Wakati Masogange akitozwa faini hiyo mwenzake Melissa Edward
ameachiwa huru na Mahakama hiyo baada ya kukosekana ushahidi wa kumtia
hatiani.
Msemaji wa Kitengo cha Uchunguzi wa Makosa ya Jinai cha Afrika
Kusini(Hawk), Kapteni Paul Ramaloko alisema Watanzania hao wameachiwa
huru baada ya kuonekana kuwa hawakubeba dawa za kulevya, bali kemikali
aina ya ephedrine.
Hata hivyo, Mahakama ilibaini kuwa, Melissa hana hatia kwa kuwa
ilionekana kuwa amemsindikiza Masogange, ambaye alimwomba amsaidie
kubeba mzigo huo.
“Mahakama iliona kuwa Melissa aliombwa tu kumsaidia kubeba baadhi ya
mabegi, lakini hayakuwa yake. Mizigo yote iliandikwa jina la Agness
Gerald na si Melissa,” alisema Kapteni Ramaloko.
Kapteni Ramaloko alisema, Melissa alijitetea kuwa hakuwa amesafiri
pamoja na Masogange bali walikutana ndani ya ndege na Masogange
alimwomba amsaidie kubeba mizigo hiyo, kwani ilikuwa mikubwa.
Kwa sheria za Afrika Kusini kubeba kemikali zozote ambazo zimepigwa
marufuku ni kosa la jinai kisheria, hivyo mahakama iliamuru Masogange
ahukumiwe kwenda jela kwa miezi 30 (miaka miwili na miezi mitano) au
alipe faini ya R30, 000 (sawa na Sh4.8 milioni).
Hata hivyo, Kapteni Ramaloko alisema mdhamini wa Masogange alilipa nusu ya fedha na kwamba zinazobaki amalizie baadaye.
Alisema kutokana na kutomalizia kulipa fedha hizo ataendelea kubaki
nchini humo hadi atakapomaliza kulipa nusu ya faini iliyobaki.
Masogange na mwenzake walipokamatwa na SARS ilielezwa walikuwa wamebeba dawa za kulevya aina ya
Methamphetamine, lakini Mahakama juzi ilithibitisha walikamatwa na kemikali aina ya Ephedrine, ambayo siyo dawa za kulevya.
Wakati Kamishna Mkuu wa Kitengo cha Kudhibiti Dawa za Kulevya nchini,
Geofrey Nzowa alipoulizwa na Mwananchi Jumamosi juzi alisema mzigo
walioubeba Masogange na mwenzake haukuwa ni dawa za kulevya bali ni
kemikali za dawa za kulevya, lakini Msemaji wa Mamlaka ya Mapato ya
Afrika Kusini, (SARS), Marika Muller alieleza kuwa timu ya SARS ina
uhakika kuwa mabegi sita yaliyokamatwa Julai 5 ni dawa za kulevya aina
ya Methamphetamine.