Marehemu Steven Kanumba
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
HII ni Jumamosi ya
mwisho kabla ya mwaka huu kumalizika na kuuanza mwaka mpya wa 2013. Ni
mwaka uliokuwa na matukio mengi katika sekta karibia zote.

Sharomillionea kabla ya umauti wake
Sio kisiasa,
kimichezo na kiutamaduni. Pande zote hizo zimeguswa na matukio ambayo
kwa kiasi Fulani yaliumiza watu na kuwaacha njia panda kwa kiasi
kikubwa.
Hapa nitaelezea
japo kwa ufupi matukio ya kisanaa na burudani hasa ya vifo yaliyotokea
kwa mwaka huu, ambayo kwa kiasi kikubwa yalitikisa katika viunga hivyo
nchini.
![]() |
| Add caption |
Mariam Khamis, enzi za uhai wake
Yalichanganya kiasi
kwamba hadi sasa, ukimuuliza mtu anayefuatilia sanaa nini anakumbuka
kwa mwaka huu, ni wazi atakwambia misiba isiyopungua mitano ya wasanii
wetu.
Misiba ambayo
imeacha pengo kubwa. Watu bado wanaendelea kulia na kuumizwa na misiba
hiyo. Tena misiba mingine mitatu imetokea ndani ya kipindi cha mwezi
mmoja ule wa Novemba.
Tuanze na msiba wa
kwanza uliogusa watu wengi na kulifanya jiji zima litetemeke. Kila
mdau wa sanaa aliumia. Si mwingine, bali ni msiba wa Steven Kanumba,
uliyotokea nyumbani kwake Sinza Vatcan, jijini Dar es Salaam, Aprili 7.
Kifo cha msanii
huyo wa filamu hapa nchini kilihuzunisha wengi. Siku ya Aprili 8,
takribani vyombo vya habari vyote viliripoti msiba huo na kufanyia
mwendelezo katika kipindi cha zaidi ya siku 30.
Msiba huo inadaiwa
ulitokana na ugomvi wa kimapenzi kati yake na msanii mwenzake
Elizabeth Michael, maarufu kama (Lulu), ambaye hadi leo yupo rumande.
Mwili wa Kanumba
uliagwa katika viwanja vya Leaders Club, kabla ya kuzikwa makaburi ya
Kinondoni, huku msiba wake ukivunja rekodi kutokana na kujaza watu
wengi.
Jiji zima
lilifurika watu. Tax zilifanya kazi pamoja na bodaboda zilizobeba watu
kuwatoa sehemu moja kwenda nyingine, hasa wale waliokuwa na haraka ya
kufika eneo la tukio.
Kwa mwaka huu,
msiba wa Kanumba ndiyo uliyokusanya watu wengi kwa mara moja, hasa
kutokana na umahiri wake katika kazi, akicheza filamu nyingi
zinazopendwa hadi leo.
Kanumba tayari
alishaanza kuvuka nje ya mipaka ya Tanzania kwa kucheza filamu zaidi ya
tatu za Kimataifa, ikiwamo ile ya Dar to Lagos.
Baada ya msiba huo
kupoa na watu kuendelea na maisha ya kawaida, mwishoni kabisa mwa
mwaka huu, msiba mwingine ulitokea katika tasnia ya taarabu, Mariam
Khamis kupoteza maisha.
Mwanadada huyo
aliyekuwa anafanya kazi na TOT Taarab, chini ya Malkia wa Mipasho
Tanzania, Khadija Omari Kopa, alifariki kutokana na matatizo ya uzazi
na kuacha kichanga.
Mwanadada huyu
alizikwa katika makaburi ya Magomeni Ndugumbi, ikiwa ni siku moja tu
baada ya kifo chake. Kutokana na imani ya dini yake ya Uislamu,
mwimbaji huyo alizikwa mapema.
Msiba wa Mariam
uligusa watu wengi katika tasnia hiyo ya taarabu, wakijitokeza watu
wengi wa kushiriki mazishi yake. Hata hivyo, bado hajaweza kufikia hata
robo ya watu waliomzika marehemu Kanumba.
Msiba wa Mariam
Khamis ulikuwa mzito kwa wadau wa taarabu hapa nchini, ukizingatia kuwa
alikuwa na mashabiki waliopenda kazi zake alipokuwa kwenye kundi hilo
linalomilikiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Wakati watu
wanaendelea kutafakari maisha ya sanaa na wasanii hapa nchini, wadau
walishtushwa na taarifa za msiba wa msanii wa zamani wa Kaole, Khalidi
Mohamed, maarufu kama Mlopelo, kilichotokea Novemba 23.
Msiba wa msanii
haujatingisha sana, labda ni kwasababu hakucheza nafasi zinazokaa
kwenye fikra za watu kichwani au maisha ya Kaole Sanaa Group yalivyokuwa
yakishuka kwa kasi.
Ilikuwa hadi mtu
amuelezee sana ndio mtu akumbuke sura yake au kumuona kwenye picha
yake. Hata hivyo pengo lipo, maana kila mtu ana umuhimu wake katika
jamii.

Msiba wa Mlopelo
bado ukiwa mbichi, taarifa za kifo cha John Maganga nazo zilisikika na
kuzidi kuwaacha watu kwenye maswali mengi wakiangalia namna gani habari
hizo zinakuwa nyingi kwa wasanii.
Taarifa za kifo
cha Maganga zilichanganya watu wengi, tangu Novemba 25, wakipishana siku
moja, ukingatia kuwa msiba huo ingawa haujafikia mshtuko wa Kanumba,
ila wengi walimjua na kuheshimu kazi zake za sanaa hapa nchini.
Moja ya kazi aliyocheza marehemu Maganga ni ile ya Mrembo Kikojozi iliyofanya vyema katika tasnia hiyo ya filamu Tanzania.

Msiba huu ulikuwa
ni wa Hussein Mkiety, maarufu kama Sharomillionea, uliyotokea Novemba
27 mwaka huu. Kijana aliyeibadilisha kabisa soko la sanaa ya vichekesho.
Wengi walizoea kuigiza wamevaa vinyago.
Lakini ujio wake
ukawa na matunda zaidi. Mwonekano wake wa usafi zaidi, lakini bado
alichekesha. Ni kazi nzuri. Marehemu Sharomillionea alikufa kwa ajali ya
gari wilayani Muheza na kuzikwa katika makaburi ya kijiji chao cha
Lusanga, wilayani humo.
Ukitaka kupanga
misiba iliyogusa hisia za wengi, basi huu wa Kanumba ulishika nafasi ya
kwanza na Sharomillionea akishika namba mbili, ingawa utaratibu huu ni
mchungu zaidi, maana kiubinadamu huwezi kufananisha kupendeza kwa
misiba.
Pamoja na vifo vya
wasanii hao, kazi zao, uwezo wao utaendelea kukumbukwa na wengi, huku
kazi iliyobakia ni kuwaombea kwa Mungu ili wakapumzike kwa amani.


