Yanga imeweka rekodi ya kufunga
mabao saba na kuziongoza klabu za Ukanda wa Afrika Mashariki kuanza kwa
kishindo michuano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika.
Mabingwa wa Tanzania Yanga, waliitungua Komorozine
ya Comoro mabao 7-0 ambao ni ushindi mkubwa zaidi kwa matokeo ya mechi
zote za ufunguzi zikiwamo za Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho
zilizopigwa Februari 7, 8 na 9.
Katika michuano ya Ligi ya Mabingwa, Afrika Mashariki inawakilishwa na timu sita.
Miongoni mwa timu hizo sita ni KMKM ya Zanzibar
pekee ndiyo ilipoteza mchezo wake katika mechi hizo baada ya kukung’utwa
mabao 3-0 na Dedebit ya Ethiopia, wakati nne zilishinda na moja ilitoka
suluhu.
Timu zilizovuna ushindi ni Gor Mahia ya Kenya
iliyoidungua 1-0 US Bitam ya Gabon, Yanga ikaizaba Komorozine mabao 7-0,
Flambeau de l’EST ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Diables Noirs ya
Congo, KCCA iliikandamiza El Merrikh ya Sudan mabao 2-0, wakati Rayon
Sports ililazimishwa suluhu na AC Leopards ya Congo.
Kwa upande wa Kombe la Shirikisho, Ukanda wa
Afrika Mashariki, pia unawakilishwa na timu sita, ambapo Chuoni ya
Zanzibar walifungwa mabao 2-0 na How Mine ya Zimbabwe, Academie Tchite
ya Burundi ililazwa bao 1-0 na AS Kigali ya Rwanda na Victoria
University ya Uganda iliyobonyezwa mabao 3-0 na Don Bosco ya DR Congo.
AFC Leopards ya Kenya iliichapa 2-0 Defence ya Ethiopia, Azam ya Tanzania iliizaba Ferroviario ya Msumbiji bao 1-0.
|
