WAKULIMA wa mahindi wilayani Muheza, mkoani Tanga wameiomba
serikali kuwakopesha tani 222 za mbegu inayoweza kustahimili bila
kuathiriwa na magugu ya kiduha.
Wakizungumza katika shamba la mfano lililopandwa mbegu, wakulima hao
walisema wanatumia nguvu nyingi kujikita katika kilimo, lakini wanavuna
mazao kidogo kutokana na magugu ya kiduha kuathiri mimea yao.
Walitoa ombi hilo katika mkutano wa wakulima ulioandaliwa na Kampuni
ya Tanseed International Ltd, uliokuwa na lengo la kuwapa uelewa wa
kutumia mbegu itakayohimili kiduha kutokana na eneo lao kuathiriwa na
magugu hayo.
Abeid Abdallah mwanakijiji wa Mafere, alisema wakulima wengi hawana uwezo hivyo hushindwa kununua mbegu hiyo.
Akiitolea ufafanuzi mbegu hiyo kwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Luteni
mstaafu Chiku Galawa, Mkurugenzi wa Tanseed International Ltd, Isaka
Mashauri alisema iwapo itatumika vizuri itatokomeza tatizo kabisa.
Akizungumza na wakulima hao, Luteni Galawa aliwataka kuongeza juhudi
za kilimo ili kuondokana na tatizo la utapiamlo, huku akiwataka kutumia
mbegu hiyo badala ya zile walizokuwa wakizitumia ambazo hazina wezo wa
kukabiliana na magugu ya kiduha.
Mbegu hiyo imetengenezwa kwa teknolojia mpya inayoweza kuua magugu ya
kiduha yanayonyonya chakula cha mmea na kuufanya ushindwe kutoa mazao
bora.
|