NIYONZIMA:SITAZUNGUMZA JUU YA MWELEKEO WANGU

Haruna Niyonzima.
Na Lucy Mgina
KIUNGO wa Yanga, Haruna Niyonzima amefunguka kuwa atazungumza juu ya mwelekeo wake kwenye klabu yake mara baada ya mechi ya mwisho ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Simba mnamo Mei 18, mwaka huu.
Niyonzima, raia wa Rwanda, anatarajiwa kumaliza mkataba wa kuitumikia Yanga mwishoni mwa msimu huu na kumekuwa na taarifa tata juu ya mwelekeo wake, huku baadhi zikieleza kuwa hataongeza mkataba wa kuendelea kuitumikia timu hiyo.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Niyonzima anayesifika kwa kupiga pasi zenye ‘macho’ alisema kwa sasa hawezi kuzungumzia chochote kuhusiana na mkataba wake ila mara baada ya kumalizika kwa mechi yao dhidi ya Simba ndipo atakuwa na jibu.
“Kwa sasa siwezi kusema chochote lakini mara baada ya mechi na Simba kila kitu kitakuwa wazi, mawazo yangu nimeyaweka huko zaidi,” alisema Niyo na kuongeza:
“Mechi itakuwa ngumu sana lakini sisi tumejipanga kushinda licha ya kuwa tayari ni mabingwa.”
Wakati Niyonzima akisema hayo, kumekuwa na taarifa kuwa Simba ambayo imeyumba msimu huu, imekuwa ikifanya mipango kadhaa ya chinichini ili kufanya usajili wa nguvu huku jina la Niyonzima likitajwa kuwemo kwenye orodha ya wachezaji inaowahitaji.
Yanga imeshatangazwa kuwa bingwa wa Ligi Kuu Bara huku Simba iliyochini ya mwenyekiti wake, Ismail Aden Rage ikishika nafasi ya nne, nyuma ya Azam na Kagera Sugar.
 
© 2012. Design by Ernest James Siwigo Chambasi - Supported By John James Chambasi And Maganza Family