MIJI NA VIWANJA VITAKAVYOTUMIKA KATIKA KOMBE LA DUNIA BRAZIL



Rio de Janeiro, Brazil
Zimebaki siku 16 kabla ya kuanza kwa fainali za Kombe la Dunia 2014 nchini Brazil.
Mwaka huu, fainali hizo zimepangwa kufanyika Juni 12 mpaka Julai 13 na zitachezwa kwenye viwanja 12.
Vifuatavyo ni viwanja hivyo 12:
Uwanja wa Itaipava Pernambuco (Recife)
Una uwezo wa kuchukua mashabiki 46,000. Inatarajiwa hali ya hewa katika mji wa Recife wakati wa mwezi Juni itakuwa joto la 25°C.
Mji wa Recife unafananishwa na mji wa Venice, Italia kwa sababu ya mito na mifereji ya maji. Recife pia inajulikana kwa kuwa na fukwe nzuri. Shujaa wa mji huu ni nyota wa zamani wa Brazil, Rivaldo.
Uwanja wa Amazonia-Manaus
Una uwezo wa kuchukua mashabiki 44,000. Hali ya hewa mwezi Juni inatarajiwa nyuzijoto 27.5°C.
Uwanja wa Amazonia upo katika mji wa Manaus ambao una msitu wa Amazonia wenye mvua nyingi na unaotembelewa na watalii wengi. Nyota kutoka mji huu ni Francisco Lima Govinho aliyekuwa kiungo mkabaji wa timu ya taifa ya Brazil.
Uwanja wa Pantanal (Cuiaba)
Una uwezo wa kuchukua mashabiki 43,000. Hali ya hewa mjini Cuiaba mwezi Juni inatarajiwa kuwa 24.1°C. Cuiaba ni mji wa tatu kwa kuwa na ng’ombe wengi Brazil. Mchezaji maarufu kutoka mji huu ni kiungo mkabaji Lucas Leiva anayeichezea klabu ya Liverpool ya England.

Uwanja wa Das Dunas (Natal)
Una uwezo wa kuchukua mashabiki 43,000. Wakati wa fainali, hali ya hewa mjini Natal inatarajiwa kuwa 25°C. Mji wa Natal ni maarufu kwa miti mikubwa, hasa mikorosho.
Marinho Chagas ndiye mchezaji maarufu kutoka mji huu na ambaye wachezaji wengi walimuiga staili yake ya kucheza beki wa kushoto na kushambulia kama winga.
Uwanja wa Maracana (Rio de Janeiro)
Una uwezo wa kuchukua mashabiki 78,838. Uwanja huu utakaotumiwa kwa mechi ya fainali. Hali ya hewa mjini Rio mwezi Juni itakuwa 22°C.
Rio ina watu zaidi ya 6.3 milioni, ukiwa na fukwe kubwa za kuvutia. Pia ni maarufu kwa sherehe za Carnival na ngoma za samba. Mji wa Rio una milima miwili maarufu ambayo ni The Corcovado na Sugarloaf inayotembelewa na watu wengi.
Wachezaji nyota duniani, Ronaldo, Zico, Romario na Zizinho wanatokea mji huu.
Uwanja wa Itaquera (Sao Paulo)
Una uwezo wa kuchukua mashabiki 68,000 na hali ya hewa mjini Sao Paulo itakuwa 22°C wakati wa fainali hizo.
Sao Paulo ina watu zaidi ya 20 milioni, pia ndiyo mji wenye utamaduni mwingi wa Brazil, na una migahawa mingi.
Wachezaji maarufu kama Cafu na Roberto Carlos, na mchezaji wa kwanza mweusi wa Brazil katika karne ya 20 kucheza soka ya kulipwa, Arthur Friedenreich wanatokea mji huu wa Sao Paulo wenye watu wengi kulinganisha na miji mingine nchini Brazil.
Uwanja wa Mineirao (Belo Horizonte) 

Una uwezo wa kuchukua mashabiki 64,000. Hali ya hewa mjini Belo Horizonte inatarajiwa kuwa 25°C wakati wa fainali hizo.
Belo Horizonte ni maarufu kwa shughuli za utalii nchini Brazil.
Shujaa wa mji wa Belo Horizonte ni mshambuliaji wa zamani wa timu ya taifa ya Brazil, Tostao.
Uwanja wa Baixada (Curitiba)
Una uwezo wa kuchukua mashabiki 41,456. Inatarajiwa kuwa hali ya hewa mwezi Juni itakuwa 18°C.
Jina la Curitiba linatokana na lugha ya Kireno likiimaanisha miti mingi aina ya pine ambayo hapa nchini inafahamika kama miti ya krisimasi. Mshambuliaji wa zamani wa klabu ya Curitiba FC, Duillio Dias anatokea mji huu na ndiye shujaa wa mji huu.
Uwanja wa Taifa wa Brasilia (Brasilia)
Una uwezo wa kuchukua mashabiki 70,064. Inatarajiwa hali ya hewa katika mji wa Brasilia wakati wa mwezi Juni itakuwa na joto la 26C.
Brasilia ndiyo mji mkuu wa Brazil na ndiko anakotokea mshambuliaji wa AC Milan, Kaka ambaye hivi sasa hajachaguliwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Brazil kitakachoshiriki Fainali za Kombe la Dunia.
Uwanja wa Castelao (Fortaleza)
Una uwezo wa kuchukua mashabiki 67,037. Inatarajiwa hali ya hewa katika mji wa Fortaleza wakati wa mwezi Juni itakuwa na joto la 29.6C.
Kila siku ya Jumatatu klabu ya usiku ya El Pirata inafahamika kwa burudani motomoto mjini Fortaleza kiasi kwamba gazeti la Marekani la New York Times liliwahi kuandika kwamba Fortaleza ndiyo sehemu inayopagawisha duniani kwa starehe.

Mario Jardel, aliyewahi kuichezea Bolton Wanderers ya England, anatokea mji huu wa Fortaleza.
Uwanja wa Fonte Nova - Salvador
Una uwezo wa kuchukua mashabiki 55,000 na hali ya hewa mjini Salvador inatarajiwa kuwa 26.5C. Salvador inajulikana kama mji wa furaha na kila mwaka huwa ndiyo unaandaa sherehe za Carnival ambazo ni maarufu sana nchini Brazil. Mchezaji shujaa wa mji huu ni Bebeto.
Uwanja wa Jose Pinheiro Borda (Porto Alegre)
Una uwezo wa kuchukua mashabiki 50,287. Inatarajiwa hali ya hewa katika mji wa Porto Alegre mwezi Juni itakuwa 19.7C.
Mji huu wa Porto Alegre ndiko anakotokea kocha wa timu ya taifa ya Brazil, Luiz Felipe Scolari, pia kocha aliyemtangulia Mano Menezes. Hali kadhalika zipo klabu maarufu ambazo ni Gremio na Internacional.
Mchezaji nyota kutoka mji huu ni Ronaldinho ‘Gaucho’ ambaye aling’ara akiwa na klabu za Barcelona na AC Milan, lakini hivi sasa hajachaguliwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Brazil.





 
© 2012. Design by Ernest James Siwigo Chambasi - Supported By John James Chambasi And Maganza Family