MOYES KUPATA KIUNGO SPAIN, MOURINHO ASHANGAA, WENGER HANA PRESHA!


MOYES-MOURINHO-WENGER

MAN UNITED KUTUMIA £20M KUMNUNUA KIUNGO LA LIGA
Imeripotiwa kuwa Mabingwa wa England Manchester United wako mbioni kumsaini Kiungo wa Valencia Ever Banega.
Ever Banega, Mchezaji kutoka Argentina mwenye Miaka 25, anatarajiwa kuuzwa na Klabu ya La Liga huko Spain, Valencia, ambayo inakabiliwa na ukata mkubwa wa Fedha kiasi ambacho wako tayari kumuuza kwa Bei nusu ya Kipengele cha Mkataba wake kinachotaka ilipwe Pauni Milioni 50 ikiwa atahama kabla Mkataba kwisha.
Ingawa Juventus, Tottenham na Arsenal pia zimeripotiwa kumfukuzia Banega, inadaiwa David Moyes ndie atashinda kumsaini Mchezaji huyo wa zamani wa Boca Juniors.
Banega amedumu Valencia kwa Misimu mitano hadi sasa lakini inasemekana anataka kuondoka ili kupata changamoto nyingine huku Moyes akitaka kuimarisha safu yake ya Kiungo ambayo inalegalega kutokana na kupwaya kwa Anderson, kutowika mfululizo kwa Tom Cleverley, kuugua kwa Darren Fletcher na kuwaacha Wakongwe Michael Carrick na Ryan Giggs wakisaidiwa na mpya Marouane Fellaini kuwa tegemezi kubwa.
Huko Spain, Banega anasifika kwa kuwa Kiungo imara anaegawa vizuri Mipira, mwenye akili ya Mpira na msomaji mzuri wa Gemu.
JOSÉ MOURINHO ASHANGAA MKUU WA MAREFA KUOMBA RADHI!
Meneja wa Chelsea, José Mourinho, amekiri kuwa ameshangazwa na hatua ya Mkuu wa Marefa, Mike Riley, kuomba radhi kwa West Bromwich Albion kwa Penati tata waliyopewa Chelsea katika Dakika za majeruhi iliyowapa Chelsea Sare ya 2-2 Timu hizo zilipotokutana Stamford Bridge Wiki mbili zilizopita.
Mourinho amedai Mike Riley, Kiongozi Mkuu wa Professional Game Match Officials Limited, Chombo cha Marefa huko England, ameweka mfano na mwanzo mbaya.
Mike Riley alimpigia Simu Meneja wa West Brom, Steve Clarke, mara baada ya Mechi kati ya Chelsea na West Brom ambapo Refa Andre Marriner alimwadhibu Beki Steven Reid kwa kudhani amemchezea faulo Ramires wa Chelsea na kutoa Penati tata iliyowapa Chelsea Bao la kusawazisha katika Dakika za majeruhi.
Mourinho amelalamika: “Nimeshangazwa, pengine kuanzia sasa Mike Riley atafanya hivyo hivyo kwa kila Klabu na Meneja.”
ARSENE WENGER HANA PRESHA KUSAINI STRAIKI JANUARI!
Bosi wa Arsenal, Arsene Wenger, amekiri kuwa ni ngumu kupata Mchezaji anaefaa kwa Mwezi Januari wakati Dirisha la Uhamisho litakapofunguliwa lakini amesisitiza kupona kwa Theo Walcott kumemuondolea presha ya kusaini Straika wakati huo.
Walcott, ambae alikuwa nje kwa Miezi miwili baada kufanyiwa upasuaji tumboni, yupo fiti kucheza Mechi yao ya Ligi Kuu England ya leo dhidi ya Timu yake ya zamani Southampton.
Lakini Arsenal inaendelea kumkosa Straika wao Lukas Podolski ambae anauguza Musuli ya Pajani na anatarajiwa kurudi dimbani mwishoni mwa Desemba.
Hali hii imewafanya Arsenal kumtegemea Olivier Giroud pekee huku Nicklas Bendtner akiwa Sentafowadi pekee kwenye Rizevu.
Akielezea hali hii, Wenger amesema: “Podolski bado hajarudi lakini tunae Theo ambae tunaweza kumtumia kama Straika anaezunguka ikiwa Giroud atakuwa nje lakini, mbali ya Bendtner, hatuna Sentafowadi mwenye ubavu. Bendtner ni mzuri ila hachezi Mechi nyingi na kichwani anafikiria kuhama.”
Hata hivyo, Wenger amekiri Mwezi Januari ni ngumu sana kupata Mchezaji anaefaa.
 
© 2012. Design by Ernest James Siwigo Chambasi - Supported By John James Chambasi And Maganza Family