Malinzi kuhamisha makao ya TFF..
Rais mpya wa shirikisho la soka
nchini Jamal Malinzi ana mpango wa kuhamisha ofisi za TFF kutoka kwenye
Uwanja wa Karume, jijini, ili eneo hilo lijengwe kitega uchumi.
Akizungumza na waandishi wa habari kwa mara ya kwanza kama rais wa
TFF tangu achaguliwe Jumapili iliyopita, Malinzi alisema katika
kuimarisha uwezo wa kifedha wa shirikisho amepanga kuamisha ofisi ili
kutoa nafasi ya uwekezaji kwenye eneo la sasa la ofisi hizo.
“Najua kwa kanuni na sheria huwezi kuhamisha ofisi za shirikisho au
Chama kilichosajiliwa kisheria bila ya maamuzi ya kamati ya Utendaji,”
alisema Malinzi. “(Lakini) Nitalipeleka hili jambo kwa kamati ya
utendaji na naamini litaungwa mkono ili ofisi zihame hapa (Karume) na
kutafuta sehemu nyingine ili kutoa nafasi ya uwekezaji ambao unalenga
kuliongezea kipato shirikisho.
” Pia alisema katika uongozi wake TFF itaimarisha kitengo cha masoko
kwa ajili ya kufanikisha kupata udhamini kwa ajili ya timu zaidi za
taifa. Mpaka sasa ni Taifa Stars tu ndiyo yenye udhamini kutoka kampuni
ya bia ya TBL ambayo ilichukua jukumu lililokuwa likitekelezwa awali na
SBL kuanzia mwaka 2006 huku timu za vijana na wanawake zikiwa kama
yatima.
Wakati huo huo, rais wa shirikisho la soka (TFF) Jamal Malinzi
amesema kuanzia mwakani kutakuwa na mashindano ya taifa ya vijana ya
U-12 ya kila mwaka ambapo watakuwa wakiongeza umri wa wachezaji kwa
mwaka mmoja. “Hii itatusaidia kujenga misingi ya wachezaji bora kwa
ajili ya vilabu na timu za taifa,” alisema na kueleza zaidi kuwa lengo
la kuongeza mwaka mmoja katika umri kila mwaka ni ili kufika mahali
ambapo “tutakuwa na mashindano ya taifa kwa wachezaji wenye umri wa
miaka 18.”

