Waziri Mkuchika
akizungumza kwenye katika Semina ya Wahariri wa Vyombo vya Habari semina hiyo.
|
Baadhi ya washiriki wa
Semina.
|
Waziri Mkuchika akizungumza na wanahabari. |
(Picha zote na Hussein Makame)
Na Hussein Makame.
RAIS Jakaya Kikwete
ameongeza vyeo vya wa viongozi wa umma wanaowajibika na Sheria ya Maadili ya
Viongozi wa Umma ambao watapaswa mara moja kujaza fomu za kutangaza mali
walizonazo kila mwaka.
Hayo yamesemwa na
Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Jaji Mstaafu Salome
Kaganda katika Semina ya Wahariri wa Vyombo vya Habari iliyofanyika katika
hoteli ya Peacock jijini Dar es Salaam Septemba 12 mwaka huu.
Jaji Mstaafu Kaganda
alisema kuwa nyongeza hiyo iliyotiwa sahihi na Rais Kikwete Agosti 14 mwaka huu na tayari na imeshatoka
kwenye gazeti la Serikali, inaongeza wigo wa viongozi wa umma wanaotakiwa
kutangaza mali zao.
Alitaja vyeo vya
viongozi hao walioongezwa kuwa ni Msajili wa Hati, Wasajili Wasaidizi wa Hati
wa Kanda, Makamishna Wasaidizi katika Taasisi za Umma, Wakuu wa Hazina ndogo,
Wakuu wa Idara na Vitengo na sehemu za ugavi na manunuzi katika Wizara, Idara
za Serikali, Wakala wa Serikali na Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Wengine ni Mtendaji
Mkuu Shirika la Magazeti ya Serikali (TSN),Makanali wa Jeshi la Wananchi wa
Tanzania, Waratibu wa Miradi katika Wizara, Idara, Wakala na Taasisi za Umma,
Waganga Wakuu wa mikoa, Watendaji Wakuu wa Taasisi, Makatibu, Wakurugenzi na Mameneja
katika Taasisi za Umma.
Viongozi wengine walioongezwa
ni Msajili wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba, Wasajili Wasaidizi wa Baraza la
Ardhi na Nyumba wa Kanda, Wenyeviti wa Barza la Ardhi na Nyumba la Wilaya, Wakuu
wa Idara na Vitengo vya Serikali za Mitaa, Wakuu wa Polisi wa Wilaya(OCDs),
Wakuu wa Upelelezi wa Wilaya(OCCIDs), Wakuu wa Upelelezi wa Mikoa(RCOs),Maafisa
Usalama wa Wilaya na Mikoa.
Akizungumza katika
ufunguzi wa semina hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utawala Bora George
Mkuchika aliwaasa wahariri wa vyombo vya habari na waandishi kwa ujumla kutumia
kalamu zenu na midomo yao katika kuheshimu maadili ya kazi zao ili kutoa
mchango katika kuijenga Tanzania.
Alisema vyombo vya
habari vinayo fursa ya kuishawishi jamii kuendeleza yale mema yaliyo katika
jamii, hivyo aliwaomba wanahabari kuhakikisha kwamba wanatumia kalamu zao
kuendeleza umoja na amani nchini.
Naye Mkurugenzi wa
Idara ya Habari MAELEZO, Assah Mwambene aliviasa vyombo vya habari kuacha kuwa
sehemu ya kuendeleza ajenda za watu badala ya kutekeleza moja ya majukumu yao
ya kuweka ajenda zenye muelekeo wa kuijenga jamii ya Watanzania.
Akifafanua juu ya semina
hiyo, Waziri Mkuchika alisema semina hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa
kujenga uelewa kwa umma kuhusu Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma,
unaofadhiliwa na Shirika la Misaada la Marekani USAID.
“Lengo ni kuhakikisha
kuwa kila mdau wakiwemo waandishi wa habarai wanashiriki kikamilifu kuunga
mkono jitihada za Serikali kujenga misingi imara ya maadili na utawala bora ili
kuongeza kasi ya maendeleo endelevu katika nchi yetu” alisema Waziri Mkuchika
Alisema kuwa Sekretarieti
ya Maadili ya Viongozi wa Umma ni chombo kilichoundwa kikatiba kwa mujibu wa
Ibara ya 132 ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na kupewa dhamana ya
kusimamia maadili ya viongozi wa Umma iliyoainishwa katika Sheria ya Maadili ya
Viongozi wa Umma namba 13 ya mwaka 1995.
Alibainisha kuwa lengo
la Sheria hiyo ni kuhakikisha kwamba viongozi wa umma wanatekeleza majukumu yao
kwa namna ambayo wanadumisha na kukuza imani na heshima ya wananchi kwa Serikali
yao.
Akizungumzia vyeo vya
viongozi walioongezwa na Rais Kikwete kutangaza mali zao, Waziri Mkuchika
alisema kuwa Sheria imeweka kifungu kinachomruhusu Rais kuongeza idadi ya
viongozi wanaotakiwa kutangaza mali zao kila mwaka kwa kadri atakavyoona inafaa
kwani hawakuwepo wakati wa kutungwa sheria hiyo.
Mada zilizowasilishwa
kwenye semina hiyo ni Umuhimu wa Maadili katika Maendeleo ya Nchi, Sheria ya
Maadili ya Viongozi wa Umma na Majukumu ya Sekretarieti ya Maadili na Nafasi ya
Vyombo vya Habari Katika Kusimamia Maadili na Utawala Bora katika Jamii, ambayo
ilikuwa maudhui kuu ya semina hiyo.
SOURCE:GOVERNMENT OFFICIAL BLOG