Waziri
Mkuu, Mhe. Mizengo Pinda akiwasisitizia wahitimu na wageni (hawako
pichani) waliofika katika mahafali ya kwanza na ya pili ya Chuo cha
Ufugaji Nyuki Tabora kuwa serikali lazima ijenge Chuo KIkubwa Cha
Ufugaji Nyuki Tabora.
======== ======= ========
Na Tulizo Kilaga, Tabora
|
SERIKALI
imeahidi kujenga chuo kikubwa cha mafunzo ya ufugaji nyuki katika eneo
la Chuo cha Mafunzo ya Ufugaji Nyuki mkoani Tabora ili kuhakikisha
Tanzania inakuwa nchi ya kwanza Barani Afrika katika uzalishaji wa mazao
yatokanayo na nyuki.
Ahadi
hiyo imetolewa mwishoni mwa wiki na Waziri Mkuu, Mhe. Mizengo Pinda
aliyekuwa Mgeni Rasmi katika mahafali ya kwanza na ya pili ya Chuo cha
Mafunzo ya Ufugaji nyuki Tabora alipokuwa akiwahutubia wahitimu kabla ya
kuwatunuku vyeti na zawadi.
Mhe.
Pinda alisema pamoja na mapungufu ya chuo hicho yaliyotokana na tabia
ya kuhamisha mafunzo yake mara kwa mara kwenda kwenye vyuo mbalimbali
vya Wizara ya Maliasili na utalii nchini, chuo kina umuhimu mkubwa
kutokana na kuwa ni chuo pekee katika Ukanda wa Afrika Mashariki na
Kusini mwa Afrika.
“Siku
za nyuma chuo kiliweza kupata watu kutoka nchi za nje kuja kujifunza,
hivyo serikali haiwezi kukiacha solemba! Kama tumeweza kujenga Chuo
kikubwa cha Serikali za Mitaa, Hombolo kinachotufanya tushindwe kujenga
chuo kikubwa hivi ni nini? Kwamba hatuoni thamani yake? Si kweli, miaka
kumi ijayo thamani yake itaonekana tu,” alisema Mhe. Waziri Mkuu.
Aliongeza
kuwa, tatizo la kutoendelezwa kwa chuo hicho wakati mwingine kunatokana
na viongozi kutojua kinachoendelea, hivyo aliomba uongozi kuwakilisha
mpango mkakati wake ili serikali iweze kuipembua na kuona wapi
pakuanzia.
Aidha,
Mhe. Pinda aliipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa uamuzi wake wa
kukirudisha Chuo cha Mafunzo ya Ufugaji Nyuki mkoani Tabora na kutoa
onyo kwa yoyote atakayetaka kujaribu kukihamisha tena kutofanya hivyo
ili serikali iweze kujipanga na kusonga mbele.
Aliongeza
kuwa, Tanzania ina hifadhi za misitu na maji ya kutosha inayotoa fursa
ya kuzalisha asali nyingi, hivyo amewaasa wananchi kuchangamkia fursa
hiyo ili kuiwezesha nchi kushika namba moja kwa nchi za Bara la Afrika
zinazozalisha asali.
“Tanzania
hivi sasa inapitwa na Ethopia kwa uzalishaji asali, nchi ambayo haina
misitu yakutosha, hili haliwezekani tuangalie mpango mikakati yetu.
Ufugaji asali hauhitaji mtaji mkubwa, na soko lake ni la uhakika,
tumshinde Ethiopia na hili linawezekana kama tutapanua mawazo yetu juu
ya sekta hii,” alisema Mhe. Pinda.
Kwa
upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Khamis
Kagasheki, alimshukuru Waziri Mkuu kwa moyo wake wakusimamia kidete
sekta ya ufugaji nyuki nchini na kutoa fursa za ajira kwa wananchi
wengi.
Aidha,
Mhe. Pinda alisisitiza kiu yake ya kuona Tanzania inazalisa asali
nyingi kwa kuwaahidi wahitimu kuwapa zawadi ya mizinga 100 endapo
wataunga na kuunda kikundi cha ufugaji nyuki na kutumia elimu waliopata
kuweza kujipatia kipato.
Katika
kusisitiza hilo Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Bi. Fatma Mwasa naye aliwahidi
wahitimu ambao ni wakazi wa mkoa wake, kuunda vikundi vya watu
waiopungua kumi kwa kikundi ili aweze kuwapatia mtaji wa mizinga.