MKUTANO wa 13 wa Bunge unaanza leo mjini hapa, ambapo pamoja na mambo
mengine, unatarajia kujadili Miswada ya sheria mbalimbali, ukiwamo ule
wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa Mwaka 2013.
Aidha, miswada mingine inayotarajiwa kujadiliwa na wabunge katika
mkutano huo ni Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali na ule wa Kura
ya Maoni wa Mwaka 2013.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari jana Kaimu Mkurugenzi wa
Habari, Elimu kwa Umma na Uhusiano wa Kimataifa wa Bunge, Deogratias
Egidio, alisema Serikali imesema itaupeleka bungeni Muswada wa Sheria ya
Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa Mwaka 2013 kwa ajili
ya kujadiliwa katika Mkutano wa Bunge wa sasa.
Hata hivyo, Egidio alisema hadi jana Bunge lilikuwa bado halijapokea
muswada huo. Alisema kutokana na mabadiliko ya kalenda ya Mkutano wa
Bajeti ya Serikali na pia kwa mujibu wa Kanuni ya 94 ya Kanuni za Bunge
toleo la 2013, Bunge litakaa kama Kamati ya Mipango ili kutekeleza
matakwa ya Ibara ya 63(3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alisema Ibara hiyo, inalipa uwezo Bunge kujadili na kuishauri
Serikali juu ya mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa
na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2014/2015. Bunge linategemewa kuujadili
Mpango huu kwa siku tano mfululizo.
Alisema Bunge linaweza pia kufanya shughuli nyingine yoyote, kama litajiridhisha kuwa inakidhi kanuni zake.
Aidha miongoni mwa mambo yaliyotarajiwa kuwamo kwenye orodha ya
shughuli za Mkutano wa sasa wa Bunge na kujadiliwa na wabunge ni Muswada
binafsi, uliowasilishwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe
(Chadema) ambaye anataka Sheria ya Magazeti ya Mwaka 1976 ifutwe.
Egidio alisema katika Mkutano wa sasa wa Bunge, kutakuwa na maswali
ya kawaida ya msingi 125 na 16 ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu,
yatakayoulizwa na wabunge. ***************************************

