HABARI KUHUSU MTU ALIYEUWAWA NA KUZIKWA KABURI MOJA NA MAREHEMU ALIYEFARIKI MDA HUKO MKOANI MBEYA

Kamanda Wa Polisi Mkoani Mbeya
KATIKA hali isiyo ya kawaida, mkazi wa Kitongoji cha Maweni, Kijiji cha Mkwajuni wilayani Chunya, Flavin Mwamosi Mwachuki (70) amepigwa hadi kufa na hatimaye kuzikwa kaburi moja na mtu anayedaiwa kumuua kishirikina.
Hayo yamethibitishwa na Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya, Diwani Athuman aliyezungumza na gazeti la habari leo  jana.
Alisema Mwachuki aliyekuwa mkulima na mkazi wa Maweni alifikwa na mauti hayo juzi Ijumaa saa tisa alasiri baada ya kushambuliwa kwa mawe hadi kufa na watu waliojichukulia sheria mkononi, wakimtuhumu kuwa amemloga na kumuua Peter Robert (28), mkazi wa kijijini hapo.
Kamanda Athuman aliongeza kuwa, Mwachuki aliuawa makaburini ulikokuwa unazikwa mwili wa Robert na baada ya watu hao kufanikisha mauaji, waliichukua miili yote na kuizika katika kaburi moja. Kutokana na tukio hilo, Kamanda Athuman amesema msako mkali unafanywa ili kuwabaini waliohusika na kifo cha Mwachuki.
Aidha, ametumia fursa hiyo kuwaasa wananchi na jamii kwa ujumla kuachana na imani za kishirikina, akisema hazina faida zaidi ya kuchochea migogoro katika jamii zao, huku akionya kuwa, kujichukulia sheria mkononi ni kinyume na sheria za nchi.
“Tupuuze ushirikina na tuepuke kuwatuhumu watu na kujichukulia sheria mkononi. Kwa kuwa haya yameshatokea, tunaomba ushirikiano wa karibu kwa watu wenye taarifa zaidi ya tukio hili ili Jeshi la Polisi liweze kuchukua hatua za haraka dhidi ya wahusika,” alisema Kamanda Athuman.

sourcehabari leo
 
© 2012. Design by Ernest James Siwigo Chambasi - Supported By John James Chambasi And Maganza Family