ISOME HUTUBA YA KAMBI YA UPINZANI ILIYOSOMWA NA TUNDU LISU,KATIBA NA SHERIA YAIBUA MAKUBWA BUNGENI

MAONI YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI, WIZARA YA KATIBA NA SHERIA,

MHESHIMIWA TUNDU A.M. LISSU (MB.)

KUHUSU

MPANGO NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA YA WIZARA YA KATIBA NA SHERIA KWA MWAKA 2013/2014
(Kanuni ya 99(9) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, 2013)


UTANGULIZI


Mheshimiwa Spika,


Ofisi ya Waziri wa Katiba na Sheria imeanzishwa kwa mujibu wa kipengele cha 12 cha Nyongeza ya Waraka wa Rais uliochapishwa kama Tangazo la Serikali Na. 494 la tarehe 17 Desemba 2010. Majukumu ya Ofisi hii yameainishwa katika Tangazo la Ukasimishaji wa Majukumu ya Kiuwaziri la mwaka 2010 (The Ministers [Assignment of Ministerial Functions] Notice, 2010) lililochapishwa katika Gazeti la Serikali kama Tangazo la Serikali Na. 494A la tarehe 17 Desemba 2010. Kwa mujibu wa Nyongeza ya Pili ya Tangazo hilo, pamoja na mengine, Ofisi ya Waziri wa Katiba na Sheria imekasimiwa majukumu ya masuala ya kikatiba, uendeshaji na utoaji wa haki, uendeshaji mashtaka na haki za binadamu. Kwa sababu ya matukio ya hivi karibuni yanayohusu utendaji wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba katika mchakato wa Katiba Mpya na kwa kuzingatia umuhimu wake katika mustakbala wa taifa letu, tunaomba kuanza na masuala yanayoihusu Tume na uendeshaji wake wa mchakato huo.


TUME YA MABADILIKO YA KATIBA NA MCHAKATO WA KATIBA MPYA


Mheshimiwa Spika,


Katika mwaka wa fedha 2012/2013, Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliidhinishiwa jumla ya shilingi bilioni 33.944 kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83 ya Sheria za Tanzania. Kwa mujibu wa Maelezo ya Makadirio ya Matumizi Mengineyo kwa Mwaka wa Fedha 2013/2014 yaliyoletwa mbele ya Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala mwezi uliopita, hadi kufikia tarehe 25 Februari, 2013 Tume ilishapokea shilingi bilioni 18.473 kutoka Hazina na ilikwishatumia shilingi bilioni 14.968, sawa na 81% ya fedha zilizopokelewa. Kwa mujibu wa Maelezo hayo, shilingi bilioni 3.504 ambazo hazijatumika zimetengwa kwa ajili ya kulipia madeni kutokana na huduma za uchapishaji wa Mwongozo wa Mabaraza ya Katiba, uratibu wa mchakato wa kupatikana Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba na gharama nyingine za uendeshaji wa Ofisi.


Maelezo ya Tume yanaonyesha kwamba shillingi bilioni 15.471 ambazo hazijatolewa na Hazina zitatumika kwa ajili ya kusambaza nakala milioni moja za Rasimu ya Katiba Mpya (shilingi bilioni 3.848); elimu kwa umma juu ya Rasimu ya Katiba Mpya (shilingi milioni 400); kuratibu na kuendesha Mabaraza ya Katiba kwa nchi nzima (shilingi bilioni 4.734); na shilingi bilioni 6.488 kwa ajili ya matumizi mengine pamoja na ‘stahili za Wajumbe na Sekretarieti.’


Mheshimiwa Spika,


Katika Maoni yetu ya mwaka jana, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ililalamikia kile ilichokiita “... matumizi yasiyoelezeka na yasiyokubalika ya fedha za umma hasa hasa katika mazingira ambayo wananchi wanahubiriwa na watawala kwamba miradi ya maendeleo yao ya kiuchumi na kijamii haitekelezeki kwa sababu ya ufinyu wa bajeti ya Serikali.” Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilidai kwamba shilingi bilioni 14.633 zilizotengwa kwa ajili ya kuwalipa wajumbe na watendaji wa Tume posho mbali mbali zilikuwa zinatishia kuigeuza “heshima ya kutumikia waliyopewa wajumbe wa Tume kuwa hongo ya Serikali.” Madai ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuitaka Serikali ieleze Bunge hili tukufu gharama zote za kila Mjumbe wa Tume, Sekretarieti na watumishi wengine wote wa Tume “ili Wabunge na wananchi wa Tanzania wafahamu kodi wanazolipa zinavyotumika katika mchakato wa Katiba Mpya” yalikataliwa na Serikali kwa hoja kwamba taarifa hizo ‘ni siri kati ya mwajiri na mwajiriwa.’


Mheshimiwa Spika,


Bunge lako tukufu linaombwa kuidhinisha shilingi bilioni 33.944, kiasi kile kile kilichoidhinishwa mwaka jana, kwa ajili ya matumizi ya Tume kwa mwaka wa fedha 2013/14. Kiasi hiki ni pamoja na shilingi bilioni 12.193 kwa ajili ya “... kulipia posho za vikao kwa Wajumbe wa Tume 34 na Sekretarieti 160 ...”; shilingi bilioni 1.728 ambazo “... zitalipia posho ya kujikimu kwa ajili ya Wajumbe na Sekretarieti wanaposafiri ndani ya nchi kikazi”; na shilingi bilioni 1.650 kwa ajili ya “... kulipa gharama za nyumba za Wajumbe na Sekretarieti wanaotoka nje ya Dar es Salaam.”


Aidha, kuna shilingi milioni 18 zinazoombwa “... kwa ajili ya kugharamia chakula kwa Wajumbe wa Tume na Sekretarieti watakaokuwa wamepata maambukizi ya ukimwi”; shilingi milioni 60 kwa ajili ya usafiri wa ndani; shilingi milioni 50 kwa ajili ya gharama za malazi kwa Wajumbe wa Tume na Sekretarieti ‘wanaposafiri kikazi’; shilingi milioni 423 kwa ajili ya ‘chai na vitafunwa’; na shilingi milioni 50 kwa ajili ya “... wahudumu wanaosaidia kazi za Tume wakiwa mikoani wakati wa kushiriki kwenye Mabaraza ya Katiba na zoezi la upigaji kura ya maoni.”


Vile vile, Mheshimiwa Spika, Bunge lako tukufu linaombwa kuidhinisha shilingi milioni 60 ya kulipia maji kwa matumizi ya ofisi za Tume; shilingi milioni 30 “... kwa ajili ya kulipia gharama za usafiri wa basi na taxi kwa Wajumbe na Sekretarieti watakaposafiri ndani ya nchi kikazi”; na shilingi milioni 103 kwa ajili ya kulipia gharama za simu za mikononi.


Mheshimiwa Spika,


Bunge lako tukufu linaombwa kuidhinisha posho na ulaji zaidi ya huu kwa ajili ya wajumbe na Sekretarieti ya Tume. Ulaji huu mwingine unajumuisha shilingi milioni 604 “... kwa ajili ya posho kwa Wajumbe wa Tume na Sekretarieti wakati wa Bunge Maalum la Katiba.” Maelezo ya Tume yamejaribu kuhalalisha matumizi ya fedha hizi za ziada kwa kuzibatiza jina la ‘hardship allowances’, yaani ‘posho ya mazingira magumu’, wakati vikao vya Bunge Maalum la Katiba vitafanyika Dar es Salaam au hapa Dodoma!


Vile vile, katika ulaji huu mpya zipo shilingi milioni 266 zinazoombwa “... kwa ajili ya chakula na viburudisho wakati wa vikao vya Bunge Maalum la Katiba”; shilingi milioni 12 nyingine “... kwa ajili ya huduma za chakula na viburudisho kwa shughuli zinazohusiana na Tume”; na shilingi milioni 185 kwa ajili ya kulipia “... usafiri wa basi na taxi....” Aidha, kuna shilingi milioni 30 za “... utengenezaji wa T-shirts na kofia kwa Wajumbe wa Tume na Sekretarieti wakati wa kushiriki kwenye zoezi za uhamasishaji kuelekea upigaji wa kura ya maoni”; shilingi milioni 40 nyingine kwa ajili ya “... utengenezaji wa sare wakati wa maadhimisho mbali mbali ya kitaifa”; na shilingi milioni 12 “... kwa ajili ya posho za kujikimu kwa watumishi wa Tume watakaohudhuria kwenye maadhimisho mbali mbali ya kitaifa....” Zaidi ya hayo, kuna shilingi bilioni 1.307 zinazoombwa kwa ajili ya “... posho za kujikimu kwa ajili ya Wajumbe na Sekretarieti ya Tume wanaposafiri ndani ya nchi wakati wa kushiriki kwenye zoezi la upigaji wa kura ya maoni”; na shilingi milioni 218 kwa ajili ya “... ununuzi wa mafuta ya magari ya Tume wakati wa kushiriki zoezi la uhamasishaji kuelekea upigaji wa kura ya maoni.”


Kwa ujumla, Mheshimiwa Spika, Bunge lako tukufu linaombwa kuidhinisha jumla ya shilingi bilioni 19.039 kwa ajili ya posho za aina mbali mbali na malipo mengine yanayowahusu Wajumbe na Sekretarieti ya Tume kwa mwaka wa fedha 2013/14. Hii ni zaidi ya 56% ya bajeti yote inayoombwa kwa ajili ya Tume. Kwa ulinganisho, posho na malipo mengine yanayowahusu Wajumbe na Sekretarieti ya Tume yalikuwa shilingi bilioni 14.633 au 43% ya bajeti yote ya mwaka wa fedha uliopita. Hii ina maana kwamba gharama za moja kwa moja za Wajumbe na Sekretarieti ya Tume zitaongezeka kwa zaidi ya shilingi bilioni 4.406 au zaidi ya 30% ya gharama za mwaka jana kama Bunge lako tukufu litaidhinisha maombi haya!


