Mkuu
wa Mkoa wa Dar es salaam, Saidi Meck Sadiki akizungumza na waandishi wa
habari kuhusu sherehe za maadhimisho ya kumbukumbu ya Mashujaa
zitakazofanyika kitaifa katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es
salaam.
Askari
wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wakiwa katika mazoezi
katika viwanja vya Mnazi Mmoja leo jijini Dar es salaam ikiwa ni sehemu
ya maandalizi ya mwisho ya sherehe za Kumbukumbu ya Mashujaa.
========= ========= =========
RAIS JAKAYA KIKWETE MGENI
RASMI SIKU YA MASHUJAA.
Na. Aron Msigwa –MAELEZO.
23/7/2014. Dar es salaam.
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Kikwete anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya kumbukumbu ya Siku ya Mashujaa itakayofanyika kitaifa katika viwanja vya
Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam.
Akizungumza na
waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam, Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam
Saidi Meck Sadiki amesema kuwa maadalizi ya sherehe hizo yamekamilika na
kuongeza kuwa maadhimisho ya mwaka huu kihistoria yanalenga kuwaenzi wote waliojitoa muhanga
katika jitihada za kuikomboa ardhi ya
Tanzania, kuilinda na kudumisha amani na utulivu uliopo.
Amesema maadhimisho hayo yatapambwa na shughuli mbalimbali
zikiwemo Gwaride la Kumbukumbu litakaloonyeshwa na Vikosi vya Ulinzi na Usalama
vya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Polisi, Jeshi la Magereza na Jeshi la
Kujenga Taifa (JKT).
Ameongeza kuwa katika
maadhimisho hayo kutakuwa na uwekaji na silaha za asili, maua kwenye mnara wa
kumbukumbu pamoja na viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini kutoa dua na sala
kuliombea taifa.
Bw. Sadiki amefafanua
kuwa shughuli zote katika viwanja vya Mnazi Mmoja zitaanza saa mbili Asubuhi na
kumalizika saa sita mchana, pia wananchi watakaohudhuria kumbukumbu hiyo
watapata fursa ya kushuhudia matukio yatakayokuwa yananendelea uwanjani hapo kupitia
Luninga kubwa zitakazokuwepo katika maeneo yote muhimu ya uwanja huo.
Aidha, katika hatua
nyingine ameeleza kuwa wakati wa maadhimisho hayo barabara ya Lumumba, Uhuru na Bibi Titi
zitafungwa kwa muda kwa lengo la kuhakikisha usalama kwa watumiaji wa barabara
hizo watakaohudhuria maadhimisho hayo.