MUHIDIN MAALIM GURUMO AUGUA GHAFLA, ALAZWA MUHIMBILI LEO

GWIJI wa muziki wa dansi mstaafu Muhidin Maalim Gurumo (pichani) ameugua ghafla mapema leo na kulazwa Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es salaam.

Wajumbe wa Kamati ya maandalizi ya Tamasha la Gurumo, Juma Mbizo na Said Mdoe, waliokuwepo Muhimbili, wameiambia Globu ya Jamii kuwa mwimbaji huyo mkongwe alipatwa na tatizo la shinikizo la damu na hali ikawa mbaya kabla ya kukimbizwa hospitalini hapo. Wamesema kwa sasa hali yake inaendelea vizuri na amelazwa katika wodi ya Mwaisela namba 1.

Wajumbe hao wamesema siku chache zilizopita Gurumo alikuwa kwenye afya njema na hata siku ya Jumanne alihudhuria kikao cha kamati hiyo kilichofanyika Vijana Social Hall Kinondoni.

Aidha, wajumbe hao wamedai kuwa kwa mujibu wa mke wa Gurumo, Bi Pili, ni kwamba hata jana mwimbaji huyo alikuwa hana tatizo lolote na alifanya mizunguko yake bila ya mikwaruzo yoyote.

Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya tamasha la Gurumo, Bi Asha Baraka amewataka wapenzi wa muziki kuwa watulivu kwa vile hali ya mwanamuziki huyo aliyeitumikia fani kwa miaka 53, inaendelea vizuri. 
Tamasha la Gurumo limepangwa kufanyika tarehe 14 mwezi ujao katika viwanja vya TCC Club Chang’ombe. Tumuombee dua mzee wetu Gurumo.
 
© 2012. Design by Ernest James Siwigo Chambasi - Supported By John James Chambasi And Maganza Family