
VIJANA wawili waliokuwa wanafunzi wa
Shule ya Sekondari ya Chemchem wilayani Mkalama katika Mkoa wa Singida,
wamehukumiwa kifungo cha miaka sita kila mmoja baada ya Mahakama kuwatia
hatiani kwa kosa la mauaji ya mwalimu wao. Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma
inayoendesha vikao vyake mjini Singida, ilitoa hukumu hiyo jana.
Waliohukumiwa ni Shani Mtua na Mohammed
Salimu ambao wakati walipotenda kosa hilo, mwaka 2008, walikuwa Kidato
cha Tatu na walikuwa na umri wa miaka 18 kila mmoja.
Ilielezwa mahakamani kwamba kulikuwa na
washitakiwa wengine wawili katika kesi hiyo; Emmanuel Daud na Michael
Msengi, walikufa wakiwa mahabusu wakisubiri kesi yao kusikilizwa na
Mahakama Kuu.
Hukumu ilitolewa na Jaji Rehema Mkuye
baada ya washitakiwa hao kukiri shitaka la kuua bila kukusudia
walilofanya katika Kijiji cha Mpambala, Tarafa ya Kirumi Wilaya ya
Mkalama.
Awali, Mwanasheria wa Serikali, Zakaria
Elisaria aliyekuwa anasaidiwa na Karen Mrango, alidai mahakamani kwamba
washitakiwa walihusika na mauaji ya Rajabu Idude (49), aliyekuwa Mwalimu
wa Nidhamu shuleni hapo. Ilidaiwa walifanya mauaji hayo Agosti 2008.
Mwanasheria huyo wa Serikali alidai
chanzo cha mauaji hayo ni mshitakiwa wa kwanza , Shani, kupewa barua ya
kusimamishwa masomo kwa wiki mbili kutokana na utovu wa nidhamu na kisha
akashawishi wenzake watatu kumpiga mwalimu huyo.
Zakaria alisema wanafunzi hao walimvizia
mwalimu huyo katika kichaka cha karibu na shule yao wakampiga ngumi na
mateke, kisha wakamjeruhi mwilini kwa kisu alichokuwa nacho mshitakiwa
wa kwanza.
Inadaiwa kutokana na kipigo hicho,
Mwalimu Idude alipiga kelele na mwanawe aliyetajwa kwa jina la Maye
Rajabu, alifika haraka kwenye eneo la tukio, lakini akakuta ameshakufa.
Wanafunzi hao (washitakiwa) hawakukutwa katika eneo hilo lakini msako ulifanyika usiku huo na wanafunzi wanne walikamatwa.
Baada ya kuhojiwa kuanzia ngazi ya mlinzi wa amani kwenye kijiji hicho hadi jana mahakamani, walikiri kosa.
Kwa upande wake, Wakili wa washitakiwa,
kutoka Kampuni ya Uwakili ya Kim & Company, Raymond Kimu, alimwomba
Jaji Mkuye kutoa adhabu nafuu dhidi ya wateja wake, kutokana na kuonesha
ushirikiano wa kutosha tangu siku waliyokamatwa. Aidha, alidai
washitakiwa walifanya kosa hilo kutokana na kusukumwa na umri mdogo wa
utoto.
Alidai ni wakosaji wa mara ya kwanza,
wanajutia kosa hilo na kwamba wamekaa jela kwa muda mrefu wa miaka sita,
hivyo wamejifunza kutokana na mauaji hayo.
Akitoa hukumu, Jaji Mkuye alisema hakuna
ubishi kwa yote aliyosema wakili wa utetezi. Hata hivyo alisema,
anadhani sababu hizo siyo kibali kwa washitakiwa hao kupanga na
kutekeleza mauaji dhidi ya mwalimu wao aliyekuwa anasimamia nidhamu.
“Nadhani kosa walilofanya haliwezi
kukubalika kwa jamii hata kidogo…fujo zimekuwa zikitokea kwenye mashule
na vyuo, hata kusababisha vurugu kiasi cha kuathiri utendaji…, kufuatia
kosa hili, kila mmoja atatumikia kifungo cha miaka sita jela,” alisema
Jaji Mkuye.
