Mtaalamu
kutoka Idara ya Nishati iliyopo chini ya Wizara ya Nishati na Madini Mhandisi
Nyaso Makwaya akisisitiza jambo wakati alipokuwa akiwasilisha mada kuhusiana na mikakati ya
Wizara katika kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi
Na Greyson Mwase, Morogoro
Wizara
ya nishati na madini inatarajia kuanzisha mpango wa taifa wa matumizi bora ya
nishati unaotarajiwa kuanza kutekelezwa
mara baada ya maandalizi yake kukamilika.
Akizungumza
katika kongamano la mabadiliko ya
tabianchi lililokutanisha wataalamu mbalimbali kutoka Wizara ya Nishati na
Madini, Ofisi ya Makamu wa Rais- Mazingira na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
linaloendelea mjini Morogoro, Mhandisi Nyaso Makwaya kutoka Idara ya Nishati,
Wizara ya Nishati na Madini alisema kuwa mpango huo uko katika hatua za mwisho
za ukamilishwaji wake.
Mhandisi
Makwaya alisema kuwa maandalizi ya mpango huo yalianza mwaka 2013 na kuongeza
kuwa lengo la mpango huu ni kuweka malengo ya kitaifa kwa kila sekta kwa ajili
ya matumizi bora ya nishati, kuzichanganua changamoto zilizopo za matumizi bora
ya nishati na kuzitafutia utatuzi na kuandaa miradi ya matumizi bora ya nishati.
“
Nishati ya umeme ni muhimu sehemu yoyote, inahitaji usimamizi bora hivyo mpango huu unalenga kuboresha matumizi ya nishati katika
sekta zote nchini, iwe viwanda, kilimo, ujenzi,mawasiliano n.k, mpango huu
unatoa dira sahihi kwa kila sekta” Alisema Mhandisi Makwaya Mhandisi
Makwaya aliongeza kuwa mpango huu
utapelekea uanzishwaji wa sheria na kanuni katika usimamizi wa matumizi
bora ya nishati.
Aliongeza
kuwa wadau na watekelezaji wakuu wa
mpango huo ni Wizara ya Nishati na Madini, Shirika la Umeme Nchini (TANESCO),
Mamlaka ya Udhibiti na Usimamizi wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) na
Shirika la Taifa la Viwango (TBS) ambao watajengewa uwezo na mradi huu.
Akizungumzia
changamoto zilizopo katika usimamizi wa matumizi bora ya nishati Mhandisi Makwaya alieleza kuwa ni kutokuwepo kwa kanuni zinazosimamia matumizi bora ya nishati katika ujenzi
na matokeo yake ni wajenzi kujenga majengo yasiyokuwa na uwiano kati ya ukubwa wake na
kiasi cha nishati ya umeme
kinachohitajika.
Mhandisi
Makwaya alisisitiza kuwa changamoto hiyo
ilipelekea Wizara kubuni mkakati huo ambao utaisaidia nchi kuokoa kiasi cha nishati
kinachopotea na kuongeza kuwa katika utekelezaji wa mpango huo elimu kwa umma itatolewa ili wananchi wawe na
uelewa wa kusimamia vyema matumizi bora ya nishati .
“Wananchi
wengi hususani wafanyakazi maofisini na viwandani hawana uelewa juu ya matumizi
sahihi ya nishati ya umeme, mpango huu utakuwa ni mkombozi na hii itachangia
uchumi wa nchi kukua kwa haraka kwa kuokoa gharama zisizo za lazima. “
Alisisitiza Mhandisi Makwaya.