NG’OMBE 150 wameuawa na askari wa Wanyama Pori katika Hifadhi ya
Biharamulo, kutokana na mgogoro uliokuwepo wa kuwaondoa baadhi ya
wafugaji, waliovamia eneo la hifadhi.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna
Tibaijuka, amekiri kuuawa kwa ng’ombe hao wakati akizungumza na gazeti
hili kwa njia ya simu jana.
Alisema Waziri Mkuu, Mizengo Pinda amewaagiza baadhi ya mawaziri
kwenda wilayani humo, kusuluhisha mgogoro huo, na kwamba kwa sasa
wamefikia mahali pazuri.
“Tuko huku baadhi ya mawaziri, tumeagizwa na Serikali Kuu kuja
kushughulikia mgogoro huu, kulikuwa na mgogoro ambapo watu waliokuwa
wakiondolewa hifadhini, sasa mchakato huo ukasababisha ng’ombe hao
uliowataja kufa,” alisema Waziri Tibaijuka.
Alisema wachungaji wa ng’ombe hao, walikamatwa ndani ya hifadhi
pamoja na mifugo yao, na utaratibu ulipaswa kuwapiga faini au kufikishwa
mahakamani kwa wale watakaogoma kulipa faini, lakini katika mazingira
hayo kuliibuka mgogoro huo.
“Tuko huku na sasa hivi ndiyo tumetoka kwenye kikao cha kushughulikia
mgogoro huu, lakini mpaka sasa tumeshafikia pazuri,” alisema Waziri
Tibaijuka.
|
