Clinton alikagua miradi ya midogomodogo ya wananchi iliyo chini ya mfuko wake ikiratibiwa na kutekelezwa na Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Watoto (Plan) pamoja na Benki ya Barclays kupitia Vikoba.
Miradi aliyokagua ni pamoja na saluni za kinamama, ushonaji na chips ambapo pia alishuhudia mmoja wa wanachama wa vikundi hivyo akikabidhiwa mkopo wa Sh100,000 ambaye alieleza mbele ya Clinton kuwa atazitumia kwa mradi wa maandazi, hali iliyomfanya rais huyo na umati wa watu uliohudhuria kucheka.
Akizungumza katika ziara hiyo Clinton alizishauri benki nchini, kuwekeza kwenye vikundi vya kuweka na kukopa (Vikoba) akieleza kuwa ndiyo mkombozi kwa wananchi hasa wanawake.
“Nimekuwa kwenye miradi hii kwa miaka 30 kabla sijawa rais, hivyo basi najua umuhimu wake. Benki zinatakiwa zisaidie Vikoba kwani vikundi hivyo huwafikia wananchi kwa haraka na wepesi hivyo basi kunahitajika njia mbadala za kuhakikisha vinakuwa imara,” alisema Clinton na kuongeza;
“ Raha ya maendeleo ni kuona watu wanajitegemea wenyewe katika shughuli za kujiingizia kipato.”
Mmoja wa wananchi walionufaika, Zainab Paul ambaye ni mwanachama wa Kikundi cha Amani Hisa alisema kuwa kupitia Mfuko wa Bill Clinton na Vikoba ameweza kujikwamua kimaisha ikiwamo kumlipa mtoto wake karo ya shule.
“Kikundi chetu kina wanachama 30 na huwa tunanunua hisa kwa Sh2000 na kila mwanachama anaruhusiwa kukopa zaidi ya mara tatu,” alisema Paul.
Clinton alieleza kufurahishwa kwake na hatua walizofikia wakazi hao wa Vingunguti akiwapongeza kinamama kwa jitihada zao na baada ya ziara hiyo alielekea Ikulu kwa mazungumzo na Rais Jakaya Kikwete.
Awali, Mtendaji Mkuu wa Plan, Tanzania, Jorgen Haldorsen alisema shirika lake limekuwa likihudumia nyanja za kiuchumi na kijamii kwa lengo la kuhakikisha wananchi wa kada ya chini wanapata huduma mbalimbali ikiwamo afya.
Naye, Mshauri wa Mambo ya Kujikimu wa Plan Stella Tungaraza aliwataka wananchi kujiunga zaidi na Vikoba na kwamba shirika lake limepanga kuanza kutoa mafunzo ujasiriamali kwa vijana ili waweze kujikwamua kiuchumi.
Baadaye Rais Clinton alitia saini makubaliano ya taasisi yake ya Bill Clinton Foundation kusaidia sekta ya kilimo nchini.
Makubaliano hayo yalitiwa saini Ikulu jijini Dar es Salaam na Sophia Kaduma ambaye ni Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Chakula pamoja na mwakilishi wa taasisi ya rais huyo mstaafu, Walker Morris.
Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Clinton alisema wakulima wa Tanzania wanatakiwa kutambua kuwa kuna nchi nyingine zinashindwa kuendesha shughuli za kilimo kutokana na uhaba wa ardhi au kuwa na ardhi isiyokuwa na rutuba na kuwataka watumie fursa hiyo kukuza uzalishaji wa kilimo .
Alisema kama wakulima hao watajituma Tanzania inaweza kuzalisha chakula ambacho kinaweza kulisha dunia.
Na Bakari Kiango na Fidelis Butahe, Mwananchi