MCHEZAJI wa Yanga, Mrisho Ngassa ameomba wanachama na wapenzi wa Yanga kumchangia ili kurejesha fedha alizoilipa Simba.
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ilimuamuru Ngassa kuilipa
Simba Sh milioni 45 ambapo ni Sh milioni 30 alizochukua kama fedha ya
usajili na Sh milioni 15 kama fidia baada ya kusaini klabu mbili, Simba
na Yanga.
Mbali na kuamuriwa kulipa fedha hizo, Ngassa pia alifungiwa kutocheza
mechi sita za Ligi Kuu, adhabu iliyokwisha mwishoni mwa wiki iliyopita.
Ngassa aliichezea Yanga Jumamosi iliyopita dhidi ya Ruvu Shooting
ambapo alionesha kiwango kizuri na kutoa pasi iliyozaa bao lililofungwa
na Hamisi Kiiza.
Akizungumza kwa njia ya simu jana, Ngassa aliwaomba wanachama na
wapenzi wa Yanga walioguswa na kitendo cha kujilipia mwenyewe fedha hizo
wamchangie.
“Najua wapo wanachama wa naosononeka juu ya hilo, basi wanichangie
kupitia akaunti yangu namba 01J2095037800 ya benki ya CRDB ambapo
natumia jina la Mrisho Halfan Ngassa,” alisema.
“Naomba wanachama na wapenzi wa Yanga SC walioguswa kunichangia fedha
katika akaunti hiyo ili tuwe tumesaidiana kulipa deni hilo,” alisema.
Katika maelezo yake wiki iliyopita alipopeleka fedha hizo kwenye
ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Ngassa alidai Simba
haikumuweka wazi ilipomsainisha fomu za mkataba wake, kwani ilidai kuwa
anasaini mkataba wa mkopo kumbe haikuwa hivyo, badala yake alisaini
mkataba mpya wa kuichezea klabu hiyo.
Aidha, Ngassa aliwashauri wachezaji kuwa makini wanapoingia mkataba na klabu na kuwataka wawe na wanasheria ili kuwatafsiria
yaliyomo kwenye mkataba.
yaliyomo kwenye mkataba.