KWA idhini ya Fifa, Yanga itamrejesha kwa mara ya kwanza uwanjani straika wake, Emmanuel Okwi ambaye usajili wake ulikuwa na utata.
Benchi la ufundi limempa kazi moja tu kuipiga Ruvu Shooting na kupunguza nyodo za Azam inayopepea kileleni kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara.
Azam chini ya Kocha wake, Mcameroon, Joseph Omog ilikuwa na malengo mawili msimu huu, kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho na kutwaa ubingwa wa Bara. Lakini baada ya kuchemsha na kutolewa na Ferroviario ya Msumbiji, Straika wa Azam, Kipre Tchetche ameliambia Mwanaspoti kwamba sasa hasira zao ni kwenye Ligi Kuu na watapambana kiume wakianza dhidi ya Prisons kesho Jumapili kwenye Uwanja wa Chamazi.
Mechi ya Yanga leo Jumamosi ni muhimu kwao kusaka pointi za kuongoza lakini mashabiki wamepania kuona vitu vya Okwi aliyekuwa amezuiwa kucheza na Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) lililokuwa likitaka muongozo wa Fifa ambao waliwajibu kuwa Okwi ni halali.
Ruvu Shooting imembeza Okwi na imewapa
kazi mabeki wake wawili, Mbonosi Mangasini na Shaaban Sunza 'Chogo'
wahakikishe kwamba straika huyo hana madhara.
Mkenya Tom Olaba ambaye ni kocha wa
Ruvu alisema: "Eti kila mtu Okwi, Okwi kwani huyo Okwi ni nani. Hivi
huyo ni mtu spesho sana, Okwi, Okwi anaweza kucheza na wachezaji 11 wa
Ruvu, simhofii hata kidogo, nitakachokifanya ni kucheza na timu nzima na
si yeye mmoja."
Olaba hawajui wala hajawaona Yanga ila
atakachokifanya, ndani ya dakika 15 za mwanzo ni kuwasoma na
kuwadhibiti ingawa kocha msaidizi wa Yanga, Boniface Mkwasa aliifundisha
Ruvu mzunguko wa kwanza hivyo anajua kiufundi uwezo wa mchezaji mmoja
mmoja.
Kocha wa Yanga, Hans Van Der Pluijm
ambaye atawakosa, Mnyarwanda Haruna Niyonzima 'Fabregas' mwenye kadi
tatu za njano, Hussein Javu na Reliants Lusajo ambao ni majeruhi
alisema: "Tumejiandaa vizuri kuhakikisha tunashinda, timu ipo vizuri.
Coastal Union vs Mbeya City
Mbeya City itatokea Mombasa ilikokuwa
imeweka kambi ya muda kuja Tanga kuikabili Coastal Union ambayo kiwango
chao hakijauridhisha uongozi kutokana na matokeo hafifu ambayo
hayaendani na kambi waliyoweka Oman.
Noah tano za madiwani wa Jiji la Mbeya
na mabasi matatu ya mashabiki yaliingia Tanga jana Ijumaa usiku
kuisapoti timu yao katika mechi hiyo.
Azam inaongoza ligi hiyo na pointi 36,
Yanga ni ya pili ina 35, pointi sawa na Mbeya City inayoshika nafasi ya
tatu, wakati Simba ni ya nne ina pointi 32.
Mechi nyingine za ligi hiyo leo ni
Kagera Sugar na Rhino Kaitaba, Bukoba, Mtibwa Sugar na Ashanti Uwanja wa
Manungu, Morogoro, JKT Oljoro wataikaribisha Mgambo Shooting mjini
Arusha.
Mchezo miwili ya kesho Jumapili ni
Azam na Prisons, Dar es Salaam huku Simba ikicheza na JKT Ruvu. Kocha wa
Simba, Zdravko Logarusic alisema: "Tuna uhakika wa kushinda mechi hiyo
kwa sababu vijana wana ari ya ushindi, na hii ni kwa sababu watakuwa
kwenye uwanja wa nyumbani waliouzoea. Ni mechi muhimu sana kwetu kwa
vile tuko nyumbani na tunataka kumaliza kazi mapema."
Chanzo:Mwanaspoti mtandaoni