Mheshimiwa Spika,


Maombi haya ya mabilioni ya fedha za wananchi yanatoa uvundo na harufu mbaya ya ufisadi, na hayaelezeki na wala kukubalika kwa misingi ya kisheria, na kwa rekodi ya utendaji kazi wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Kwanza kabisa, kwa mujibu wa kifungu cha 7(1) cha Sheria ya Mabadailiko ya Katiba, Tume ina Wajumbe wasiozidi thelathini pamoja na Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wake. Kwa maana hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua uhalali wa maombi ya shilingi bilioni 12.193 kwa ajili ya posho za vikao kwa Wajumbe 34 wa Tume wanaotajwa katika kijifungu 210321 cha kasma 210300 kwenye randama ya Fungu 08 linalohusu Tume. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua Wajumbe hawa wanne wa ziada ni akina nani na wameteuliwa lini kuwa Wajumbe wa Tume? Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kuelezwa, inakuwaje Tume iwe na Wajumbe 34 wakati Sheria iliyoiunda inataka Tume yenye Wajumbe wasiozidi thelathini?


Pili, kwa mujibu wa kazi za Tume kama zilivyoainishwa katika kifungu cha 9 cha Sheria; na kwa mujibu wa utaratibu wa utendaji kazi wa Tume kama ulivyofafanuliwa katika Sehemu ya Nne ya Sheria; na kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 22(1) cha Sheria hiyo, Wajumbe na Sekretarieti ya Tume sio wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba. Badala yake, uhusiano pekee wa kisheria uliopo kati ya Tume na Bunge Maalum ni ule uliotajwa katika vifungu vya 20(3), 20(4) na 25(2) vya Sheria vinavyomruhusu Mwenyekiti wa Tume kuwasilisha Rasimu ya Katiba Mpya kwenye Bunge Maalum, na kuwaruhusu Mwenyekiti na wajumbe “... kutoa ufafanuzi utakaohitajika wakati wa majadiliano katika Bunge Maalum.”


Hii ina maana kwamba mara baada ya kuwasilisha Rasimu ya Katiba Mpya, Mwenyekiti wa Tume anakuwa functus officio, yaani hana kazi nyingine yoyote ya kufanya kwenye Bunge Maalum. Aidha, Mwenyekiti na Wajumbe wa Tume hawana kazi nyingine yoyote ya kufanya katika Bunge Maalum hadi hapo watakapohitajika na Bunge Maalum kwa ajili ya kutoa ufafanuzi wa jambo lolote linalohusu Rasimu ya Katiba Mpya. Wakishatoa ‘ufafanuzi utakaohitajika’ walioitiwa, nao pia wanakuwa functus officio. Kwa sababu hizo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua uhalali wa shilingi bilioni 1.055 ambazo Bunge lako tukufu linaombwa kuziidhinisha kwa ajili ya posho, chakula na viburudisho na usafiri wa basi na taxi kwa Wajumbe wa Tume na Sekretarieti wakati wa vikao vya Bunge Maalum la Katiba.


Tatu, kwa mujibu wa kifungu cha 33(2) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, jukumu pekee la Tume katika hatua ya uhalalishaji wa Katiba Mpya ni “... kutoa elimu ya uraia na uhamasishaji juu ya Katiba inayopendekezwa kwa muda usiozidi siku thelathini kuanzia siku ya kuchapishwa katika Gazeti la Serikali.” Kwa kazi ya mwezi mmoja tu Wajumbe na Sekretarieti ya Tume wanaombewa shilingi bilioni 1.307 kwa ajili ya posho za kujikimu. Kwa mahesabu hayo, kila Mjumbe wa Tume, Katibu na Naibu Katibu pamoja na wakuu wa vitengo saba vya Tume na madereva wa kila mmoja wao watalipwa wastani wa shilingi milioni 16.756 kwa mwezi huo mmoja, au shilingi 558,547 kama posho ya kujikimu kwa kila siku moja!


Mheshimiwa Spika,


Katika nchi ambayo wauguzi katika hospitali za umma wanalipwa mshahara wa kuanzia wa takriban shilingi 360,000 kwa mwezi; na walimu wa shule za msingi wanaanzia shilingi laki mbili na nusu na wale wa sekondari shilingi 325,000 kwa mwezi, malipo haya kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba yana uvundo na harufu mbaya ya rushwa kwa Wajumbe wa Tume! Hivyo basi, kwa vile kifungu cha 14(2) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kinatamka kwamba Wajumbe wa Tume na Sekretarieti “watalipwa kwa mujibu wa sheria na kanuni za nchi”, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali hii ya CCM iliambie Bunge lako tukufu ni sheria na kanuni zipi za nchi yetu ambazo zimetumika kuhalalisha malipo haya makubwa kwa Wajumbe na Sekretarieti ya Tume.


Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali hii ya CCM itoe kauli rasmi mbele ya Bunge lako tukufu kama kuna uhalali wowote wa kutumia fedha za wananchi wa Tanzania ili kununua ‘chakula maalum’ (special foods) kwa ajili ya Wajumbe na Sekretarieti ya Tume watakaopata ukimwi kwa sababu ya kuendekeza ngono zembe na starehe zao binafsi wakati wanatakiwa wafanye kazi ya Tume! Vinginevyo, Bunge lako tukufu lielezwe kwa ufasaha ni kwa namna gani mchakato huu wa Katiba Mpya unatazamiwa kusababisha maambukizi ya ukimwi kwa Wajumbe na Sekretarieti ya Tume!


Kwa Serikali kujificha nyuma ya pazia la ‘siri ya mwajiri na mwajiriwa’ hakutoshi tena, kwani ni kulizuia Bunge lako tukufu kutekeleza wajibu wake kikatiba wa kuisimamia Serikali chini ya ibara ya 63(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Sura ya 2 ya Sheria za Tanzania. Aidha, ni haki kwa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kujua uhalali wa malipo haya kwani, kwa mujibu wa ibara ya 63(3)(a) ya Katiba, Bunge lako tukufu “laweza kumuuliza Waziri yeyote swali lolote kuhusu mambo ya umma katika Jamhuri ya Muungano ambayo yako katika wajibu wake....”


Mheshimiwa Spika,


Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua shilingi milioni 218 kwa ajili ya ununuzi wa mafuta ya magari ya Tume zitatumikaje ndani ya kipindi cha siku thelathini za uhamasishaji na kuelimisha wananchi kupiga kura ya maoni kwa Katiba Mpya. Hii ina maana kwamba hata kama kila Mjumbe wa Tume, Katibu, Naibu Katibu na wakuu wa vitengo saba vya Tume watapewa gari moja kwa kila mmoja wao kwa kipindi hicho, kila gari itatumia wastani wa shilingi 186,325 kwa siku kwa ajili ya mafuta tu! Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua ni safari zipi hizo za Tume ambazo zitalazimu matumizi ya full tank ya mafuta kila siku kwa mwezi mzima? Huu, kama Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere alivyowahi kusema, ni ‘wizi mtupu’!


Mheshimiwa Spika,


Amlipaye mpiga zumari ndiye achaguaye wimbo. Baada ya Tume kulipwa mabilioni yote tuliyoyapigia kelele kwenye Maoni yetu ya mwaka jana, kuna ushahidi kwamba Tume imekuwa inacheza wimbo uliochaguliwa na CCM na Serikali yake. Mwezi Februari ya mwaka huu, Tume ilichapisha Mwongozo Kuhusu Muundo, Utaratibu wa Kuwapata Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya (Mamlaka za Serikali za Mitaa) na Uendeshaji Wake. Mwongozo huo ulisainiwa na Mwenyekiti wa Tume Jaji Joseph Sinde Warioba na ulianza kutumika tarehe 1 Machi, 2013. Ingawa Tume imedai kwamba Mwongozo huo ulitolewa kwa kuzingatia matakwa ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini kwamba Mwongozo ulitolewa kinyume na matakwa ya Sheria hiyo na kwa lengo la kuinufaisha CCM na washirika wake.


Mheshimiwa Spika,


Kifungu cha 17(8) cha Sheria kinailazimu Tume kubuni “... utaratibu unaofanana ambao utatumika katika kila upande wa Jamhuri ya Muungano katika ukusanyaji na uchambuzi wa maoni ya wananchi, uendeshaji wa mabaraza na uandaaji wa ripoti.” Katika utekelezaji wa majukumu yake, Tume inatakiwa kufuata msingi huu mkuu “isipokuwa kama mazingira yatahitaji vinginevyo....” Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inatambua kwamba, kwa kiasi kikubwa, Tume iliweka utaratibu unaofanana ambao ulitumika katika hatua ya ukusanyaji wa maoni ya wananchi katika kila upande wa Jamhuri ya Muungano.


Kwanza, Tume haikuweka utaratibu wowote wa maana wa kutoa elimu kwa wananchi juu ya masuala yote yanayohusu Katiba Mpya ili kuwaandaa wananchi kuchangia maoni yao kwa Tume wakiwa na uelewa wa kutosha. Badala yake, wakati wa mikutano ya Tume ya kupokea maoni ya wananchi, wajumbe wa Tume walipewa jukumu la kuwaeleza wananchi juu ya Katiba Mpya kwa muda usiozidi nusu saa. Hii ilifanyika katika mikutano yote ya Tume katika kila upande wa Jamhuri ya Muungano.


