HAWA NDO WACHEZAJI WAWILI KATI YA HAMSINI WALIOULA KWENDA QATAR

WACHEZAJI wawili wa Tanzania wamechaguliwa miongoni mwa 50 waliofanyiwa majaribio Uganda ili kuingia katika kituo cha kuendeleza vipaji kilichoko Doha nchini Qatar kupitia mpango wa kukuza vipaji wa Aspire Football Dream.
Abdulrasul Bitebo (15) ambaye ni mshambuliaji kutoka Kituo cha Uwanja wa Karume, na Martin Tangazi (14) ambaye ni beki kutoka Kituo cha Ukonga, wamechaguliwa kutoka Tanzania kuingia katika kituo ambapo watakaa kwa mwezi mmoja kabla ya kusaini mkataba rasmi wa kuendelezwa.
Kwa mujibu wa taarifa ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), wachezaji wengine walikuwa wakitoka nchi za Uganda na Kenya. Mchezaji mwingine aliyefuzu katika nafasi tatu zilizokuwepo ni kutoka Kenya.
Mpango wa Aspire Football Dream unafadhiliwa na Mtoto wa Mfalme wa Qatar katika nchi 16 duniani, na kwa nchini, uko chini ya Idara ya Ufundi ya TFF. TFF ina jumla ya vituo 14 vya kuendeleza vipaji kupitia mpango huo wa Aspire Football Dream.
Vituo hivyo ni Karume, Kigamboni, Tandika, Kawe, Ukonga, Kitunda, Mbagala, Magomeni, Makongo, na Tabata vya mkoani Dar es Salaam, Bagamoyo kilichopo mkoani Pwani, Morogoro, Arusha na Moshi mkoani Kilimanjaro.
Kituo kingine cha kuendeleza vipaji cha Aspire kipo Dakar nchini Senegal.

 
© 2012. Design by Ernest James Siwigo Chambasi - Supported By John James Chambasi And Maganza Family