RAMA MLA VICHWA AACHIWA HURU,NI YULE ALIYEKUTWA NA KICHWA CHA MTOTO KWENYE MFUKO WA RAMBO 2008

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imemuachia huru Ramadhani Selemani (Rama mla vichwa) aliyekutwa na kichwa cha mtoto pamoja na mama yake, Hadija Ally anayedaiwa kumuua mtoto huyo kwa shoka. Ramadhani aliyekutwa na kichwa hicho kwenye mfuko wa rambo aliachiwa huru jana na Jaji Rose Temba baada ya kubainika kwamba alitenda makosa hayo akiwa hana akili timamu na mahakama kuridhika na taarifa hiyo.
“Mshtakiwa Ramadhani pamoja na Hadija wanashtakiwa kwa mauaji, mahakama imepokea taarifa ya daktari mtaalamu ikieleza kwamba ana matatizo ya akili, mahakama imetilia maanani taarifa hiyo, imeridhika mshtakiwa alitenda kosa akiwa hana akili timamu.

“Kwa kuwa hakuwa na akili timamu hawezi kutiwa hatiani kwa kosa la kuua, mshtakiwa anaachiwa huru, atabakia katika uangalizi wa hospitali ya wagonjwa wa akili na hospitali itoe taarifa kwa Waziri wa Sheria na Katiba,”alisema Jaji temba.

Wakili wa Serikali, Cecilia Mkonongo alidai kwa kuwa washtakiwa katika kesi hiyo walikuwa wawili, mshtakiwa Ramadhani ameachiwa huru kwa sababu hakuwa na akili timamu na ndiye aliyemtaja Hadija kuwa alimuua Salome Yohana.

“Mheshimiwa Jaji tunaiomba mahakama imwachie huru Hadija chini ya kifungu cha sheria namba 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Mkurugenzi wa Mashtaka nchini haoni haja ya kuendelea na mashtaka dhidi ya mshtakiwa huyo,”aliomba Mkonongo.

“Umesikia hawaoni haja ya kuendelea kukushtaki, mahakama inakuachia huru,”alisema Jaji Temba.

Awali Mkonongo alidai Aprili 24, 2008, saa 2.30 usiku, Ramadhani alikuwa akicheza na Salome na baadaye mtoto huyo alipotea katika mazingira ya kutatanisha.

Alidai alipotafutwa mtoto hakupatikana hadi walipopata taarifa kwamba katika nyumba ya Mzee Pembe chooni kimekutwa kiwiliwili bila kichwa. Wazazi walipokwenda kukagua walibaini kilikuwa cha mtoto wao.

Wakiwa katika kuangalia tukio hilo Aprili 26, 2008 pamoja na askari, taarifa iliwafikia askari kwamba katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alikamatwa mtoto akiwa na kichwa cha mtu akidai alikuwa akikipeleka kwa shangazi yake anayefanya kazi za usafi hospitalini hapo.

“Polisi na ndugu walipofika Muhimbili walibaini kwamba kichwa kilikuwa cha marehemu Salome na mwili ulipofanyiwa uchunguzi ilibainika kwamba sababu ya kifo haijulikani isipokuwa marehemu alionekana kakatwa na kitu chenye ncha kali.

“Ramadhani alipohojiwa alikiri kukutwa na kichwa hicho na kuongeza kwamba aliyemuua mtoto huyo ni mama yake kwa kutumia shoka na mama alipoulizwa alikiri kiwiliwili cha marehemu kukutwa chooni kwao,”alidai Mkonongo.

Wakili wa utetezi Yusuph Shehe akitoa taarifa ya Dk. Mdeme Erastus alidai mshtakiwa Ramadhani alifanyiwa uchunguzi wa akili na kubainika kwamba wakati akitenda kosa hakuwa na akili timamu.

“Kutokana na taarifa hiyo naomba mahakama iongozwe na kipengele cha 220(4) kinachoiongoza kuelekea kipengele namba 219(2) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai katika kumaliza tatizo la mshtakiwa,”alidai Shehe.

Ramadhani na mama yake Hadija baada ya kuachiwa huru viliibuka vilio kutoka kwa mama wa marehemu, Upendo Dunstun na shangazi wa marehemu, Furaha Musa wakipinga kitendo hicho.

“Hapana, hapana…hapana…,” alisema Upendo huku akilia kwa uchungu akielekea nje ya mahakama.

 
© 2012. Design by Ernest James Siwigo Chambasi - Supported By John James Chambasi And Maganza Family