Pili, muda uliowekwa na Tume wa kukusanya maoni ya wananchi ulikuwa mdogo sana ukilinganisha na ukubwa wa nchi yetu na wingi wa Watanzania. Katika Majimbo karibu yote ya uchaguzi, Tume iliendesha wastani wa mikutano saba kwa kila jimbo kwa lengo la kukusanya maoni ya wananchi. Lakini huu ni wastani tu, katika majimbo mengi, Tume ilifanya mikutano minne au mitano tu. Hili pia lilifanyika katika kila upande wa Jamhuri ya Muungano.


Tatu, katika mikutano yote ya ukusanyaji maoni, wananchi walitakiwa kutoa maoni yao kuhusu Katiba Mpya kwa muda wa dakika tano kila mmoja na mikutano yenyewe ilichukua muda wa masaa matatu ikiwa ni pamoja na muda wa kutambulishana wajumbe wa Tume na mambo mengine yaliyo nje ya kuchukua maoni ya wananchi. Hii ilifanyika hata kwa Wabunge wakati Tume ilipokuja kuchukua maoni ya Wabunge hapa Dodoma. Utaratibu huu ulitumika katika kila upande wa Jamhuri ya Muungano. Aidha, utaratibu unaofanana katika kila upande wa Jamhuri ya Muungano ulitumika pia kukusanya maoni ya makundi maalum kama vile vyama vya siasa, taasisi zisizokuwa za kiserikali, mashirika ya kidini na hata taasisi za kiserikali na viongozi wake, wa sasa na waliostaafu.


Mheshimiwa Spika,


Wakati Tume iliweka utaratibu unaofanana katika kila upande wa Jamhuri ya Muungano wakati wa zoezi la kukusanya maoni ya wananchi, Tume hiyo hiyo iliweka utaratibu tofauti na wa kibaguzi katika hatua ya kuunda Mabaraza ya Katiba ya Wilaya. Kwanza, Tume iliweka ngazi mbili za uchaguzi wa wajumbe wa Mabaraza kwa upande wa Tanzania Bara wakati kwa upande wa Zanzibar Tume iliweka ngazi moja tu ya uchaguzi.


Hivyo, kwa mfano, aya ya 6.1.4 ya Mwongozo wa Tume imeweka Mkutano Mkuu Maalum wa Kijiji au Mtaa “ambao utakuwa na agenda moja tu ya kuwapendekeza kwa kuwapigia kura watu wanne ambao majina yao yatawasilishwa kwenye Kamati ya Maendeleo ya Kata.” Hii ni ngazi ya kwanza ya uchaguzi wa wajumbe wa Mabaraza kwa upande wa Tanzania Bara na kazi yake ni kupendekeza tu. Baada ya hapo majina ya watu walioshinda katika uchaguzi wa ngazi ya Kijiji au Mtaa yatawasilishwa kwa Afisa Mtendaji wa Kata “ambaye ataitisha Kikao Maalum cha Kamati ya Maendeleo ya Kata, ambacho ... kitachagua majina manne ...” ya wajumbe wa Baraza la Katiba la Wilaya. (aya ya 6.1.8, 6.1.9 na 6.1.10) Hii ni ngazi ya pili na ndiyo inayoamua nani awe mjumbe wa Baraza la Katiba la Wilaya kwa upande wa Tanzania Bara na nani asiwe.


Kwa upande wa Zanzibar, ngazi ya uchaguzi ni moja tu, Mkutano wa Shehia ambao, kwa mujibu wa aya 6.3.4 ya Mwongozo wa Tume, “... utakuwa na agenda moja tu ya kuwapigia kura ya siri watu watatu ... ambao majina yao yatawasilishwa kwa Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa au Katibu wa Halmashauri ya Mji au Wilaya ambapo Shehia hiyo ipo.” Kwa utaratibu huu, wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya kwa upande wa Tanzania Bara wamechaguliwa na watu wanne au watano tu ambao ni wajumbe wa WDC wakati wajumbe wa Mabaraza ya hayo kwa upande wa Zanzibar wamechaguliwa na watu wote walioshiriki katika Mkutano wa Shehia.


Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya kwa upande wa Zanzibar wana uhalali wa kisiasa kwa sababu wanawakilisha matakwa ya wananchi waliowachagua moja kwa moja bila mchujo, wakati wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya kwa upande wa Tanzania Bara hawana uhalali wowote wa kisiasa kwa sababu wanawakilisha maslahi ya CCM ambayo ndiyo inayotawala asilimia zaidi ya themanini ya WDC zote ambazo ndio zilizowachuja wajumbe hao.


Mheshimiwa Spika,


Eneo la pili linalothibitisha kwamba utaratibu wa Tume ni wa kibaguzi ni katika uendeshaji wa mikutano ya uchaguzi wa wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya. Kwa mujibu wa aya ya 6.1.4 ya Mwongozo wa Tume, kwa upande wa Tanzania Bara Mkutano Maalum wa Kijiji au Mtaa “... utaendeshwa na Mwenyekiti wa Kijiji au Mtaa, ambapo Afisa Mtendaji wa Kijiji au Mtaa atakuwa Katibu wa Mkutano na ndiye atakayewasilisha majina ya wananchi walioomba kuingia kwenye Baraza la Katiba la Wilaya.”


Hata hivyo, kwa upande wa Zanzibar kwa mujibu wa aya ya 6.3.5 ya Mwongozo wa Tume, “Mkutano wa Shehia utachagua Mwenyekiti na Katibu wa Mkutano huo kutoka miongoni mwa wananchi waliohudhuria Mkutano. Katibu ndiye atakayewasilisha kwenye Mkutano majina ya wananchi wote walioomba kuwa wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya....” Karibu Maafisa Watendaji wa Vijiji na Mitaa wote wa Tanzania Bara ni wanachama na makada wa CCM, ilhali zaidi ya 90% ya Wenyeviti wa Vijiji na Mitaa wote ni wanachama na makada wa chama hicho.


Kwa maana hiyo, mikutano ya uchaguzi wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya kwa upande wa Tanzania Bara imeendeshwa na makada wa CCM wakati kwa upande wa Zanzibar mikutano imeendeshwa na viongozi waliochaguliwa na wananchi walioshiriki katika mikutano hiyo bila kujali itikadi au uanachama wao katika vyama vya siasa. Ndiyo maana, karibu nchi nzima ukiacha Zanzibar, kwa mujibu wa taarifa ilizo nazo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, wananchi wengi wasiokuwa wanachama wa CCM ambao walipata kura nyingi katika kura za mikutano ya uchaguzi ya Vijiji na Mitaa walienguliwa kwenye michujo iliyofanyika katika Kamati za Maendeleo za Kata zilizowekwa kwa mujibu wa Mwongozo wa Tume.


Mheshimiwa Spika,


Hata mahali ambapo wananchi wasiokuwa wanaCCM walifanikiwa kupenyeza katika chekecheke la mchujo wa WDC wamefanyiwa mizengwe na wanaCCM ili waondolewe katika orodha ya wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya. Mfano mzuri ni yaliyomkuta Bw. Beatus Kipeya aliyechaguliwa mjumbe wa Baraza la Katiba la Wilaya ya Arusha Mjini kwa kupitia Kata ya Sombetini. Mara baada ya Bw. Kipeya kuchaguliwa kwenye kikao cha Kamati ya Maendeleo ya Kata ya Sombetini cha tarehe 8 Aprili, 2013, siku hiyo hiyo Katibu wa CCM Wilaya ya Arusha Allan G. Kingazi alimwandikia Mkuu wa Wilaya ya Arusha barua ya malalamiko juu ya kuchaguliwa kwa Bw. Kipeya.


Pamoja na kumpa Mkuu wa Wilaya ‘salaam za Chama’ chao, Katibu wa CCM Kingazi alilalamika kwamba Afisa Mtendaji wa Kata ya Sombetini amemruhusu “... raia wa Burundi Bwana Beatus Ndanyahubwi Kipea (ambaye katika kugombea ametumia jina la Beatusi Kipea ili asijulikane kama ni Mrundi – ila mtu wa Kigoma yaani Muha) kugombea nafasi ya Ujumbe wa Baraza la Katiba la Wilaya na akashinda, kinyume na maagizo ya Tume ya Katiba, kwamba Mjumbe ni lazima awe Raia wa Tanzania.”


Baada ya maelezo mengi kuhusu ‘Urundi’ wa Bw. Kipeya, Katibu wa CCM Kingazi anamwambia Mkuu wa Wilaya yafuatayo: “... (N)ashauri matokeo ya Uchaguzi wa Wajumbe wa Baraza la Katiba ufutwe na utangazwe upya. Aidha, Afisa Mtendaji huyo achukuliwe hatua za kinidhamu kwa kuvuruga kwa makusudi Uchaguzi wa Muundo wa Baraza la Katiba la Wilaya.”


Mheshimiwa Spika,


Kitu cha kwanza cha kushangaza kuhusu barua ya Katibu wa CCM Kingazi ni kwamba aliyetumiwa malalamiko ni Mkuu wa Wilaya ambaye, kwa mujibu wa ibara ya 42(3), 44(3) na 46(3) ya Katiba ya CCM Toleo la 1982, Mkuu wa Wilaya ni mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Wilaya, Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya na Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya. Kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na Mwongozo wa Tume, Mkuu wa Wilaya hana mamlaka yoyote kushughulikia jambo lolote linalohusu uchaguzi wa Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya. Kwa maana hiyo, sababu pekee ya Mkuu wa Wilaya ya Arusha kuandikiwa malalamiko haya ni kwa sababu ni kada wa CCM!


