Wakati Serikali imewasilisha muswada wa marekebisho ya sheria
mbalimbali ikiwemo Sheria ya Magazeti, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni,
imepinga marekebisho ya sheria hiyo kwa madai kuwa hayakufanyiwa
tafakuri na utafiti.
Akiwasilisha maoni hayo bungeni jana, Msemaji wa Kambi hiyo kuhusu
Sheria, Tundu Lissu, alisema mapendekezo hayo yamefikishwa bungeni bila
kufanyia tafakuri au utafiti wowote.
“Mwanasheria Mkuu wa Serikali angefanya utafiti kidogo tu angegundua
kwamba kifungu cha 55 hakina na hakijawahi kuwa na, sababu yoyote ya
kuendelea kuwepo katika kanuni ya adhabu,”alisema .
Alisema hiyo inatokana na kifungu hicho hicho kutungwa upya, kwa
maneno yale yale, kama kifungu cha 31 cha Sheria ya Magazeti kwamba
kifungu hicho hakikupaswa kuwepo kwa sababu, makosa ambayo kifungu hicho
kinafafanua hayako tena kwenye kanuni ya adhabu na badala yake, yako
katika Sheria ya Magazeti.
“Inaelekea katika fasta fasta ya kupitisha muswada wa Sheria ya
Magazeti, kifungu cha 55 kilisahauliwa katika kanuni ya adhabu wakati
vifungu vyote vinavyohusu makosa ya uchochezi na kashfa ya kijinai
vilipohamishiwa katika Sheria ya Magazeti,”alisema Lissu.
Alisema kwa sababu hiyo kambi yake inapendekeza kwamba mapendekezo ya aya ya 47 ya muswada huo yaondolewe.
“Na sasa, kwa muswada huu, badala ya kupendekeza sheria hii ifutwe
kama ilivyokuwa kwa Sheria ya Shihata na kama ilivyopendekezwa na Tume
ya Nyalali, Serikali hii ya CCM inaliomba Bunge lako tukufu kuiongezea
makali zaidi,” alisema.
Awali akiwasilisha muswada huo bungeni, Mwanasheria Mkuu wa Serikali,
Jaji Frederick Werema, alisema muswada huo unapendekeza kuongeza adhabu
ya faini kwa makosa ya kuchapisha habari za uchochezi ama habari
inayoweza kusababisha uvunjifu wa amani.
Jaji Werema alisema hivi sasa adhabu ya makosa hayo ni Sh 150,000
ambayo ni ndogo ikilinganishwa na madhara ya kosa husika kwa jamii.
“Muswada unapendekeza katika ibara ya 40 na 41 kuwa vifungu hivyo
virekebishwe kwa lengo la kuongeza adhabu ya faini kwa makosa hayo ili
adhabu hiyo isizidi Sh5 milioni,” alisema.
Jajin Werema alisema marekebisho hayo yanalenga katika kutekeleza
azimio la Bunge katika mkutano wa 11 kikao cha 21, ambapo pamoja na
mambo mengine Serikali ilitakiwa kupitia sheria zilizopo ili kuona kama
zinatosheleza kuzuia lugha au kauli za uchochezi.
Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala, iliunga mkono marekebisho hayo
yanayolenga kuongeza adhabu kwa makosa ya kutumia lugha za matusi na
uchochezi unaoweza kusababisha machafuko.
Wanasheria walonga
Baadhi ya wanasheria waliozungumza na gazeti hili wamesema
marekebisho yanayofanywa na Bunge, hayana maana kwa sasa na badala yake,
sheria nzima inapaswa ifutwe kwa sababu
hailengi kujenga bali kuvibana vyombo vya habari.
Mwanasheria wa kujitegemea, Aloyce Komba alisema ni wakati mwafaka wa
Serikali kurejea na kuridhia mapendekezo ya Tume ya Jaji Nyalali ya
kuzifuta sheria 40 zilizoainishwa na tume yake.
Alisema miongoni mwa sheria 40 zilizopendekezwa kufutwa na Jaji Nyalali, ni sheria ya magazeti ya mwaka 1976.
Ofisa Habari wa Mpango wa Kujitathmini Kiutawala Bora Afrika, Wakili
Hamza Abbas, alisema endapo Serikali inafanya marekebisho ya vifungu
ambavyo havitajwi katika kesi au shauri lililopo mahakamani, inakuwa
haijaingilia mahakama.
Source: Mwananchi
Source: Mwananchi