AJALI YA JAHAZI LILILOZAMA ENEO LA NUNGWI,12 WAHOFIWA KUFA

Na Josephat Isango
WATU 12 wanahofiwa kufa maji, huku wengine 20 hali zao zikiwa mbaya baada ya jahazi moja lililokuwa linasafiri kutoka mkoani Tanga kwenda Pemba, kuzama katika mkondo wa bahari wa Nungwi.
Abiria hao 20 waliookolewa, inasemekana kuwa walikuwa hawawezi kuzungumza huku wanne kati yao wakidaiwa kuzidiwa zaidi na wote walimbizwa hospitalini.
Habari zilizolifikia gazeti hili jana jioni kutoka eneo la tukio zilisema kuwa jahazi hilo linalojulikana kwa jina la Sunrise lilizama mchana, kwa kile kinachodhaniwa kuwa ni upepo mkali uliosababisha mawimbi na hivyo maji kujaa katika chombo hicho na kisha kuzama.
Juhudi za kuwapata wakuu wa polisi visiwani Zanzibar kudhibitisha ajali hiyo ziligonga mwamba baada ya simu zao kuita bila kupokelewa, ingawa taarifa za awali zilisema kuwa jahazi hilo lilikuwa na abiria zaidi ya 35.
Taarifa za awali zilisema kuwa jahazi hilo lilisajiliwa mwaka 2010 kwa ajili ya kubeba mizigo na si abiria.
Hadi tunakwenda mitamboni, Tanzania Daima ilidokezwa kuwa vikosi vya KMKM pamoja na meli za wavuvi zilielekea eneo la ajali kwa ajili ya kutoa msaada wa uokoaji.
Tanzania Daima ilimtafuta msemaji wa jeshi la polisi Zanzibar lakini simu yake ilikuwa haipatikani.
Kwa mara nyingine tena visiwa vya Unguja na Pemba vinakumbwa na msiba mzito kutokana na kuzama kwa jahazi hilo la Sunrise huku ajali za meli za Mv Skagit na Spice Islenders zikiwa bado hazisahaulika.
Mv. Skagit ilizama Julai mwaka jana wakati inatoka jijini Dar es Salaam kwenda Zanzibar ikiwa na abiria zaidi ya 300 ambapo watu zaidi ya 100 walipoteza maisha.
Na Septemba mwaka juzi, meli ya Spice Islanders ilizama eneo hilohilo la Nungwi ikiwa safarini kuelekea Pemba ikitokea Bandari ya Malindi, Unguja na watu zaidi ya 240 kupoteza

 
© 2012. Design by Ernest James Siwigo Chambasi - Supported By John James Chambasi And Maganza Family