Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete usiku wa
jana, Alhamisi, Februari 7, mwaka huu, ametuma salamu za rambirambi kwa Mkuu wa
Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Askofu Mkuu Dkt. Alex Malasusa
kuombeleza kifo cha Askofu Thomas O. Laizer wa Jimbo la Kaskazini Kati Arusha
la KKKT aliyeaga dunia jioni ya jana.
Katika salamu zake, Rais Kikwete
amemwambia Askofu Mkuu Malasusa kuwa amepokea kwa mshtuko mkubwa na huzuni
nyingi taarifa za kifo cha Askofu Thomas Laizer ambaye amejulishwa kuwa ameaga
dunia, katika Hospitali ya Rufaa ya Selian, Arusha.
Rais Kiwete ameongeza kusema Askofu
Thomas Laizer ameaga dunia licha ya kwamba ataendelea kukumbukwa kama kiongozi
aliyetoa mchango mkubwa katika uongozi wa kiroho wa Watanzania na ambaye wakati
huo alitafuta namna bora zaidi ya kuwatumikia waumini wake.
Ameongeza Rais kikwete: “Kufuatia
msiba huu mkubwa, nakutumia wewe Baba Askofu Mkuu Alex Malasusa salamu za
rambirambi za dhati ya moyo wangu kukupa pole ya msiba huu na kupitia kwako
kuwapa pole nyingi maaskofu na viongozi wenzako katika KKKT pamoja na waumini
wote wa Kanisa kwa kuondokewa na kiongozi mwenzao na muumini mwenzao.”
Aidha, Rais Kikwete ameongeza,
“Pia
kupitia kwako Baba Askofu Mkuu, natuma salamu nyingi za moyoni mwangu kwa
familia na wana-ndugu wa Marehemu Thomas Laizer. Naungana nao katika kuomboleza. Naelewa
machungu yao katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na Baba, Babu na mhimili
wa familia. Nawaombea subira ili waweze kuvuka kipindi hiki kwa sababu yote ni
Mapenzi ya Mungu. Aidha, naungana nao katika kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa
Rehema, aiweke pema peponi roho ya Marehemu Thomas Laizer. Amen.”
Imetolewa
na:
Kurugenzi
ya Mawasiliano ya Rais,
IKULU
DAR ES SALAAM
07
Februari, 2013