Dar es Salaam. Kauli ya Serikali
iliyotolewa bungeni juu ya kufutwa kwa matokeo ya mtihani wa kidato cha
nne na sababu za kufeli kwa wanafunzi wengi, imeibua utata baada ya
taarifa kadhaa kuonyesha kuwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi
ilibariki mabadiliko ya mfumo mpya wa kupanga madaraja.
Taarifa
ya Serikali iliyosomwa bungeni Mei 3, mwaka huu na Waziri wa Nchi Ofisi
ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi ilisema Baraza la
Mitihani la Taifa (Necta), lilifanya mabadiliko ya mfumo bila
kushirikisha wadau.
“Baraza la Taifa la Mitihani
lilikuwa linachakata alama za mwisho kwa kutumia mfumo ambao ulikuwa
unabadilika kwa kutegemeana na hali ya ufaulu wa mwanafunzi... lakini
mwaka 2012 lilitumia mfumo mpya wa kuwa na viwango maalumu vya kutunuku
(fixed grade ranges).”
“Tume imebaini kwamba, pamoja na
mfumo huo kuandaliwa kwa nia nzuri, utaratibu huo mpya haukufanyiwa
utafiti na maandalizi ya kutosha kabla ya kutumika.
“Baraza
la Taifa la Mitihani limeelekezwa kuzingatia kuwa pamoja na kwamba
sheria ya kuanzishwa kwake inawaruhusu kufanya marekebisho ya mchakato
wa mtihani, lakini marekebisho yoyote ya kubadilisha utaratibu wa
kupanga viwango vya ufaulu na madaraja ya matokeo ya mtihani lazima
yahusishe wadau wote wanaohusika na mitalaa, ufundishaji na mitihani.”
Kwa
mujibu wa vielelezo vilivyochapishwa na Gazeti la Wiki la Jamhuri,
mfumo huo ulipitishwa na Serikali kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya
Ufundi.
Nyaraka hizo zinaonyesha kuwa, kikao kilichokutana na
kujadili mapendekezo ya Necta ya kubadili mfumo huo kiliongozwa na
Waziri wa Elimu, Dk Shukuru Kawambwa na Katibu wake alikuwa Naibu Waziri
wa Elimu, Philip Mulugo.
Muhtasari wa kikao hicho
unaonyesha wajumbe wa mkutano huo walikuwa ni pamoja na Kaimu Katibu
Mkuu wa Wizara hiyo Selestine Gesimba, Kamishna wa Elimu, Profesa
Eustell Bhalalusesa, Paulina K Mkonongo, Marystella Wassena, T.E. Temu,
Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (Nacte), Dk Primus
Nkwera, Bunyanzu Ntmabi, H.A Lihawa wote wakiwa wajumbe kwa upande wa
Wizara.
Kutoka Necta wajumbe walikuwa ni Dk C.E Msonde,
Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Dk Joyce Ndalichako, Mwenyekiti wa Bodi
ya Necta, Profesa Rwekaza Mukandara pamoja na Profesa Sifuni Mchome,
ambaye ni Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu (TCU).
Aidha,
Gesimba alimwandikia barua Katibu Mtendaji wa Necta yenye kumbukumbu
namba CAC.109/437/01N Desemba 12 mwaka jana akiliagiza kutumia mfumo
mpya wa kukokotoa alama za mitihani ya kidato cha nne na sita.
“Tafadhali
rejea kikao kilichofanyika tarehe 10/12/2012 katika ukumbi wa mikutano
wa wizara kuhusu somo tajwa hapo juu (Maagizo ya kuhusu utaratibu wa
matumizi ya viwango vya ufaulu katika mitihani ya kidato cha nne na
sita).
“Viwango vya ufaulu vilivyopendekezwa na Baraza
la Mitihani la Tanzania vitumike kwa mitihani ya Kidato cha Nne 2012 na
Kidato cha Sita kwa mwaka 2012 tu.
“Viwango vya kutunuku (grade rage) vifanyiwe kazi zaidi
ili kupunguza au kuondoa mrundikano (bunching) wa alama katika kundi
moja.”
“Necta ifanye utafiti kuhusu matumizi ya alama
za maendeleo kwa O level (kidato cha kwanza mpaka cha sita) na A Level
(kidato cha tano na sita) na kutoa mapendekezo mapya ya matumizi ya
alama za maendeleo (continuous assessment).”
“Utekelezaji
wa maagizo haya ufanyike mapema ili mapendekezo yaliyowasilishwa yaweze
kuanza kutumika katika Mwaka wa Fedha 2013/2014.”
Mbali
na barua hiyo, Profesa Bhalalusesa aliandika barua kwa Katibu Mtendaji
wa Necta, Novemba 14, mwaka huu kuhusu utaratibu wa matumizi ya alama za
maendeleo ya mtihani na viwango vya ufaulu katika mitihani ya taifa.
“Rejea
kichwa cha habari hapo juu na barua yako yenye kumbu Na. MTS.
1/29/VOL.XII/61 ya tarehe 20/09/2012. Kutokana na maelezo ya barua yako,
Wizara imeridhia mapendekezo ya uwiano wa alama za maendeleo ya
wanafunzi (CA) na alama za mtihani wa mwisho kubadilishwa kutoka alama
50:50 na kuwa 30:70.”
“Wizara inaridhia pia alama 15 zitokane na mtihani wa kidato cha pili kwa wanafunzi wa kidato cha nne.”
“Aidha, wizara inataka mlete mchanganuo wa jinsi alama
15 zilizobakia zitakavyopatikana ili kuleta uelewa wa pamoja. Vivyo
hivyo, mchanganue utaratibu wa mgawanyo wa alama za maendeleo ya
mwanafunzi wa kidato cha sita,” ilisema.
Akizungumza na
mwandishi wetu jana, Dk Kawambwa alisema hawezi kuzungumza chochote na
badala yake atafutwe Mwenyekiti wa Tume ya Kuchunguza Kushuka kwa
Kiwango cha Ufaulu wa Mtihani huo, Profesa Sifuni Mchome kwa kuwa kwa
sasa masuala yote yapo chini yake.
“Naomba nisi-comment
(nisizungumze) chochote kwa sasa, muulizeni Profesa Mchome kwa kuwa
sasa hivi mambo yote yapo chini ya tume, nikizungumza nitawaudhi,”
alisema.
Hata hivyo, jana Profesa Mchome ambaye pia
alikuwa mjumbe wa kikao kilichopitisha mapendekezo hayo ya awali,
hakupatikana kuzungumzia madai hayo lakini juzi akizungumza na mwandishi
wetu alisema tume yake ilibaini kuwa Necta na wizara walikubaliana
mwaka jana kuanza kutumia kanuni hiyo na utekelezaji wake ukaanza mwaka
jana jambo ambalo halikuwa sawa.
Alisema mabadiliko
makubwa kama hayo yalipaswa kuchukua angalau miaka minne ili watoto
waandaliwe kuanzia kidato cha kwanza na waje wapimwe wanapofika kidato
cha nne.
“Vyote hivi ni vyombo vya Serikali (Necta na
Wizara ya Elimu) kwa hiyo kujikosoa siyo tatizo, sisi tumeona hilo ni
tatizo na tukapendekeza hivyo na Serikali ikaamua kujikosoa,” alisema.
Alisema kuwa baada ya mabadiliko yanayoweza kufanyika bila kushirikisha
wataalamu wengi lakini suala la alama za mtihani kwa kuwa tayari matokeo
yake yameonekana baada ya kujaribiwa, ni vyema wadau wakashirikishwa
zaidi.
|