Mheshimiwa Spika,


Ukiacha Afisa Uhamiaji wa Mkoa wa Arusha, watu wengine wote walionakiliwa barua ya malalamiko ya Katibu wa CCM Kingazi ni makada wa CCM. Hivyo basi, nakala za malalamiko hayo zinaonyeshwa kupelekwa kwa Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Katibu wa CCM Mkoa, Mkuu wa Mkoa (ambaye pia ni mjumbe wa vikao vyote vya kikatiba vya CCM katika ngazi ya mkoa), Afisa usalama wa Taifa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Jiji la Arusha. Wote hawa hawahusiki kisheria kwa namna yoyote ile katika mchakato wa uundaji wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya. Chombo pekee ambacho kinahusika kisheria na mchakato wa kuunda Mabaraza hayo na ambacho kilitoa Mwongozo wa namna ya kuyaunda, yaani Tume, haikuandikiwa wala kunakiliwa barua ya malalamiko ya Katibu wa CCM Kingazi!


Mheshimiwa Spika,


Mara tu baada ya Afisa Uhamiaji Mkoa wa Arusha Bw. R. Gowelle kupata nakala yake, alimwandikia Bw. Kipeya barua ya ‘wito wa kufika ofisi ya uhamiaji Mkoa wa Arusha’, ambapo alimtaka kufika ofisini kwake ‘bila kukosa wala kutuma mwakilishi.’ Cha kushangaza ni barua hiyo imenakiliwa kwa Afisa Mtendaji Kata ya Sombetini, Mwenyekiti wa Mtaa wa Kirika A, Sombetini na Balozi wa Mtaa wa Zurich, Sombetini. Mbali na Afisa Mtendaji Kata ambaye alikuwa mlalamikiwa, wengine wote walionakiliwa barua ya Afisa Uhamiaji Mkoa ni makada wa CCM na, kwa taarifa za Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, ndio walikuwa chanzo cha malalamiko ya Katibu wa CCM Kingazi. Kwa taarifa za Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Bw. Kipeya ni raia halali wa Tanzania anayetoka katika Jimbo la Muhambwe katika Wilaya ya Kasulu ya Mkoa wa Kigoma. Dhambi pekee na kubwa aliyoifanya na kustahili kusumbuliwa na Idara ya Uhamiaji ni kugombea na kuchaguliwa kuwa mjumbe wa Baraza la Katiba la Wilaya ya Arusha wakati yeye sio mwanachama wa CCM.


Mheshimiwa Spika,


Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ina ushahidi unaoonyesha kwamba njama za kuhakikisha kwamba wanaCCM pekee ndio watakaochaguliwa kuwa wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya kwa upande wa Tanzania Bara zilipangwa katika ngazi za juu kabisa za CCM. Mnamo tarehe 3 Machi, 2013, siku mbili tu baada ya Mwongozo wa Tume kuanza kutumika, Katibu wa NEC ya CCM, Uhusiano wa Kimataifa Dr. Asha-Rose Migiro alituma barua pepe kwa wajumbe na watendaji wa Sekretarieti ya NEC ya CCM yenye kichwa cha habari: ‘MUHIMU!! MABARAZA YA KATIBA YA WILAYA.’


Barua pepe ya Dr. Asha-Rose Migiro inasema: “Naandika kuhimiza kazi ya kuwatia hamasa Makatibu wa Mikoa wasimamie kikamilifu mchakato wa kuundwa kwa Mabaraza ya Wilaya ya Katiba. Kama mnavyofahamu Tume ya Katiba imeshatoa taarifa rasmi kwenye vyombo vya habari ... kuhusu zoezi hili muhimu. Sambamba na hatua za awali tulizochukua baada ya kupata rasimu ya mwanzo ya Mwongozo wa Tume, hivi sasa tunatakiwa tuongeze juhudi za ushiriki wetu na kutayarisha makundi husika kama tulivyokwishaongea.”


Baada ya kuagiza ‘mawasiliano kati ya SUKI na Makatibu wa Mikoa’ kuhusu mambo ya kufanya, Dr. Asha-Rose Migiro alimalizia barua yake kwa maneno yafuatayo: “Tafadhali wanakaliwa msisite kutoa maoni, ushauri na mbinu bora zaidi za kutimiza azma yetu katika suala hili muhimu.” ‘Wanakiliwa’ wa barua pepe ya Dr. Asha-Rose Migiro ni pamoja na Mh. Mwigulu Nchemba, Mh. Zakhia Meghji, Mh. Muhamed Seif Khatib na Bw. Nape Nnauye, Katibu Mwenezi wa NEC ya CCM.


Siku moja baadaye, Nape Nnauye aliwaandikia ‘wanakiliwa’ wenzake kama ifuatavyo: “NASHAURI ikiwezekana kwa sababu ya unyeti wa swala hili tupate taarifa kila siku/au walau siku tatu ya HALI HALISI inavyoendelea katika kila mkoa, ni vizuri idara ikaandaa checklist ya mambo muhimu ya kupima kama mchakato unakwenda vizuri au la! Mfano ... idadi ya walioandaliwa kugombea katika kila eneo, idadi ya waliohamasishwa kuhudhuria na kupiga kura, n.k.”


Mheshimiwa Spika,


Njama za CCM kuteka nyara mchakato wa Katiba Mpya zinahusu pia mchakato wa uhalalishaji wa Katiba Mpya kwenye kura ya maoni. Mnamo tarehe 18 Desemba mwaka jana, Katibu wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Francis K. Mwonga, aliwaandikia barua Makatibu wote wa CCM wa Mikoa kuwapa ‘Maelekezo ya Kikao cha Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa na Makatibu wa CCM wa Mikoa Kilichofanyika Dar es Salaam Tarehe 10/12/2012.’


Sehemu ya Maelekezo hayo inasema: “Wakati wa kupiga kura ya maoni kuhusu Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mawasiliano yafanywe na wahusika ili vituo vya kupigia kura visiwe mbali sana na wananchi.” Maneno haya yameandikwa hata kabla Tume haijamaliza zoezi la kukusanya maoni ya wananchi na tayari Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM inawaelekeza makada wake mikoani kufanya mawasiliano na ‘wahusika’ juu ya namna ya kupanga vituo vya kupigia kura.


Mheshimiwa Spika,


Kwa mujibu wa kifungu cha 56(a) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 ya Sheria za Tanzania, mamlaka inayohusika kupanga vituo vya kupigia kura ni Msimamizi wa Uchaguzi, yaani Mkurugenzi wa Jiji, Mkurugenzi wa Manispaa, Mkurugenzi wa Mji na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya. Wasimamizi hawa wa uchaguzi wamelalamikiwa kwa miaka mingi na vyama vya upinzani kwa kupendelea CCM na wagombea wake katika chaguzi mbali mbali. Hawa ndio wanaotakiwa wawasiliane na Makatibu wa CCM Mikoa ili wapange vituo vya kupigia kura ya maoni juu ya Katiba Mpya!


Mheshimiwa Spika,


Mawasiliano haya ya viongozi wa ngazi za juu za CCM yanathibitisha kwamba mchakato wa Katiba Mpya umeiingiliwa na kuhujumiwa kwa kiasi kikubwa na CCM. Aidha, mawasiliano haya yanathibitisha kauli iliyotolewa mbele ya Bunge lako tukufu na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni wakati wa mjadala wa hoja ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwamba “...viongozi wa kiserikali kama vile Wakuu wa Wilaya na wa Mikoa waliwahamasisha wenyeviti wa vijiji, mitaa na madiwani kuhakikisha kwamba wagombea wote wasiokuwa wa CCM, hasa wa CHADEMA, wanaenguliwa katika chaguzi za vijiji, mitaa au kata.” Aidha, mawasiliano haya yanathibitisha kauli ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwamba Mabaraza ya Katiba ya Wilaya yaliyochaguliwa kwa utaratibu “...ni mabaraza ya CCM na sio mabaraza ya katiba ya Watanzania wote.”


Mheshimiwa Spika,


Yote ambayo tumeyasema hapa yanathibitishwa pia na Tume yenyewe. Tarehe 29 Aprili, 2013 Mwenyekiti wa Tume Jaji Warioba alikiri kwenye mkutano wa waandishi habari kwamba “... sehemu kubwa ya matatizo yaliyojitokeza yalisababishwa na misukumo na misimamo ya kisiasa na kidini.” Mwenyekiti Warioba amekiri kwamba kuna wajumbe wamejazwa katika Mabaraza ya Katiba ya Wilaya: “‘Hao waliojazana kwenye mabaraza wanadhani wanakuja kupiga kura, hapana.... Tume inazingatia uzito wa hoja zilizotolewa na wananchi na si idadi ya watu waliotoa maoni.’” Kwingineko, Mwenyekiti Warioba amekaririwa na vyombo vya habari akikiri kwamba kulikuwa na rushwa katika mchakato wa uchaguzi wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya. Hata hivyo, licha ya kukiri kuwepo kwa matatizo makubwa kama haya katika mchakato wa kuunda Mabaraza hayo, Mwenyekiti Warioba na Tume yake wamekataa madai ya kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi wa Mabaraza kwa hoja kwamba kufanya hivyo kutachelewesha kupatikana kwa Katiba Mpya!


