Wagombea Urais Kenya Kupambana Katika Mdahalo
WAGOMBEA urais nchini Kenya wanatarajia kuumana
katika mdahalo utakaowakutanisha viongozi hao na kuoneshwa moja kwa moja
kupitia runinga. Mdahalo huo ambao ni wa kwanza kabisa katika historia
ya nchi hiyo na unaotarajiwa kupima uwezo wa wagombea hao juu ya masuala
muhimu ya kitaifa unafanyika wakati joto la kampeni likiwa juu hivi
sasa.
Mjadala huo ambao unafanyika baada ya juhudi za vyombo vya habari
nchini Kenya, unatarajiwa kufuatiliwa na mamilioni ya watu ndani na nje
ya mipaka ya Kenya kupitia njia za mitandao ya kijamii pamoja na
magazeti, huku vituo vinane vya televisheni, vituo 34 vya redio
vikitegemewa kuutangaza moja kwa moja tukio hilo.
Kwa awamu hii ya kwanza, mdahalo huo utajikita kuangalia masuala ya
uongozi, huduma za kijamii, afya na elimu pamoja na usimamizi wa
rasilimali bila ya kuliacha nyuma suala la usalama.
Wagombea sita wa urais – Uhuru Kenyatta, Raila Odinga, Musalia
Mudavadi, Martha Karua, Peter Kenneth na James Ole Kiyiapi – watapambana
kujibu masuali na kujieleza juu ya walivyojiandaa kuyatatua matatitizo
ya Wakenya katika ajenda zitakazojadiliwa.
Watangazaji watakaohusika kuwabana wagombea hao kujibu masuali
yaliyoandaliwa na jopo maalum la waandalizi wa mdahalo huo ni Linus
Kaikai kutoka kituo cha televisheni cha Nation na Julie Gichuru akiwa ni
mtangazaji wa kituo cha televisheni cha Citizen jijini Nairobi. Mdahalo
huo utakaoanza saa 1:30 magharibi kwa saa za Afrika Mashariki
utafanyika katika ukumbi wa shule ya kimataifa ya Brookehouse jijini
humo.
Bunge la mwanzo baada ya uchaguzi wa 2007 nchini Kenya. Mdahalo huo
unafanyika katika wakati ambapo tafiti za maoni zilizofanywa na
mashirika mbalimbali zikionesha kwamba matokeo ya uchaguzi mkuu
utakaofanyika tarehe 4 Machi yatakuwa ni ya kukaribiana kabisa, hasa
kati ya wagombea wakuu wawili – Raila Odinga kutoka muungano wa CORD na
Uhuru Kenyatta akishikilia bendera ya muungano wa Jubilee – huku
ikitajwa kuweko uwezekano mkubwa wa kufanyika duru ya pili.
Kwa mujibu wa mashirika ya kukusanya maoni ya Ipsos Synovate na
Infotrack wapiga kura ambao watafuatilia kwa makini zaidi mdahalo huo ni
wale ambao hadi sasa hawajaamua ni nani anayestahili kupigiwa kura
kuliongoza taifa hilo kubwa kiuchumi katika eneo la Afrika Mashariki.
Wadadisi wa mambo wanasema mdahalo huo wa kwanza kabisa kuwahi
kufanyika nchi humo unaweza kuwa chachu muhimu kwa wapiga kura juu ya
mtu wa kumpigia kura, ingawa mtazamo utakaojitokeza baada ya mdahalo juu
ya vipi matokeo ya uchaguzi yanavyoweza kuwa ni suala litakalotegemea
mambo mengi.
Lakini, juu ya hilo, wakati zikiwa zimesalia wiki tatu tu kufanyika
kwa uchaguzi huo mkuu na kukitarajiwa mdahalo wa pili tarehe 25
Februari, ni wazi mdahalo huo unaweza kabisa kuwashawishi wapiga kura
wengi kujitokeza kuitafuta hatma ya nchi yao. |