumia vyombo vya habari kubeba kikundi kimoja na hususan kwa wanasiasa (magazeti) yanatumika sana tufanyeje?” aliendelea kuhoji Dk Pindi.
Akitoa mfano alisema kuna nchi leo zinashindwa kurudisha amani, na kuitaja nchi ya Misri kuwa wameshindwa kurudisha amani yao na kutaka Watanzania na wadau nchini kusaidiana kupata jibu ya swali hilo.
Akitoa mfano alisema kichwa cha habari kinapoandikwa kwamba mtu fulani ni jangili, alafu kesho akaombwa radhi, ili hali hata Mahakama haijathibitisha mashitaka yaliyoandikwa dhidi ya mtu huyo, na kusema hali hiyo inamshushia heshima mtuhumiwa.
“Magazeti yanapaswa kuelimisha umma na kuwafundisha lakini vichwa vya habari hivi leo vinaandika nini?" alihoji Dk Pindi.
Mbunge wa Peramiho, Jenista Muhagama (CCM), aliitaka Serikali kuleta Muswada wa Sheria ya Vyombo vya Habari ili ujadiliwe bungeni, kwani ndio suluhu na ukombozi wa vyombo vya habari. “Serikali yangu tuleteeni Muswada huo, Kamati ya Maendeleo ya Jamii inalia huko, kwa nini tunachelewa kuuleta?Uletwe ili Bunge liujadili na kuupitisha tupate sheria itakayolinda tasnia yote na kuangalia weledi,” alisema Muhagama.
Alisema kuna watu wanaidhalilisha tasnia ya habari bila sababu na kuitaka Serikali ilete Muswada huo ili itoe majibu ya maswali yanayoulizwa kila kukicha ya magazeti nchini.
“Ukiletwa hapa tutaujadili na tutapata sheria nzuri ya kuangalia vyombo hivi, na kuhakikisha amani ya taifa hili inalindwa, uleteni hapa tuujadili,” alisema Mhagama.
Kambi ya Upinzani Bungeni katika hotuba yao iliyosomwa na Msemaji wao,Tundu Lissu, imeitaka Serikali kufuta kabisa Sheria ya Magazeti ya sasa na badala yake, ilete Muswada bungeni utakaotunga sheria mpya itakayohifadhi uhuru wa habari na uhuru wa mawazo.
Lissu alisema hiyo inatokana na ukweli kwamba kuna madai ya msingi ya muda mrefu yaliyotolewa Mwaka 1991 na Tume ya Nyalali ikitoa mapendekezo kwa Serikali kuleta Sheria ya Uhuru wa Magazeti, kwani sheria zilizopo hazitoi uhuru huo.
Awali akiwasilisha marekebisho ya sheria hiyo, Jaji Werema alisema katika sheria hiyo vifungu vinavyofanyiwa marekebisho ni kile cha 36(1) na 37 (1) (a).
Sheria hiyo kwa sasa kabla ya marekebisho kuletwa bungeni, kifungu cha 36 (1), kinasomeka; “ mtu yeyote atakayechapisha habari za uongo, au za uzushi au kuchapisha taarifa itakayosababisha woga na kuleta uchochezi katika jamii au kuleta usumbufu, utakaondoa hali ya amani, atakuwa amepatikana na hatia ya kutenda kosa na atakabiliwa na adhabu ya kulipa faini isiyozidi Sh 150,000. Au kwenda jela kwa miaka isiyozidi mitatu au kutumikia adhabu zote kwa pamoja.”
Baada ya marekebisho, sheria hiyo imeongeza adhabu ya faini hadi kufika Sh milioni tano. Kadhalika, kifungu cha 37 (1) b, kinachohusu uchochezi kwa lengo la kusababisha vurugu, na kuharibu mali, wahusika watakabiliwa na makosa ya kulipa faini ya Sh milioni tano au kwenye jela kwa miaka mitatu au kutumikia adhabu zote kwa pamoja.
Akiwasilisha marekebisho kwenye sheria hiyo, Jaji Werema alisema lengo ni kuongeza adhabu ya faini kwa makosa ya kutumia lugha za matusi na uchochezi zinazoweza kusababisha machafuko nchini.
 
© 2012. Design by Ernest James Siwigo Chambasi - Supported By John James Chambasi And Maganza Family