Mheshimiwa Spika,


Kauli ya Mwenyekiti wa Tume ni ya kinafiki na ya kujikosha kutokana na makosa ya Tume yenyewe. Hii ni kwa sababu Tume yake ilitahadharishwa mapema juu ya uwezekano mkubwa wa matatizo hayo kujitokeza. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kiliitahadharisha Tume mapema mwezi Februari ya mwaka huu kwamba rasimu ya Mwongozo wa Tume itazaa mabaraza ya kiCCM na italeta manung’uniko mengi ya wadau ambao wataenguliwa kwenye ngazi ya WDC ambazo zinatawaliwa na CCM kwa kiasi kikubwa.


CHADEMA iliishauri Tume iachane na mapendekezo ya kuziweka WDC kuwa ni kikao cha uchaguzi wa wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya na badala yake wajumbe wa Mabaraza wachaguliwe moja kwa moja na wananchi kama ilivyopendekezwa kwa upande wa Zanzibar. Jaji Warioba na Tume yake walikataa kata kata mapendekezo haya ya CHADEMA. Kama alivyosema Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni: “... (L)icha ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kupatiwa maoni ya wadau kwamba utaratibu huo utaharibu mchakato wa Katiba Mpya, Tume ilikataa kata kata kuubadilisha Muundo wa Mabaraza haya. Ni wazi kwamba Tume inafahamu inachokifanya. Ni wazi vile vile kwamba Tume inafahamu matokeo ya hicho inachokifanya, yaani kuundwa kwa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya ambayo ni ya wanaCCM.”


Mheshimiwa Spika,


Jaji Warioba na Tume yake hawawezi wakasikika sasa hivi wakisema kwamba vyama vya kisiasa na taasisi za kidini ndio zenye makosa kwa kuvurugika kwa mchakato wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya! Aidha, Tume iliyotengeneza Mwongozo uliosababisha wanachama wa CCM ‘kujazana’ katika Mabaraza ya Katiba ya Wilaya haiwezi sasa ikalalama na kudai kwamba haitaangalia idadi ya waliotoa maoni bali itaangalia uzito wa hoja! Katika hili Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali iwaeleze Watanzania kama kuna uhalali wowote kutumia shilingi bilioni 4.734 kwa ajili ya kuratibu na kuendesha Mabaraza ambayo Tume imesema maoni ya wengi katika Mabaraza hayo hayatafuatwa.


Zaidi ya hayo, kukataa kwa Tume kufuta matokeo ya uchaguzi wa Mabaraza ambayo Tume yenyewe inakiri umevurugwa ni uthibitisho tosha kwamba ndivyo Tume ilivyodhamiria tangu mwanzoni. Mabaraza haya ya kiCCM ni matunda ya moja kwa moja ya Tume kukiuka utaratibu uliowekwa na kifungu cha 18(3) cha Sheria ulioilazimu Tume kuunda Mabaraza ambayo “... yatashirikisha na kuwakutanisha wawakilishi toka makundi mbali mbali ya wananchi katika jamii.”


Mheshimiwa Spika,


Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali itoe kauli mbele ya Bunge lako tukufu kama CCM au viongozi na makada wake wamefanya mawasiliano yoyote na vyombo vitakavyosimamia kura ya maoni juu ya Katiba Mpya kama zinavyoashiria nyaraka za CCM ambazo tumezielezea hapa. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali hii ya CCM itoe kauli juu ya uhalali wa mawasiliano haya wakati mchakato wa kutengeneza Katiba Mpya haujakamilika na wala sheria husika za uchaguzi hazijafanyiwa marekebisho ili kuruhusu kura ya maoni kufanyika kihalali, hasa kwa upande wa Tanzania Bara.


Mheshimiwa Spika,


Kifungu cha 10 cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kinafafanua kwamba “Tume itakuwa na mamlaka na uhuru kwa kadri itakavyokuwa muhimu kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu na mamlaka yake chini ya Sheria hii na haitaingiliwa na mtu au mamlaka yoyote.” Nyaraka za CCM ambazo tumezielezea hapa zinaonyesha dhahiri kwamba CCM imeingilia uhuru na mamlaka ya Tume. Kwa uchache kabisa, nyaraka hizi zinaonyesha viongozi wa ngazi za juu kabisa wa Sekretarieti ya NEC ya CCM wamefanya makosa ya kula njama kutwaa mamlaka ya Tume kwa kuwatumia Makatibu wa Mikoa wa CCM ‘kusimamia kikamilifu mchakato wa kuundwa kwa Mabaraza ya Wilaya ya Katiba.’ Kwa mujibu wa kifungu cha 21(2)(b) cha Sheria, “mtu yeyote ... atakayejifanya kuwa mjumbe wa Tume au Sekretarieti ... atakuwa ametenda kosa.” Kifungu cha 21(3) kinaelekeza adhabu ya faini isiyopungua shilingi milioni mbili na isiyozidi shilingi milioni tano au kifungo kwa muda usiopungua mwaka mmoja na usiozidi miaka mitatu au adhabu zote mbili, kwa mtu yeyote atakayepatikana na hatia na kosa hilo. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali hii ya CCM itoe kauli mbele ya Bunge hili tukufu kama iko tayari sasa kuwachukulia hatua tajwa za kisheria Dr. Asha-Rose Migiro, Mh. Mwigulu Nchemba, Mh. Zakia Hamdani Meghji, Mh. Muhamed Seif Khatib, Nape Nnauye na wengine wote waliotajwa katika nyaraka za CCM kwa uhalifu walioufanya dhidi ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.


Mheshimiwa Spika,


Baada ya ushahidi wote huu, hakuwezi kuwa na ubishi kwamba utaratibu mzima wa kuundwa kwa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya ni haramu. Hakuwezi kuwa na ubishi tena kwamba uharamu huu una lengo moja tu: kuhakikisha kwamba Katiba Mpya itakayopatikana kwa mchakato huu haramu “... itakuwa ni Katiba Mpya kwa jina tu, mambo mengine ya msingi yatabaki vile vile (yalivyo katika Katiba ya sasa). Kwa maneno mengine, itakuwa ni Katiba ile ile, ya watu wale wale, wa chama kile kile.”


Kama alivyosema Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni: “Katika mwaka wa kwanza wa mchakato wa upatikanaji Katiba mpya, Tume ya Mabadiliko ya Katiba imethibitisha hofu tuliyokuwa nayo toka mwanzo kwamba lengo la mchakato wa Katiba Mpya uliowekwa kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ni kuhakikisha kwamba mabadiliko pekee yakayokuwepo ni yale yenye kulinda matakwa ya CCM na Serikali yake au yale pekee yatakayokuwa na baraka za “‘status quo.’”


Mheshimiwa Spika,


Katika Maoni ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu hoja ya Ofisi ya Waziri Mkuu, tulitangaza kwamba CHADEMA itajitoa ushiriki wake katika mchakato wa Katiba Mpya endapo mambo yafuatayo hayatapatiwa ufumbuzi hadi kufikia mwisho wa mwezi huu, yaani tarehe 30 Aprili, 2013:


1. Kufutwa kwa uchaguzi wa wajumbe wa mabaraza ya wilaya ya Katiba uliofanywa na Kamati za Maendeleo za Kata, na badala yake wajumbe wa mabaraza ya katiba ya wilaya wachaguliwe moja kwa moja na wananchi wa Kata husika bila kuchujwa na WDC;



2. Serikali ilete mbele ya Bunge hili tukufu Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba yatayofanyia maeneo yafuatayo marekebisho:



(a) Vifungu vyote vinavyohusu uwakilishi katika Bunge Maalum la Katiba wa taasisi zilizoainishwa katika Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ili kuweka wazi namna wawakilishi wa taasisi hizo watakavyopatikana kutoka kila taasisi na idadi yao kwa kila taasisi;



(b) Vifungu vyote vinavyohusu ushirikishi wa wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kutoka Zanzibar katika mijadala inayohusu mambo yasiyokuwa ya muungano ya Tanzania Bara ili kuhakikisha kwamba wajumbe wa Zanzibar ambao hawatakuwa pungufu ya theluthi moja ya wajumbe wote watashiriki katika mijadala inayohusu mambo ya Muungano tu na sio mambo ya Tanzania Bara yasiyokuwa ya Muungano;



(c) Vifungu vyote vinavyohusu mamlaka ya Rais kuitisha tena Bunge Maalum la Katiba baada ya Bunge hilo kuwa limeshapitisha Rasimu ya Katiba Mpya kwa lengo la kufanya marekebisho katika Rasimu kabla haijapelekwa kwenye kura ya maoni ili kumwondolea Rais uwezo wa kubadilisha maamuzi yaliyopitishwa na Bunge Maalum;



(d) Vifungu vyote vinavyohusu mamlaka ya kikatiba na ya kisheria yatakayoiwezesha Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuendesha na kusimamia kura ya maoni ili kurekebisha hali ya sasa ambayo Katiba na Sheria za Uchaguzi za nchi yetu hazitambui uwepo wa kura za maoni na utaratibu wa namna ya kuiratibu, kuisimamia na kuiendesha;

Mheshimiwa Spika,

Madai ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni hayajatimizwa hadi tunatoa Maoni haya. Mwenyekiti wa Tume Jaji Warioba amesema wazi wazi kwamba uchaguzi wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya, ambayo Tume inakiri ulivurugwa na mivutano ya kisiasa na kidini, hautarudiwa na Mabaraza hayo yataendelea. Aidha, Mwenyekiti wa Tume amewaasa wale wanaolalamikia uchaguzi wa Mabaraza hayo wapeleke malalamiko yao kwenye Tume ili yashughulikiwe. Ushauri huu wa Tume hauna maana yoyote kwa sababu Mwongozo uliotolewa na Tume yenyewe haujaweka utaratibu wowote wa kufungua na kushughulikia malalamiko yoyote yanayotokana na uchaguzi wa Mabaraza hayo!


