Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Said Meck Sadiki akitoa ufafanuzi kuhusu maadhimisho ya Wiki ya Maji mkoani Dar es salaam.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam
Mhe. Said Meck Sadiki akizindua mradi wa Maji ya Kisima mtaa wa
Mongolandege, Ilala jijini Dar es salaam wakati wa uzinduzi wa
maadhimisho ya Wiki ya Maji mkoani Dar es salaam. Mradi wa Kisima hicho
umegharimu kiasi cha shilingi milioni 78.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam
Mhe. Said Meck Sadiki akifungua moja ya bomba la maji la mradi wa Maji
ya Kisima mtaa wa Mongolandege, Ilala jijini Dar es salaam wakati wa
uzinduzi wa maadhimisho ya Wiki ya Maji mkoani Dar es salaam.
Bi. Martha Singano, Mkazi wa
Mongolandege akipokea ndoo ya maji kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es
salaam Mhe. Said Meck Sadiki mara baada ya kuzindua mradi wa Maji ya
Kisima katika mtaa huo.
…………………………………………………………………………………………………
Na. Aron Msigwa – MAELEZO.
.Dar es salaam.
Tanzania inaungana na mataifa
mengine duniani kuadhimisha Wiki ya maji kuanzia tarehe 16 hadi 22,
Machi 2015 chini ya Kauli Mbiu isemayo Maji kwa Maendeleo Endelevu.
Maadhimisho ya mwaka huu yanatoa
fursa kwa Mamlaka zinazohusika na usimamizi wa Maji nchini kutathmini
huduma wanayoitoa kwa wananchi, kujenga na kuimarisha miundombinu
iliyopo katika maeneo mbalimbali nchini.
Akizindua Maadhimisho ya Wiki ya
Maji kwa mwaka 2015 katika Mkoa wa Dar es salaam, Mkuu wa Mkoa wa Dar
es salaam Mhe. Said Meck Sadiki amesema maadhimisho hayo katika jiji la
Dar es salaam pamoja na mambo mengine yataambatana na Mamlaka ya Maji
Safi na Maji Taka (DAWASA) kuzindua miradi maji katika maeneo mbalimbali
ya jiji, kutoa elimu kuhusu utunzaji wa vyanzo vya maji, utunzaji wa
miundombinu ya miradi inayojengwa, upokeaji wa maoni na kero za wananchi
pamoja operesheni za kukamata baadhi ya watu wanaoiba na kuhujumu
miundominu ya maji.
Amesema maadhimisho hayo mkoani
Dar es salaam yatazindua miradi ipatayo 9 na kuweka mawe ya msingi
katika miradi 2 na kuongeza kuwa chini ya Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa
(BRN) mkoa unatekeleza jumla ya miradi 41 ya Visima vya maji katika
wilaya za Ilala, Kinondoni na Temeke.
Mhe. Saidi Meck Sadiki ameseama
miradi mingine 14 iliyojengwa chini ya ufadhili wa Serikali ya Ubelgiji
(BTC) imekamilika na inaendelea kuwahudumia wananchi katika wilaya zote
tatu za jiji la Dar es Salaam.
Amefafanua kuwa jiji la Dar es
salaam linaongoza nchini kwa kuwa na mahitaji makubwa ya maji huku
huduma ya Maji kwa wakazi hao ikitolewa na Mamlaka ya Maji ya jiji la
Dar es salaam (DAWASA) ambayo imekodisha shughuli za uendeshaji huduma
kwa DAWASCO. Vyanzo vikuu vya maji katika jiji la Dar es salaam mto
Ruvu, Kizinga pamoja na maji yanayopatikana chini ya ardhi.
Amesema mahitaji ya maji kwa
wakazi wa jiji na baadhi ya maeneo ya mkoa wa Pwani kwa sasa ni wastani
wa lita 450 kwa siku huku uwezo wa kuzalishaji maji kwa siku ni lita
300 ambazo ni sawa na asilimia 66.7 ya mahitaji yote.
Ameeleza kuwa upungufu huo
unaosababishwa na uwezo mdogo wa mitambo na miundombinu ya kuzalisha
maji na kuongeza kuwa Serikali kupitia sekta 6 zilizopewa kipaumbele
chini ya Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa, Maji yamepewa kipaumbele ambapo
miradi ya maji 41 mkoani Dar es salaam itatekelezwa ili kufikia lengo
la Serikali la uzalishaji wa lita 710 ambazo zitakua ni zaidi ya
mahitaji mwishoni mwa mwaka 2015.
“Matarajio yangu na mkoa
ninaouongoza ni kuhakikisha kuwa tunawapatia watu milioni 3.8 ambao ni
asilimia 90 ya wananchi katika jiji la Dar es salaam huduma ya majisafi
na salama mwishoni mwa mwaka 2015” Amesisitiza.
Ameleza kuwa DAWASA inatekeleza
mpango maalum wa kuongeza upatikanaji wa maji jijini Dar es salaam kwa
kupanua Mitambo ya Ruvu chini ambayo kazi yake imekamilika kwa asilimia
100, ujenzi wa bomba kuu kutoka Ruvu chini hadi chuo kikuu cha ardhi
ambao umekamilika kwa asilimia 93, kazi ya upanuzi wa mtambo wa Ruvu juu
na ujenzi wa bomba la maji hadi Kimara ambao umefikia asilimia 55
utakaokamilika mwezi Agosti, 2015.
Aidha, amesema kazi ya uchimbaji
wa visima 20 katika awamu ya kwanza imeanza na itakamilika mwezi Agosti
mwaka huu ikihusisha pia upanuzi wa mtandao wa usambazaji wa maji
katika maeneo yaliyo kandokando ya mabomba makuu kutoka Ruvu chini na
Ruvu juu na kunufaisha vitongoji vilivyopo kati ya mji wa Bagamoyo hadi
eneo la Tegeta-Mpiji na vitongoji vilivyopo kati ya mji wa Mlandizi
–Kiluvya na maeneo ya Mbezi, Kimara na Goba.
Awamu ya pili itahusisha upanuzi
wa mfumo wa usambazaji wa maji katika maeneo yote ya jiji yatakayopata
maji kutoka Kimbiji na Mpera na maeneo mengine ya jiji yasiyo na mabomba
ya usambazaji.
Akitoa ufafanuzi kuhusu mradi wa
visima vya dharula katika maeneo yasiyo na maji ya bomba amesema jumla
ya visima 48 vimechimbwa katika maeneo mbalimbali ya jiji yakiwemo
Kimara,Kimara, Kisukuru, Keko –Chang’ombe, Sandali, Mburahati, Mbagala,
Mtoni, Kigamboni ,Gerezani na Ukonga.
Katika hatua nyingine Mhe. Saidi
Meck Sadiki ameeleza kuwa Serikali itaendelea kuchukua hatua kali za
kisheria kwa baadhi ya watu wanaorudisha nyuma juhudi za Serikali za
kuwapatia wananchi maji safi kwa kuhujumu miundombinu ya maji ya DAWASCO
kwa kuendesha vitendo vya wizi wa maji, mambomba na miundombinu
mingine.
Pia ameitaka DAWASCO na Mamlaka
ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) kuanza kuwafuatilia na
kuwadhibiti baadhi ya wafanyabiashara wanaowaibia wananchi kwa kununua
maji ya DAWASCO kwa gharama nafuu ya shilingi 1 kwa lita na kuyauza kwa
zaidi ya shilingi 50.