![]() |
MAKAMU wa Rais, Dk Mohammed Gharib Bilal amevionya vyama vya siasa
nchini na kuwataka viongozi wake kuacha kuwapandikiza wananchi mbegu za
chuki na uhasama kwa uroho wa madaraka.
Alisema hayo wakati akifungua Kongamano la Miaka 50 ya Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar mjini hapa, ambalo lililenga zaidi kuzungumza
mwelekeo wa uchumi na ustawi wa jamii.
Alisema vipo vyama vya siasa, visivyokuwa na ushawishi Zanzibar,
vimekuwa vikiendesha siasa za chuki, zenye mwelekeo wa kuwagawa
Watanzania, ambao kwa zaidi ya miaka 50 sasa wanaishi ndani ya Muungano
huo kwa ushirikiano mkubwa.
“Dhambi ya utengano ni kubwa na watakaoathirika ni wananchi wetu,
ambao wananufaika sana na faida za Muungano kijamii na kiuchumi,”
alisema.
Alielezea kusikitishwa na tabia ya baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu
la Katiba kususia vikao bungeni mjini Dodoma huku baadhi yao wakitoa
kauli za chuki zenye mwelekeo wa kukebehi viongozi wakuu wa nchi,
ikiwemo Waasisi wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amaan Karume.
Alisema kauli hizo, hazikubaliki na si za kiungwana kwa wananchi wa
Tanzania, ambao kwa muda mrefu wanaishi katika mazingira ya amani na
utulivu mkubwa.
“Nimesikitishwa sana na tabia ya hawa waliotoka nje ya kikao cha
Bunge Maalumu la Katiba huku wakitoa kauli za matusi zenye kuwakebehi
viongozi wakuu wa nchi,” alisema Bilal.
Alisema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, umepata baraka ya wananchi, ambao walihojiwa na kupatikana ridhaa yao.
|

