Na Waandishi WetuDar es Sakaam/Nairobi. Wakati
wa Jeshi la Polisi la Tanzania likisema linafuatilia taarifa za vitisho
za kundi la Al-Shabaab la Somalia za kushambulia, Mtanzania mmoja,
Vedasto Nsanzugwanko ambaye alijeruhiwa kwenye shambulio la Kenya
ameelezea yaliyomkuta.
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI),
Robert Manumba alisema jana kuwa wameanza kufuatilia kwa undani taarifa
zilizozagaa katika mitandao ya kijamii kwamba kundi la Al-Shabaab
linajipanga kuishambulia Tanzania na Uganda.
DCI Manumba alikiri kusikia taarifa hizo na kusema
kuwa Jeshi la Polisi limeanza kufanya uchunguzi wa kina: “Siwezi
kukueleza ni uchunguzi wa aina gani tutakaofanya, hiyo ni siri yetu.”
Hata hivyo, Msemaji wa Jeshi la Wananchi (JWTZ),
Meja Eric Komba alisema kuwa kuna uwezekano taarifa hizo zikapikwa na
wajanja wachache kwa ajili ya kuwajengea hofu wananchi.
“Taarifa za kwenye mitandao wakati mwingine ni
uzushi mtupu… kuna kipindi ziliwekwa taarifa za uongo zinazohusu jeshi
hili,” alisema.
Alipotakiwa kutoa msimamo wa jeshi hilo iwapo taarifa hizo zitakuwa na ukweli alisema, “Jeshi tuko tayari kwa jambo lolote.”
Mtanzania ajeruhiwa
Nsanzugwako ambaye ni Meneja wa Kitengo cha
Kulinda Watoto kwenye Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Watoto
(Unicef), Kenya alisema kwamba akiwa katika Hospitali ya Aga Khan,
Nairobi alipigwa risasi miguu yote miwili.
Alisema alifikwa na mkasa huo baada ya kupitia
katika maduka hayo akitokea kazini ili kupata kahawa... “Nilipofika
baada ya nusu saa nilisikia milio ya risasi ndipo nikaona purukushani
zimeanza.”
Nsanzugwako alisema alianza kukimbia na wenzake
huku wakijaribu kuokoa watoto waliokuwepo katika eneo hilo ambao
walikuwa katika shindano la mapishi lililoandaliwa na Radio Africa
Group.
“Watoto walianza kukimbilia ghorofa za juu zaidi na magaidi walianza kuwafuata.
“Baada ya hapo, waliendelea kutukimbiza na
nilikutana nao ana kwa ana na mmoja wa magaidi hao ambaye alinifyatulia
risasi na kunipiga miguu yote miwili,” alisema.
Mwananchi
Mwananchi