HABARI KUTOKA HABARILEO MEDIA
MABINGWA wa soka Tanzania Bara, Yanga wamemtosa kipa na nahodha wa
Simba, Juma Kaseja na badala yake kuamua kumsajili aliyekuwa kipa wa
Azam FC, Deogratius Munishi ‘Dida.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Abdallah
Bin Kleb, Dida amesajiliwa baada ya ushauri wa Kocha Mkuu, Ernie Brandts
na kipa namba moja wa mabingwa hao, Ally Mustafa.
Katika mahojiano na blogu ya BIN ZUBEIRY jana, Bin Kleb alikiri kuwa
Kaseja alikuwa miongoni mwa mapendekezo ya majina ya kusajiliwa na
mabingwa hao, lakini akazidiwa na Dida.
“Lakini kabla ya kumsainisha, tuliomba maoni ya watu mbalimbali
akiwemo kipa wetu namba moja wa sasa, naye akatoa baraka zake kwamba
Dida ndiye anayefaa,” alisema Bin Kleb katika mahojiano hayo.
Alisema kulikuwa kuna baadhi ya maoni yakipendekeza Kaseja aliyetemwa
Simba baada ya kumalizika kwa mkataba wake, asajiliwe Yanga SC, lakini
baada ya uongozi kujadili, ukaona ni bora kufuata mapendekezo ya kocha
huyo Mholanzi kwa kumsajili Dida.
“Kulikuwa kuna majina ya makipa watatu, kati yao, wawili wote
wamekwishawahi kudakia Yanga, Kaseja na Benjamin Haule, lakini katika
majumuisho, Dida akawa ameshinda mchakato nasi tukamsainisha mkataba wa
miaka miwili jana (juzi) mchana,” alisema Mwenyekiti huyo.
Alisema Dida aliyewahi pia kuidakia Mtibwa Sugar ya Manungu, Turiani,
anachukua nafasi ya Said Mohamed aliyeachwa baada ya kumaliza mkataba
wa miaka miwili. Alisajiliwa kutoka Majimaji ya Songea.
“Dida ni kipa mzuri, ana uzoefu wa kutosha. Ni kipa ambaye amekuwa
akikubalika mbele ya makocha wengi wa timu ya taifa hapa nchini, tumeona
atatufaa na tumempa mkataba wa miaka miwili,” alisema.
Kipa huyo sasa atakuwa mbadala wa Mustafa ‘Barthez,’ aliyewahi kudaka
pamoja wakiwa katika klabu ya Msimbazi. Yanga inaye kipa mwingine, Yaw
Berko, ingawa siku zake Jangwani zinahesabika.
Kaseja alitangazwa kutoongezewa mkataba wake mapema wiki hii na
Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage, na tangu hapo taarifa zimekuwa
zikimhusisha na kuhamia Yanga, Azam na Coastal Union ya Tanga.

