MSANII wa muziki wa kizazi kipya nchini, Sara Kaisi ‘Shaa’, ameweka
wazi kuwa kiwango alichonacho sasa hakina tofauti na wasanii wengine
wakali kama ‘Ommy Dimpoz’ na Nassib Abdul ‘Diamond’.
Shaa aliyabainisha hayo jana wakati akifanya mahojiano na mwandishi
wa gazeti hili aliyekuwa akitaka kufahamu kiwango cha fedha anachokipata
msanii huyo katika maonesho mbalimbali anayoyafanya.
“Sasa kama mtu anaweza kumchukua Ommy ama Diamond kwa dau hilo
wanalopewa basi ujue huyo mtu anaweza pia kunichukua mimi kwa shoo zake
kwa kiwango cha nyota hao wawili, ni kwanini na mimi nisiwe na dau la
juu katika hiyo kazi wakati uwezo ninao,” alisema Shaa.
Alisema ili kudumu katika fani ya muziki wa kizazi kipya ni kuongeza
ubora kazi za sanaa kwa kufanya kazi na wadau mbalimbali wa muziki wa
ndani na nje ya nchi.
Shaa alisema kwa sasa wimbo wake wa Love Love unaoendelea kufanya
vizuri katika vituo mbalimbali vya radio unapendwa zaidi nchini na pia
Afrika Kusini, ambako video ya wimbo huo inachezwa zaidi.