Mheshimiwa Spika,


Kwa upande wa Serikali, Waziri Mkuu aliahidi – wakati wa kuhitimisha hoja ya Ofisi ya Waziri Mkuu – kwamba Serikali italeta Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kabla ya mwisho wa Mkutano huu wa Bajeti. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imetafakari sana ahadi hii ya Waziri Mkuu. Pamoja na kwamba ni ahadi ya maneno tu, kama ilivyokuwa ahadi ya Mheshimiwa Rais Dokta Jakaya Mrisho Kikwete kwamba marekebisho yote yanayohitajika katika Sheria hiyo yatakamilika hadi kufikia Novemba 2012, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imeona ni vema iipe muda Serikali wa kuleta marekebisho tajwa ndani ya Mkutano huu wa Bunge la Bajeti. Kipindi hiki pia kitaenda sambamba na Tume kutoa Rasimu ya Kwanza ya Katiba Mpya kwa ajili ya kuanza kujadiliwa na Watanzania.


Mheshimiwa Spika,


Endapo hadi kufikia mwisho wa kipindi hicho Serikali itakuwa haijaleta Muswada wa marekebisho yanayotakiwa; au endapo Muswada utakaoletwa hautakidhi matakwa ya kuboresha mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya, basi CHADEMA itawaalika wanachama, wafuasi na mashabiki wake Tanzania nzima, pamoja na taasisi za kiraia na za kidini, vyama vya siasa na Watanzania wote wenye nia njema na taifa hili kuhamasisha Watanzania kuikataa Rasimu ya Katiba Mpya kwenye kura ya maoni itakayofanyika kwa ajili ya kuihalalisha Katiba hiyo.


Mheshimiwa Spika,


Nchi ya Kenya imepata Katiba Mpya mwezi Agosti 2010 baada ya mchakato uliochukua zaidi ya miaka kumi na moja. Kwa mujibu wa Dr. Patrice L.O. Lumumba aliyekuwa Katibu wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya Kenya, kwanza Serikali ya KANU chini ya Rais Daniel arap Moi, na baadaye Serikali ya NARC chini ya Rais Mwai Kibaki, zilijaribu kuteka nyara mchakato wa Katiba Mpya ya Kenya kwa kuandaa Rasimu ya Katiba Mpya ambayo ilipopelekwa kwenye kura ya maoni mwaka 2005 ilikataliwa na wananchi wa Kenya.


Kama inavyojulikana, baadaye Kenya ilifanya Uchaguzi Mkuu wa Desemba 2007 kwa mujibu wa Katiba ya zamani ya Kenya ya mwaka 1969. Matokeo ya uchaguzi huo chini ya Katiba ya zamani yaliingiza Kenya katika machafuko makubwa ya kisiasa yaliyosababisha mauaji ya maelfu ya Wakenya. Kwa sababu ya machafuko hayo, Kenya imeingia katika vitabu vya historia kuwa nchi ya pili katika Bara la Afrika, baada ya Hassan al-Bashir wa Sudan, yenye Rais na Naibu Rais walioko madaraka lakini wanakabiliwa na mashtaka ya uhalifu dhidi ya ubinadamu (crimes against humanity) katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai.


Mheshimiwa Spika,


Jamhuri ya Zimbabwe nayo imepata Katiba Mpya mwezi Februari ya mwaka huu baada ya mchakato uliochukua zaidi ya miaka kumi na sita. Mwaka 2000, Chama tawala cha ZANU PF cha Rais Robert Mugabe kiliwapelekea wananchi wa Zimbabwe Rasimu ya Katiba Mpya iliyotokana na mchakato uliotawaliwa na chama hicho kuanzia mwanzo hadi mwisho. Katika kura ya maoni iliyofanyika mwaka huo, Rasimu hiyo ya Katiba Mpya ilikataliwa kwa kura nyingi na wananchi wa Zimbabwe.


Matokeo yake, Zimbabwe iliingia katika giza kuu la machafuko ya kisiasa na kijamii yaliyopelekea ukiukwaji wa kutisha wa haki za binadamu na hatimaye Zimbabwe kutengwa kimataifa kwa kufukuzwa katika Jumuiya ya Madola na kuwekewa vikwazo vya kiuchumi na kidiplomasia. Baadaye, ZANU PF iliyofikiria kwamba inaweza kutawala kwa mabavu ya kijeshi, ilipoteza wingi wake Bungeni na hatimaye ililazimika kufanya maridhiano na vyama vya upinzani na makundi mengine ya kijamii yaliyopelekea kusainiwa kwa Makubaliano Makuu ya Kisiasa (Global Political Agreement). Chini ya Makubaliano hayo, Bunge la Zimbabwe liliunda Kamati ya Katiba ya Bunge iliyokuwa na wajumbe sawa kwa kila kimoja cha vyama vikuu vya kisiasa vya nchi hiyo. Kamati hiyo ya Bunge, iliyokuwa na Wenyeviti Wenza Watatu, Makamu Wenyeviti Wenza Watatu na wajumbe tisa kwa kila chama, ndiyo iliyoandaa Rasimu ya Katiba Mpya ya Jamhuri ya Zimbabwe iliyopigiwa kura ya maoni na kupitishwa na wananchi wa Zimbabwe mwezi Februari ya mwaka huu. Baadhi ya wabunge wa Bunge lako tukufu walishiriki katika kura ya maoni hiyo kama sehemu ya ujumbe wa waangalizi wa Chama cha Mabunge ya SADC.


Mheshimiwa Spika,


Mifano ya Kenya na Zimbabwe inatosha kuwaonyesha kwamba wanajidanganya wale wote wanaodhani kwamba kuwa chama tawala chenye wabunge wengi na mabavu ya kijeshi inatosha kubaki madarakani hata kwa hila na uchakachuaji. Saa ya mabadiliko inapogonga, hakuna mabavu ya kijeshi wala usalama wa taifa wala mapesa mengi wala ukatili wa aina yoyote unaoweza kuzuia wimbi la mabadiliko hayo! Bunge lako tukufu litafanya vema kujifunza kutokana na historia ya wenzetu.


HIFADHI YA HAKI ZA BINADAMU


Mheshimiwa Spika,


Katiba ya nchi yetu inatambua na kuhifadhi haki za binadamu na wajibu muhimu. Sehemu ya Tatu ya Katiba yetu imefafanua haki hizo kwa kirefu. Kama sehemu ya jumuiya ya kimataifa, Tanzania vile vile imeridhia mikataba mbali mbali ya haki za binadamu kama vile Tangazo la Ulimwengu la Haki za Binadamu (Universal Declaration of Human Rights – UDHR), 1948; Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa (International Covenant on Civil and Political Rights – ICCPR), 1966 na Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiuchumi, Kijamii na Kiutamaduni (International Covenant on Economic, Social and Cultural Rights – ICESCR), 1966. Aidha, Tanzania ni mwanachama wa Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na za Wananchi (African Charter on Human and Peoples Rights – ACHPR), 1981.


Mheshimiwa Spika,


Licha ya kuwepo kwa msingi huu wa kikatiba na kisheria, hali ya haki za binadamu imezidi kuzorota kwa kiasi kikubwa katika nchi yetu kama ambavyo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imeelezea mara nyingi katika Bunge lako tukufu. Kwenye Maoni haya, Mheshimiwa Spika, tunaomba tufanye marejeo ya taarifa rasmi za kitafiti za mamlaka za umma za kiserikali na za taasisi zisizokuwa za kiserikali kuhusiana na matumizi ya nguvu za vyombo vya dola na jinsi ambavyo zinahatarisha haki za binadamu zilizohifadhiwa na Katiba yetu. Taarifa hizi rasmi zinahusu uchunguzi wa kifo au mauaji ya mwandishi wa habari Daudi Mwangosi katika Kijiji cha Nyololo, Wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa mnamo tarehe 2 Septemba, 2012, wakati akifanya kazi ya kukusanya habari kwa niaba ya Kituo cha Televisheni cha Channel Ten katika mkutano wa ndani ulioandaliwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).


Mheshimiwa Spika,


Ibara ya 18(b) na (d) ya Katiba inahifadhi haki ya kila mtu “... kutafuta, kupokea na kutoa habari bila ya kujali mipaka ya nchi”; na “... haki ya kupewa taarifa wakati wowote kuhusu matukio mbali mbali muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi na pia kuhusu masuala muhimu ya jamii.” Aidha, kwa mujibu wa ibara ya 22(1) inatamka bayana kwamba “kila mtu anayo haki ya kufanya kazi.” Kwa misingi hii ya kikatiba, Marehemu Daudi Mwangosi alikuwa na haki zote kisheria kukusanya habari katika mkutano wa CHADEMA katika Kijiji cha Nyololo siku alipouawa.


Mheshimiwa Spika,


Katiba yetu pia inatambua na kuhifadhi “... uhuru wa kukutana na watu wengine kwa hiari yake na kwa amani, kuchanganyika, kushirikiana na watu wengine, na kwa ajili hiyo kutoa mawazo yake hadharani na kuanzisha na kujiunga na vyama au mashirika yaliyoanzishwa kwa madhumuni ya kuhifadhi na kuendeleza imani au maslahi yake au maslahi mengineyo.” (ibara ya 20(1) Ni muhimu kutambua hapa kwamba ‘aya nyakuzi’ (clawback clauses) zilizokuwa zinaweka masharti na vizingiti vya ‘kwa mujibu wa sheria’ vilivyokuwa vinazuia raia kufaidi haki na uhuru unaotambuliwa na ibara za 18 na 20 viliondolewa na Sheria ya Marekebisho ya Katiba, Sheria Na. 1 ya 2005. Kwa maana hiyo, hakuna sheria nyingine yoyote inayoweza kufunga au kupunguza uhuru na haki zilizotolewa na vifungu hivi isipokuwa masharti yaliyoko kwenye ibara ya 30 ya Katiba yenyewe.


