WANAFUNZI WAKAMATA MWIZI BWENINI,WAMSHAMBULIA HADI KUFA


WANAFUNZI wa Shule ya Sekondari Ntuchi wilayani Nkasi mkoani Rukwa wanadaiwa kumuua kwa kumpiga mkazi wa kijiji cha Ifundwa wilayani hapa, Ignas Maruku (29) wakimtuhumu kuingia kwenye bweni la wanafunzi wa kike na kuiba nguo zao mbalimbali, zikiwemo nguo za ndani.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda amemweleza mwandishi wa habari hizi kuwa tukio hilo lilitokea Aprili 25 mwaka huu saa 6.00 mchana wakati wanafunzi hao wakiwa darasani.
Akisimulia tukio hilo, Kamanda Mwaruanda alisema siku hiyo, mmoja wa wanafunzi hao wa kike ambaye jina lake halikuweza kufahamika mara moja akiwa nje ya madarasa karibu na bweni lao alimwona kijana huyo akiingia bwenini mwao hivyo alimshtukia na kuanza kupiga kelele.
Inadaiwa ndipo wanafunzi hao wa kike na wa kiume walipotoka darasani na kuanza kumfukuza mwizi huyo kisha kumkamata na kuanza kumshambulia kwa mawe, marungu na fimbo hadi akazimia.
Wakati wanafunzi hao wakimsulubu mwizi wao huyo ndipo walimu wao walipoacha shughuli zao zote shuleni hapo na kukimbilia eneo la tukio na kuamuru wanafunzi hao watawanyike na kuacha kumpiga mtuhumiwa huyo, warejee madarasani.
Kwa mujibu wa Mwaruanda, walimu hao walitaarifu polisi ambao kwa kushirikiana nao walimkimbiza mtuhumiwa huyo katika Hospitali Teule ya Wilaya hiyo mjini Namanyere, lakini alifariki dunia wakati akipata matibabu hospitalini hapo.
Kamanda Mwaruanda amedai kuwa mwalimu wa shule hiyo aliyetambuliwa kuwa Thobias Ndunguru (26) na mkazi wa kijiji hicho cha Ntuchi, Simon Osayi wanashikiliwa na Polisi kwa mahojiano kuhusu mauaji hayo, lakini hakuna mwanafuzi yeyote anayeshikiliwa hadi sasa huku uchunguzi zaidi wa tukio hilo ukiendelea.
SOURCEHABARI LEO
 
© 2012. Design by Ernest James Siwigo Chambasi - Supported By John James Chambasi And Maganza Family