RAIS KENYATTA ARUHUSIWA KUTOHUDHURIA BAADHI YA VIKAO VYA KESI ICC

017113680_35400_1b04e.jpg
Mahakama ya ICC jana Ijumaa(18.10.2013)ilimruhusu kwa kiasi fulani Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta kutohudhuria baadhi ya vikao vya kesi dhidi yake, ili kumpa muda wa kushughulikia majukumu ya kisiasa.
Kenyatta , ambaye alichaguliwa kuwa rais mwezi Machi mwaka huu, amekuwa akidai kwa muda mrefu sasa kuwa kesi hiyo mjini The Hague itazuwia uwezo wake wa kuiongoza nchi.
"Mahakama hiyo kimsingi inamuondolea Uhuru Kenyatta ulazima wa kuwapo wakati wote katika kesi dhidi yake inayoanza Novemba 12, imesema mahakama hiyo ya ICC katika taarifa, lakini ikasisitiza kuwa ni lazima afike kwa ajili ya ufunguzi wa kesi hiyo.(P.T)
Majaji wamesema kuwa ruhusa ya Kenyatta inatolewa kwa misingi kwamba anaweze kutimiza majukumu aliyonayo kama rais wa Kenya, na sio kwasababu ya kutoa hadhi kwa kazi yake kama rais.
Atakuwapo wakati wa kutoa ushahidi
Mahakama hiyo iliyoko nchini Uholanzi pia inasisitiza kuwa Kenyatta anapaswa kuwapo wakati pande zote zitakapokuwa zinatoa taarifa zao za mwisho katika kesi hiyo, wakati wahanga wanatoa ushahidi wao na pia,iwapo kutakuwa na haja wakati wa kikao cha kutoa hukumu.
Kenyatta na makamu wake William Ruto wote wameshtakiwa na mahakama ya ICC kwa madai ya kupanga njama ya ghasia za kikabila ambazo zilisababisha kiasi watu 1,100 kuuwawa na zaidi ya watu laki sita kuachwa bila makaazi baada ya uchaguzi ambao uliingia katika mvutano mwaka 2007.
Kenyatta anakabiliwa na mashtaka matano ya uhalifu dhidi ya ubinadamu ikiwa ni pamoja na mauaji, ubakaji na kuwahamisha watu kwa nguvu kutokana na madai ya kuhusika kwake katika ghasia hizo. Atakuwa rais wa kwanza aliye madarakani kukabiliana na majaji wa ICC.
Ruhusa yasitishwa
Ruto, ambaye kesi yake ilianza mwezi uliopita , alipewa ruhusa kama hiyo akipewa nafasi kutokuwepo mahakamani kwa nyakati fulani , lakini uamuzi huo ulikatiwa rufaa na anatakiwa kuhudhuria vikao vyote hadi uamuzi kuhusu pingamizi iliyowekwa ya rufaa itakapoamuliwa.
Pia mwezi uliopita , mahakama ya ICC, ambayo ni mahakama pekee ya kudumu ya kuhukumu uhalifu mbaya kabisa duniani, ilikataa ombi la wakili wa Kenyatta kutaka kesi yake iahirishwe.
Wakifafanua kuhusu uamuzi huo , majaji wamesema mawakili wa Kenyatta walipewa muda wa kutosha kujitayarisha. Lakini tukio la siku nne za kuzingirwa kwa jengo la maduka ya kifahari mjini Nairobi la Westgate, ambapo watu 67 walipoteza maisha mwezi Septemba , limerejesha hali ya kuungalia uogozi wa Kenyatta na kufika kwake mbele ya mahakama hiyo ya ICC.
Ruto aliruhusiwa kwa muda kutohudhuria kesi dhidi yake ili kusaidia katika kushughulikia mzozo huo.
Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa Kenyatta hivi sasa yuko katika nafasi imara zaidi kudai kuwa yeye anapaswa kutoa uhakika kwa umoja wa Wakenya na kwa hiyo nchi hiyo inahitaji uongozi wake.
Aahidi kushirikiana na mahakama
Kenyatta pamoja na Ruto wamesema kuwa watashirikiana na mahakama hiyo, lakini rais hivi karibuni ameishutumu mahakama hiyo katika mkutano wa mataifa ya Afrika kuwa ni chombo cha "mabeberu na wabaguzi wa rangi".
Mjini Nairobi , mmoja kati ya washauri wa kisiasa wa rais Kenyatta jana Ijumaa(18.10.2013) amesema kuwa rais "ataendelea kutoa ushirikiano kwa mahakama ya ICC".
"Wakati nikizungumzia ushirikiano, ina maana ya mambo mengi," amesema Joshua Kutuny. "Lakini nataka kusema kuwa tutaendelea kutoa ushirikiano nao, (akiwa na maana ya ICC ) kwasababu ni ahadi tuliyoitoa wakati wa kampeni yetu wakati wa uchaguzi.
 
© 2012. Design by Ernest James Siwigo Chambasi - Supported By John James Chambasi And Maganza Family