Mheshimiwa Spika,


Sehemu ya Kwanza ya Sura ya Sita ya Katiba inaunda Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na kuipa majukumu na mamlaka ya kuyatekeleza majukumu hayo. Kwa mujibu wa ibara ya 130(1) ya Katiba, majukumu ya CHRAGG ni pamoja na kuhamasisha hifadhi ya haki za binadamu na wajibu kwa jamii; kupokea malalamiko ya uvunjaji wa haki za binadamu na kuyachunguza; na, kama itabidi, kufungua mashauri mahakamani ili kuzuia uvunjaji wa haki za binadamu.


Mara baada ya mauaji ya Marehemu Mwangosi kutokea, Tume ya Haki za Binadamu ilifanya uchunguzi wa mazingira na sababu za mauaji hayo. Baada ya uchunguzi huo, Tume iliandaa Taarifa ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ya Uchunguzi wa Tukio Lililopelekea Kifo cha Daudi Mwangosi Kilichotokea Septemba 2, 2012 Kijijini Nyololo. Taarifa hiyo ilitolewa hadharani na kwa vyombo vya habari tarehe 10 Oktoba, 2012.


Mheshimiwa Spika,


Taarifa ya Uchunguzi inaeleza kwamba “... Tume ilizingatia zaidi masuala ya uvunjwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora. Hivyo basi, Tume ilitilia maanani Katiba ..., sheria mbali mbali na mikataba ya kimataifa na ya kikanda inayohusu haki za binadamu ambayo Tanzania imeridhia.” Katika uchunguzi wake Tume ilibaini mambo yafuatayo:


1) Tarehe 2 Septemba, 2012 CHADEMA kiliruhusiwa na Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Mufindi kufanya mikutano ya ndani na kuzindua matawi mapya. Lakini jioni ya tarehe 1 Septemba, 2012 Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa Michael Kamuhanda alizuia CHADEMA kufanya mikutano iliyoruhusiwa. Kwa mujibu wa Tume ya Haki za Binadamu, Kamanda wa Polisi wa Wilaya ndiye ‘“Officer in charge” wa polisi wa eneo husika kama sheria inavyotaka.’


2) Viongozi wa CHADEMA kilifanya mazungumzo na Mkuu wa Upelelezi wa Jinai Mkoa wa Iringa “... na kuruhusiwa kufungua matawi yao bila ya kuwa na mikutano ya hadhara.”


3) Msajili wa Vyama vya Siasa aliwaandikia barua viongozi wa vyama vya siasa kuwataka kusitisha shughuli zao kwa sababu ya sensa ya watu na makazi iliyokuwa inafanyika wakati huo.


4) Wakati shughuli ya uzinduzi wa tawi la Nyololo ukiendelea, Kamanda Kamuhanda alifika eneo hilo na kuamuru viongozi wa CHADEMA wakamatwe, na wafuasi wa CHADEMA walipinga kukamatwa kwa viongozi wao.

5) Kamanda Kamuhanda aliamuru kupigwa kwa mabomu ya machozi ili kuwatawanya wananchi waliokusanyika katika ofisi za tawi hilo la CHADEMA.

6) Baada ya mabomu ya machozi kupigwa, wananchi walitawanyika na kukimbia ovyo, lakini Marehemu Mwangosi “... alizingirwa na askari, aliteswa na hatimaye inadaiwa alipigwa bomu na kufa papo hapo.


7) Marehemu Mwangosi aliuawa umbali wa takriban mita 100 kutoka ilipo Ofisi ya CHADEMA tawi la Nyololo.


8) Katika tukio hilo wananchi kadhaa walijeruhiwa kwa mabomu, wakiwemo mwandishi wa habari wa gazeti la Nipashe Godfrey Mushi, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake CHADEMA Wilaya ya Mufindi, Winnie Sanga, na Mkuu wa Kituo cha Polisi Mufindi Asseli Mwampamba “aliyekuwa akifanya jitihada za kumuokoa marehemu Daudi Mwangosi.”


Kwa mujibu wa Taarifa ya Tume ya Haki za Binadamu, “... Tume imejiridhisha kuwa tukio la lililopelekea kifo cha Daudi Mwangosi limegubikwa na uvunjwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.” Taarifa ya Tume inafafanua kuwa, “... Tume imejiridhisha kuwa Jeshi la Polisi limevunja haki ... ya kuishi, haki ya kutoteswa na kupigwa, haki ya usawa mbele ya sheria na haki ya kukusanyika na kutoa maoni.”


Kuhusiana na amri ya Kamanda Kamuhanda ya kupiga marufuku mkutano wa CHADEMA, Taarifa ya Tume inasema kwamba katika utekelezaji wa majukumu yake, Kamanda Kamuhanda “... alikiuka Sheria ya Vyama vya Siasa ... kifungu cha 11(a) na (b) na Sheria ya (Jeshi la) Polisi ... kwa kuingilia kazi za OCD wa Mufindi na kutoa amri ya kuzuia shughuli za CHADEMA wakati yeye hakuwa ‘Officer in-charge’ wa polisi eneo husika. Kwa maana hiyo amri aliyoitoa haikuwa halali kwa kuwa ilitolewa na mtu ambaye hakuwa na mamlaka kisheria kutoa amri hiyo. Haya ni matumizi mabaya ya madaraka, hivyo ni ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.”


Mheshimiwa Spika,


Tume ya Haki za Binadamu ilihoji pia hatua ya Msajili wa Vyama vya Siasa John Tendwa kuwaandikia barua viongozi wa vyama vya siasa kuwataka kusitisha shughuli zao kwa sababu ya sensa. Kwa mujibu wa Taarifa ya Tume, hatua hiyo “... ilikiuka misingi ya utawala bora kwani maelekezo yaliyotolewa ndani ya barua hiyo yanakinzana na Sheria ya Takwimu, Na. 1 ya mwaka 2002 inayotoa fursa kwa wananchi kuendelea na kazi zao wakati wa sense....” Barua hiyo pia “... ni kinyume na Sheria ya Vyama vya Siasa ... inayotoa fursa kwa vyama vya siasa kufanya shughuli zake bila kuingiliwa.”


Katika hili ni muhimu kunukuu mapendekezo ya Tume ya Haki za Binadamu kwa kirefu: “Jeshi la Polisi na Msajili wa Vyama vya Siasa waepuke kufanya maamuzi au matendo yanayoibua hisia za ubaguzi au upendeleo miongoni mwa jamii wakati wanapotekeleza majukumu yao kisheria. Mfano, Jeshi la Polisi lilizuia mikutano ya CHADEMA kwa sababu ya sensa wakati huo huo ... CCM walikuwa wakifanya uzinduzi wa kampeni huko Zanzibar. Aidha, rai ya Msajili wa Vyama vya Siasa haikuzingatiwa kwa upande wa CCM Zanzibar huku CHADEMA walishurutishwa na polisi kutii rai hiyo.” Aidha, Taarifa ya Tume inasisitiza kwamba “demokrasia ya mfumo wa vyama vingi iheshimiwe na kulindwa.”


Mheshimiwa Spika,


Sio Tume ya Haki za Binadamu pekee iliyofanya uchunguzi wa mauaji ya Marehemu Mwangosi. Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), taasisi mbili huru zinazojihusisha na masuala ya habari Tanzania, nazo zilifanya uchunguzi wa pamoja. Taarifa yao inayojulikana kama Ripoti ya Timu Maalum ya Uchunguzi Iliyoteuliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Kuchunguza Mazingira Yaliyopelekea Kuuawa kwa Mwandishi wa Habari Daudi Mwangosi Septemba 2, 2012 Katika Kijiji cha Nyololo, Wilaya ya Mufindi, Mkoani Iringa, imeunga mkono Taarifa ya Tume ya Haki za Binadamu juu ya jambo hili.


Kwa mujibu wa Ripoti ya MCT/TEF, matokeo ya uchunguzi wao “... yanadhihirisha bila wasi wasi kwamba polisi kwa makusudi waliwavurumisha waandishi waliotoka Iringa wakati wakikusanya habari za shughuli za CHADEMA katika kijiji cha Nyololo. Zaidi ya hapo, Daudi Mwangosi mwenyewe aliuawa akiwa mikononi mwa polisi huku wakisimamiwa moja kwa moja na Kamanda ... Kamuhanda.” Ripoti inakubaliana na Taarifa ya Tume ya Haki za Binadamu kabla ya Mwangosi kuuawa, “... maelewano yalifikiwa katika ya RCO na maofisa wa CHADEMA, na kamanda (RCO) (aliwa)amuru maofisa wake kutotumia nguvu dhidi ya watu waliokusanyika kwenye ofisi ile.


Hata hivyo, hali hiyo maelewano ilibadilika mara baada ya Kamanda Kamuhanda kufika katika eneo la tukio. Kwa mujibu wa Ripoti ya MCT/TEF, “mashuhuda wanaeleza kuwa RPC alimwita RCO na kumuonya wazi kuhusu kushughulikia kwa amani masuala ya CHADEMA katika eneo la awali la utulivu.” Baada ya hapo, “inaelekea RCO alijitoa kuelekea eneo la umwagaji damu ... na hivyo usimamizi wa utoaji amri katika eneo la umwagaji damu ... ulibakia kwa mkuu wake ambaye ni RPC Michael Kamuhanda.”


