Vyombo
vya habari vya Misri vinaripoti kuwa serikali ya nchi hiyo imemtia
mbaroni mwanasiasa maarufu Essam El Arian ambaye pia alikuwa ni
mwanachama wa Muslim Brotherhood na Makamu Mwenyekiti wa chama cha Justice and Freedom ambacho pia ni sehemu ya Muslim Brotherhood.
Bwana El Arian ametiwa mbaroni katika mji mkuu wa Kairo.
Hapo awali mwendesha mashtaka wa
nchi hiyo aliagiza Essam El Arian akamatwe tangu mwezi July baada ya
Rais Mohammad Morsi ambaye pia alikuwa ni mwanachama wa Justice and Freedom kuondolewa madarakani.
Kukamatwa kwa kiongozi huyo ni moja ya hatua ya
serikali iliyopo madarakani kudhibiti hatakati zinazoendeshwa na kundi
hilo lenye itikadi kali za kiislamu ambazo zimepigwa marufuku.
Shirika la habari la serikali la Misri, Mena,
limesema Bwana Erian anatarajiwa kufikishwa mahakamani wiki ijayo pamoja
na Rais aliyoondolewa madarakani Mohammad Morsi na maafisa wengine wa
Muslim Brotherhood.
Msemaji wa Muslim Brotherhood ameimbia BBC kuwa Bwana Erian alikamatwa siku ya jumatano akiwa nyumbani kwake mjini Cairo.
Picha zilizosambazwa kwenye vyombo vya habari
vya Misri zinaonyesha kitendo cha kukamatwa kwake ambapo Bwana Erian
anaonekana akiwa na tabasamu amesimama karibu ni mifuko miwili.
Mwandishi wa habari wa BBC aliyepo Cairo Orla
Guerin anasema kabla ya Bwana Erian kwenda mafichoni alikuwa ni
mwanachama maarufu wa Muslim Brotherhood.

