Watu
wawili wanashikiliwa na makachero wa Jeshi la Polisi kwa tuhuma za
kumshambulia kwa risasi Padre Ambrose Mkenda wa Parokia ya Mpendae
visiwani Zanzibar.
Naibu Mkurugenzi wa
Upelelezi Zanzibar, ACP Yusuf Ilembo, amesema Kunaswa kwa watuhumiwa
hao, kumefanikiwa baada ya juzi serikali kutuma makachero kutoka Bara
kuungana na wenzao wa Zanzibar kufanya uchunguzi wa kina kubaini
waliohusika na shambulio hilo la kinyama.
Padre Mkenda alipigwa risasi na watu
wasiojulikana siku ya Krismasi, nje ya nyumba yake majira ya saa 12
jioni, akitokea kanisani. Alishambuliwa akiwa ndani ya gari lake na
kuanguka.
Ilembo alisema polisi itahakikisha wale wote waliohusika watatiwa nguvu na kukabiliana na mkono wa sheria, watuhumiwa
hao ambao majina yao yamehifadhiwa kwa sasa kupisha uchunguzi,
wanaendelea kuhojiwa na makachero hao visiwani Zanzibar.
Ingawa uchunguzi wa serikali unaendelea, lakini wadadisi wa mambo ya siasa wanalihusisha tukio hilo na uhasama wa kidini.
Tukio la kushambuliwa kwa padre
huyo, linafanana na lile la kumwagiwa tindikali kwa Katibu Mkuu wa Mufti
Zanzibar, Sheikh Fadhil Suleiman.
Hata hivyo katika hali ya
kushangaza, hadi sasa hakuna mtu yeyote aliyeshikiliwa kuhusika na tukio
la Mufti kumwagiwa tindikali, ambalo kwa namna moja au nyingine, limekuwa likihusishwa na mitazamo tofauti ya kisiasa.
SOURCE:EMMANUEL SHILATU