Sawa na Taarifa ya Tume, Ripoti ya MCT/TEF inaweka lawama za vurugu zilizotokea Nyololo kwenye miguu ya Kamanda Kamuhanda: Vurugu zilianza pale Kamanda Kamuhanda alipoamuru kukamatwa kwa viongozi wa CHADEMA waliokuwepo. “Kufuatia amri hiyo ... polisi ... waliingia kwa nguvu katika ofisi ya CHADEMA wakipiga mabomu ya machozi na kuwaamuru viongozi hao wajisalimishe.” Kwa mujibu wa Ripoti ya MCT/TEF, viongozi wa CHADEMA walitii amri hiyo na “... kujisalimisha kwa kuketi na kuinua mikono yao juu.” Hata hivyo, “... wakati makada wa CHADEMA walitii maagizo ya viongozi wao ya kuketi chini na kuinua mikono yao juu, polisi walifyatua risasi na mabomu ya machozi, na kuwapiga makada hao na waandishi kwa virungu.”


Mheshimiwa Spika,


Ripoti ya MCT/TEF inakubaliana na Taarifa ya Tume ya Haki za Binadamu juu ya jinsi Marehemu Mwangosi alivyouawa. “Alipoangalia nyuma, Daudi Mwangosi aliona kikundi cha polisi wakimpiga mwandishi mkuu wa gazeti la Nipashe wa Iringa, Godfrey Mushi.... Wakati mwandishi Godfrey Mushi akiwa bado anapigwa na polisi, marehemu Mwangosi aliwakimbilia akiwaomba waache kumdhuru zaidi Mushi kwa kuwa alikuwa mwandishi tu. Polisi hawakumsikiliza. Badala yake wakamburuta mwandishi huyo ambaye tayari alikuwa amepoteza fahamu na kumweka kwenye gari lao na wakamgeukia Daudi Mwangosi mwenyewe, wakampiga kwa nguvu mpaka akapoteza fahamu.”


Hata amri ya Mkuu wa Kituo cha Polisi Mafinga Mwampamba kuwataka askari polisi waache kumpiga marehemu Mwangosi haikusikilizwa na askari hao. Ili kujiokoa, marehemu Mwangosi alimkumbatia OCS Mwampamba na “baadaye kumwangukia miguuni mwake kuepuka kipigo zaidi.” Kwa mujibu wa Ripoti ya MCT/TEF, “picha za mgando zinaonyesha polisi mmoja akipiga bomu la machozi tumboni mwa marehemu Mwangosi kwa karibu kabisa.” Bomu hilo liliusambaratisha mwili wa marehemu Mwangosi aliyekufa papo hapo. Kwa sababu marehemu Mwangosi alikuwa chini ya miguu ya OCS Mwampamba, “naye pia alijeruhiwa vibaya.”


Mheshimiwa Spika,


Siku moja baada ya mauaji ya Daudi Mwangosi, Kamanda Kamuhanda alinukuliwa na vyombo vya habari akidai kwamba marehemu Mwangosi alifariki “kutokana na kitu kizito kilichotupwa na waandamanaji.” Aidha, siku iliyofuata Kamishna wa Operesheni wa Jeshi la Polisi Paul Chagonja alidai kwamba baada ya ghasia kudhibitiwa, marehemu Mwangosi alikimbilia walipokuwa polisi na “kitu kama bomu kikarushwa na kundi la watu wanaokimbia hovyo na kumlipua Mwangosi.”


Madai haya yanakanushwa na Ripoti ya MCT/TEF inayomnukuu shuhuda mwanamke aliyeshuhudia mauaji hayo na kubainisha kwamba marehemu Mwangosi “aliuawa chini ya usimamizi wa moja kwa moja wa RPC Michael Kamuhanda.” Ripoti hiyo pia imeelezea kwa kirefu jinsi Jeshi la Polisi lilivyotoa taarifa zinazokinzana juu ya kuhusika kwake na mauaji ya Mwangosi. Hivyo, kwa mfano, wakati Waziri wa Mambo ya Ndani Mheshimiwa Emmanuel Nchimbi alidai tarehe 4 Septemba 2012 kwamba marehemu aliuawa na bomu la machozi ambalo ‘halikulipuliwa kitaalamu na polisi’, Kamanda Kamuhanda alitokea kwenye televisheni siku iliyofuata “akitangaza habari za kuwatupia lawama wafuasi wa CHADEMA kwa kutupa kitu kizito kilicholipuka na kumuua Mwangosi....”


Mheshimiwa Spika,


Kwa miaka miwili mfululizo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imezungumzia kwa kirefu vitendo vya mauaji ya raia wasiokuwa na hatia ambavyo vimekuwa vinafanywa na vyombo vya dola hasa Jeshi la Polisi. Kama tulivyowahi kusema kwa kunukuu matokeo ya utafiti uliofanywa katika nchi za Afrika Mashariki na Mradi wa Haki za Binadamu wa Jumuia ya Madola na kuchapishwa mwezi Juni 2006, ‘“watu wa Tanzania … wanakabiliwa na tatizo la kuwa na jeshi la polisi ambalo mara nyingi lina sifa ya ulaji rushwa, matumizi ya mabavu na kuwa na chombo katili cha serikali.” Kwa mujibu wa utafiti huo, “aina hii ya uendeshaji wa shughuli za polisi inapingana na madai ya kuwepo kwa demokrasia yanayotolewa na serikali ya Tanzania.”


Mheshimiwa Spika,


Sasa Taarifa ya Uchunguzi wa Kifo cha Mwandishi wa Habari wa Channel Ten Bw. Daudi Mwangosi, iliyoandaliwa na Kamati iliyoundwa na Mheshimiwa Nchimbi na kuchapishwa tarehe 9 Oktoba 2012 imethibitisha ukweli wa kauli hii na ukweli wa madai ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni juu ya matumizi ya nguvu ya Jeshi la Polisi. Baada ya kuzunguka huku na huko ikijaribu kulisafisha Jeshi la Polisi, Taarifa ya Kamati hiyo inasema: “Hapakuwepo na uhalali wa kutumia Bomu la Kishindo kwani lengo la ulipuaji wake ni ili watu waogope na kukimbia.”


Aidha, Kamati hiyo iliyoongozwa na Jaji Mstaafu Stephen Ihema, inakiri kwamba “hapakuwepo umuhimu wa kutumia Bomu la Kishindo kwa sababu hata ingekuwa ukamataji tayari askari polisi wapatao sita walikuwepo eneo la tukio.” Kwa misingi hiyo, “… Kamati imeona kwamba … tukio la kuuawa Bw. Daudi Mwangosi na kuumizwa baadhi ya askari polisi halikustahili kabisa.”


Mheshimiwa Spika,

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali itoe kauli kama inakubaliana na matokeo ya taarifa hizi tatu zilizoandaliwa na taasisi za kiserikali kama vile Tume ya Haki za Binadamu, Kamati ya Jaji Ihema na MCT/TEF juu ya kuhusika kwa Jeshi la Polisi na mauaji ya marehemu Daudi Mwangosi. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali iteo kauli mbele ya Bunge lako tukufu kama inakubaliana na Taarifa ya Tume ya Haki za Binadamu kwamba kitendo cha Kamanda Kamuhanda kupiga marufuku mkutano halali wa CHADEMA kilikuwa ni kinyume cha Sheria ya Jeshi la Polisi, Sheria ya Vyama vya Siasa na ukiukwaji wa haki za binadamu na misingi ya utawala bora.

Vile vile, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali itoe kauli kama – baada ya ushahidi wa taarifa hizi tatu - iko tayari kuiomba radhi CHADEMA kwa kuisingizia kuhusika na kifo cha marehemu Daudi Mwangosi. Na mwisho, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali itoe kauli mbele ya Bunge lako tukufu kama iko tayari kuilipa familia ya marehemu Mwangosi fidia kwa mujibu wa sheria kwa kitendo cha Serikali kusababisha mauaji yake bila ‘uhalali.’

Mheshimiwa Spika,

Serikali na chama ambacho sera zake zinakiuka haki za binadamu na misingi ya utawala bora inapoteza uhalali (legitimacy) ya kuendelea kutawala. Hapa ndipo CCM na Serikali yake ilikoifikisha nchi yetu: waandishi wa habari wanauawa kwa sababu ya kufanya kazi yao halali ya kutafuta habari za mambo yanayohusu umma kama mikutano ya vyama vya siasa. Watanzania hawastahili Serikali ya aina hii. Kama alivyosema Baba wa Taifa katika kitabu chake Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania:


“Hatulazimiki kuendelea na uongozi mbovu wa Chama na Serikali. Wala tukiendelea na hali hii, bila kubadili uongozi wa Chama na Serikali, sina hakika kama tutafika huko salama. Masuala muhimu ya nchi yetu hayatashughulikiwa.... Na masuala mengine muhimu ... yataachwa yajitatue yenyewe. Nasema katika hali kama hiyo sina hakika kama tutafika salama; na tukifika salama tukiwa na uongozi huu huu wa Chama na Serikali mbele kutakuwa ni giza tupu. Majuto ni mjukuu, huja baadaye.”


Mheshimiwa Spika,


Baada ya maelezo haya marefu, naomba kukushukuru na wewe binafsi na naomba kuwasilisha.






---------------------------------------------------------------

Tundu Antiphas Mughwai Lissu
MSEMAJI & WAZIRI KIVULI, SHERIA, KATIBA NA UTAWALA
KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI
 
 
© 2012. Design by Ernest James Siwigo Chambasi - Supported By John James Chambasi And Maganza Family