![]() |
BUNGE la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, leo linaanza kikao chake
cha Bajeti, ambapo muda wa kuchangia na kuwasilisha bajeti za wizara
mbalimbali, umepunguzwa.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari jana, Mkurugenzi wa
Shughuli za Bunge, John Joel, alisema muda wa kuchangia Bajeti hiyo,
umepunguzwa kutoka dakika 10 hadi saba na muda wa uwasilishaji wa bajeti
za wizara mbalimbali, pia umepunguzwa.
Alisema kutokana na mabadiliko hayo, sasa kila wizara itapewa siku moja ya kuwasilisha bajeti yake na kujadiliwa.
“Tumepima muda tukaona unatosha,“ alisema.
Kwa mujibu wa Joel, Bunge litaanza kujadili hotuba ya bajeti ya Ofisi
ya Waziri Mkuu leo jioni kuanzia saa kumi baada ya kumalizika kipindi
cha maswali na majibu na kikao cha kupeana ratiba.
Joel alisema Bunge hilo pia limeongeza siku za kufanya kazi na
litakaa mpaka siku za Jumamosi, lengo likiwa ni kuokoa muda uliopotea.
“Vikao vitaanza saa tatu asubuhi hadi saa nane mchana na kutakuwa na
mapumziko, ambapo vitaanza tena saa 10 hadi saa mbili usiku na kwa siku
za Ijumaa, vikao vitaanza saa tatu hadi saa saba na Jumamosi vitaanza
saa tatu mpaka saa saba,” alisema.
Ridhiwani, Godfrey
Alisema wabunge wawili wapya, Ridhiwani Kikwete wa Jimbo la Chalinze
Mkoa wa Pwani na Godfrey Mgimwa wa Jimbo la Kalenga Mkoa wa Iringa
wataapishwa leo, kabla ya kuanza kwa mkutano wa kawaida.
Huko Kalenga, Mgimwa aliwashinda wagombea wenzake, Grace Tendega wa
Chadema na Richard Minja wa Chausta, kwa kupata kura 22,943 dhidi ya
kura 5,800 za Chadema huku Chausta ikiambulia 143.
Ridhiwani alishinda uchaguzi wa Jimbo la Chalinze kwa kupata kura
20,812, akifuatiwa kwa mbali na mgombea wa Chadema, Mathayo Torongey
aliyepata kura 2,628, mgombea wa CUF, Fabian Skauti aliyepata kura 473
na mgombea wa AFP, Munir Husein aliyeambulia kura 78.
Uchaguzi mdogo wa Kalenga ulifanyika hivi karibuni baada ya kifo cha
aliyekuwa Mbunge wake, Dk William Mgimwa na Uchaguzi wa Chalinze,
ulifanyika baada ya kifo cha aliyekuwa mbunge, Said Bwanamdogo.
|

