Watoto watano wameuawa kwa bomu wakati walipokuwa wakichimba chuma chakavu katika eneo la mji mkuu wa Juba, Sudan Kusini.
Watoto hao walikuwa wakitafuta vyuma hivyo katika eneo la makazi ya zamani wanajeshi, msemaji wa Jeshi ameiambia BBC.Kuna operesheni maalum ya kufanya usafi katika maeneo mbalimbali ya Sudan Kusini, lakini milipuko imekuwa ikiua watu kila mwaka.
Watoto wenye umri kati ya miaka 10 na 14 wameuawa katika eneo la makazi ya wanajeshi ya zamani katika wilaya ya Souk Sita katika mji wa Juba, msemaji wa Jeshi Kanali Philip Aguer amesema.
Amesema raia wa Uganda aliyekuwa pamoja watoto hao akitarajia kununua vyuma hivyo chakavu naye amejeruhiwa.
Sudan Kusini ilipata uhuru mwaka 2011 baada ya muda mrefu wa migogoro na Sudan na kubakia miongoni mwa mataifa maskini sana duniani.