
Mechi ya kwanza ya raundi ya michuano ya Kombe la Dunia, Kanda ya Afrika kwa wanawake chini ya miaka 20 kati ya Tanzania (Tanzanite) na Afrika Kusini iliyokuwa ichezwe Mwanza sasa itafanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Baada ya ukaguzi uliofanywa na maofisa wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), imebainika uwanja huo unatakiwa ufanyiwe marekebisho ambayo hayawezi kuwahi Desemba 7 mwaka huu, siku ambayo ndiyo mechi hiyo inatakiwa kuchezwa.
Vyumba vya wachezaji vya uwanja huo ndilo eneo ambalo linatakiwa kufanyiwa marekebisho makubwa.
KILIMANJARO STARS YATUA SALAMA NAIROBI
Timu ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars) imewasili salama Nairobi, Kenya tayari kwa mashindano ya Kombe la Chalenji yanayoanza kesho (Novemba 27 mwaka huu) katika Uwanja wa Nyayo.
Kilimanjaro Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager iliwasili saa 3 usiku kwa ndege ya RwandAir, na imefikia katika hoteli ya Sandton iliyoko katikati ya Jiji la Nairobi.
Kwa mujibu wa programu ya Kocha Mkuu Kim Poulsen, Kilimanjaro Stars leo (Novemba 26 mwaka huu) ni mapumziko ambapo kesho itafanya mazoezi kujiandaa kwa mechi yake ya kwanza dhidi ya Zambia itakayochezwa Novemba 28 mwaka huu Uwanja wa Machakos.(P.T)
WANNE WASHINDA UCHAGUZI CECAFA
Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu
Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limepata wajumbe wapya wa wanne wa
Kamati ya Utendaji katika uchaguzi uliofanya leo (Novemba 26 mwaka huu)
hoteli ya Hillpark jijini Nairobi.
Uchaguzi huo ulifuatiwa na Mkutano
Mkuu wa CECAFA ulioongozwa na Mwenyekiti wake Leodegar Tenga na
kuhudhuriwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa
Miguu Afrika (CAF), Kalusha Bwalya na ofisa wa Shirikisho la Kimataifa
la Mpira wa Miguu (FIFA), Emmanuel Maradas.
Rais wa zamani wa Shirikisho la Vyama
vya Mpira wa Miguu Uganda (FUFA), Lawrence Mulindwa ndiye aliyeongoza
katika uchaguzi huo ambapo wasimamizi walikuwa Bwalya na Maradas.
Mulindwa alipata kura zote 12 na
kufuatiwa na Tariq Atta wa Sudan (10), Abdigaani Saeb Arab wa Somalia
(9) na Raoul Gisanura wa Rwanda (8). Atta, Arab na Gisanura walikuwa
wakitetea nafasi zao.
Walioshindwa ni Rais wa Chama cha
Mpira wa Miguu Sudan Kusini (SSFA), Alei Chabor aliyepata kura tano na
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kenya (FKF), Sam Nyamweya
aliyepata kura nne.
MICHUANO YA UHAI YAHAMIA CHAMAZI
Michuano ya Kombe la Uhai imeingia
hatua ya robo fainali ambapo sasa mechi zinachezwa kwenye Uwanja wa Azam
Complex uliopo Chamazi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Uamuzi wa kuhamisha mechi hizo kutoka viwanja vya Karume na DUCE ni kuziwezesha zote kuoneshwa moja kwa moja (live) na Azam Tv.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) tunaomba radhi kwa washabiki ambao watakuwa wameathirika kutokana na uamuzi huo.
USAJILI DIRISHA DOGO KUFUNGWA DESEMBA 15
Wakati dirisha dogo la usajili
linafungwa Desemba 15 mwaka huu, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) tunazikumbusha klabu zote kuheshimu kanuni na kuzingatia muda
uliowekwa.
Pia tunakumbusha kuwa kupeleka
mchezaji kwa mkopo katika klabu nyingine hakutoi nafasi ya kusajili
mchezaji mpya. Kama klabu ilisaji wachezaji 30 maana yake ni kuwa haina
nafasi ya kuongeza wachezaji.
Kwa upande wa wachezaji wa kigeni
(foreign players), tunakumbusha kuwa kuanzia msimu ujao 2014/2015
watakuwa watatu tu badala ya watano wa sasa.
Kuhusu usajili wa wachezaji kutoka nje
mpaka sasa hakuna hata klabu moja imeshaingia kwenye TMS kuomba
uhamisho. Itakapofika Desemba 15, system ya TMS itafunga.
RAMBIRAMBI MSIMBA WA ANDREW KILOYI
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha mwamuzi wa zamani wa
FIFA, Andrew Kiloyi kilichotokea mjini Iringa.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Chama cha
Waamuzi wa Mpira wa Miguu Mkoa wa Iringa, Ramadhan Mahano, Kiloyi
alifariki dunia juzi (Novemba 24 mwaka huu) kutoka na ugonjwa wa fangasi
ya ubongo, na marehemu amesafirishwa kwenda kwao Kigoma ambapo
atazikwa.
Kiloyi alizaliwa Mei 5, 1968.
Alijiunga na uamuzi wa mpira wa miguu mwaka 1988 ambapo alipata beji ya
FIFA mwaka 2001 akiwa mwamuzi msaidizi. Alistaafu uamuzi mwaka 2009, na
hadi anafariki akiwa mjumbe wa Kamati ya Waamuzi ya Chama cha Mpira wa
Miguu Mkoa wa Iringa (IREFA).
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) linatoa pole kwa familia ya marehemu, IREFA, ndugu, jamaa na
marafiki kutokana na msiba huo na kuwataka kuwa na moyo wa subira na
uvumilivu katika kipindi hicho cha majonzi. Mungu aiweka mahali pema
roho ya marehemu Kiloyi.
Boniface Wambura Mgoyo
Kaimu Katibu Mkuu
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
