![]() |
Jumuiya
ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) umepokea kwa masikitiko
makubwa taarifa ya kifo cha mjumbe wa
tume ya mabadiliko ya katiba Dr Sengondo Mvungi ambacho kimetokea katika
hospitali ya Millpark nchini Afrika kusini.
Uongozi
wa UVCCM Taifa unatoa pole kwa familia na ndugu wa marehemu, pia UVCCM inatoa
pole kwa uongozi wa NCCR- Mageuzi na kwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba
Jaji Warioba pamoja na Vijana nchini kote ambao wamenufaika na Utaalamu na
mafunzo. Kama vijana tulihitaji sana mchango wa mawazo, hekima na utaalamu
kutoka kwake, hakika tumepoteza kiongozi shupavu, muadilifu na mzalendo ambae
ni mfano wa kuigwa kwa Vijana wa Taifa hili.
Kadhalika,
UVCCM inatoa pongezi za dhati kwa hotuba makini iliyojaa hekima, busara na
ushupavu wa Uongozi iliyotolewa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete.
Hakika vijana tumeridhishwa na maamuzi ya
Mheshimiwa Rais ya Kuendelea kuwa Mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
(EAC) na tunapongeza maamuzi hayo yanayolenga kudumisha Umoja na Ushirikiano wa
Nchi za kiafrika katika kujiletea maendeleo. Kwa kutambua nafasi na manufaa
yanayopatikana kwa vijana kutokana na fursa za kiuchumi, kisiasa, kijamii,
ajira nk UVCCM Inamuunga mkono Mheshimiwa Rais kwa uamuzi wake huo.
Pamoja
na kuunga mkono uamuzi huo, UVCCM inatoa angalizo kuwa ni vyema kwa nchi zote
wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuendelea kuheshimu taratibu na
kanuni za jumuiya hiyo ili kuifanya endelevu, imara na mfano kwa nchi nyingine
za Afrika na Duniani kwa ujumla. Ni lazima wazingatie kuwa Umoja na Mshikamano
ndio nguzo ya maendeleo ya kweli ya Afrika.
Pia,
Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) umesikitishwa na tuhuma ambazo
zimeripotiwa kwenye vyombo mbalimbali vya habari kutoka kwa Mbunge wa Arusha
Mjini (CHADEMA) Mheshimiwa Godbless Lema ambazo amezielekeza kwa baadhi ya
Viongozi wa Jumuiya akiwemo Mwenyekiti wa Taifa wa UVCCM Ndugu Sadifah Juma
kuwa amehusika na usambazaji wa Picha chafu mitandaoni.
Pamoja
na kusikitishwa, UVCCM inazo taarifa juu ya mgogoro unaoendelea katika Chama
Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na kwamba inamtaka Lema kutoelekeza
tuhuma kwa UVCCM na viongozi wake bali waangalie namna bora ya kushughulikia na
kutatua migogoro yao ya ndani ambayo imesababisha kuzushiana, kuchafuana na
kuvujishiana siri katika mitandao hasa ya kijamii.
UVCCM
na Viongozi wake inakana kwa namna yeyote ile kuhusika na usambazaji huo na
kwamba Jumuiya hii ni ya Vijana makini na wanaojitambua na inajielekeza katika
kufanikisha malengo ya kuundwa kwake ya kukisaidia Chama kushika dola mwaka
2015.
Na
kwamba UVCCM inalaani tabia ambayo imeasisiwa na Vijana wa CHADEMA ya
kukashifu, kuzomea na hata kutukana Viongozi wa CCM na Serikali yake na kwamba
yaliyomkuta Mhe Lema ni matunda ya kazi waliyoiasisi wenyewe.
Imetolewa
na:
PAUL
MAKONDA
KATIBU
WA IDARA YA HAMASA NA CHIPUKIZI
UVCCM
13/11/2013

