Songea. Mwalimu wa Shule ya Sekondari Luwawasi
iliyopo Manispaa ya Songea, Sophia Mgaya (28) amejifungua kwa njia ya
upasuaji watoto watano jana asubuhi katika Hospitali ya Rufaa ya Songea
ambapo watatu kati yao ni wa kiume na wawili wa kike.
Upasuaji huo ambao umefanywa na Daktari Bingwa wa
Magonjwa ya Wanawake, Dk Mgonde umefanyika kwa mafanikio ambapo
ulifanywa saa 5:15 asubuhi na kumalizika 5:45 asubuhi baada ya Mwanamke
huyo kugundulika akiwa na tatizo la kutanguliza kitovu wakati ujauzito
wake ukiwa na miezi saba.
Akizungumza na waandishi wa habari jana katika
wodi ya wajawazito hospitalini hapo, Ofisa muuguzi msaidizi Vilgilia
Mselewa amesema, walimpokea mama huyo jana saa 6 mchana baada ya
kufanyiwa upasuaji na hali yake pamoja na wanawe inaendelea vizuri.
Amesema, mtoto wa kwanza ni wa kike amezaliwa
akiwa na gramu 730, mtoto wa pili ni wa kiume ana uzito wa gramu 810,
watatu wa kiume alikuwa na gramu 670 wanne wa kiume gramu 820 na watano
ni wa kike aliyekuwa na gramu 430, hali za wototo zinaendelea vizuri na
wapo kwenye chumba cha watoto ambao hawajatimiza miezi.
Akizungumza hospitalini hapo na Mwananchi, Mama
mzazi wa watoto hao, amesema amefurahi kupata watoto hao na anamshukuru
Mwenyezi Mungu kwa upendo mkubwa aliompatia kwani alilia sana
alipopoteza mwanaye wa kwanza wa kike aliyezaliwa mwaka 2010 na kufariki
akiwa na miezi saba.
Aidha amewashukuru madaktari na wauguzi kwa
msaada walimpatia kwani bila wao hali ingekuwa mbaya na amewataka
Watanzania kuendelea kumwombea yeye na wanaye ili aweze kupata afya
njema na kuweza kuwalea watoto wake kwani ana hamu ya kuwaona wakikua na
kuendelea kumfariji katika maisha yake.
Naye baba mzazi wa watoto hao Zacharia James (30) mkazi wa Mkoa wa Njombe amemshukuru Mungu kwa kumpatia watoto hao.
|