NAIBU WAZIRI GEORGE SIMBACHAWENE AMKABIDHI OFISI MHE. CHARLES KITWANGA

 Aliyekua Naibu Waziri wa Nishati na Madini akisimamia Nishati,Mhe. George Simbachawene (wa tatu kushoto) akikabidhi majukumu ya ofisi kwa Naibu Waziri Mpya wa Wizara ya Nishati na Madini Mhe. Charles Muhangwa Kitwanga katika hafla fupi ya makabidhiano hayo iliyofanyika kwenye Ofisi za Wizara ya Nishani na Madini,jijini Dar es Salaam.wanaoshuhudia ni baadhi ya watendaji wa Wizara hiyo.
Aliyekua Naibu Waziri wa Nishati na Madini akisimamia nishati, Mhe. George Simbachawene akiwa katika mazungumzo na Naibu Waziri Mpya wa Wizara ya Nishati na Madini Mhe. Charles Muhangwa Kitwanga.

Na Asteria Muhozya

Aliyekua Naibu Waziri wa Nishati na Madini akisimamia nishati Mhe. George Simbachawene amemkabidhi majukumu ya ofisi Naibu Waziri Mpya wa Wizara ya Nishati na Madini Mhe. Charles Muhangwa Kitwanga ambaye atashughulikia Nishati.

Wakati akimkabidhi majukumu hayo, amemmtaka Naibu huyo kuhakikisha anasimamia suala la usambazaji wa umeme vijijini kwa kushirikiana na Wakala wa umeme Vijijini (REA) ili kukamilisha ghughuli hiyo kwa wakati, ikiwa ni pamoja na kukamilisha majukumu mengine ambayo ameyaacha akiwa bado hajayakamilisha.

“Namwaachia ofisi yangu mtu mzoefu, na anayejua kazi kuliko mimi naamini ataendeleza kile ambacho nimekiacha. Alisema Simbachawene.

Akizungumzia majukumu yake mapya katika Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya makazi , ameeleza kuwa, anaamini atatekeleza majukumu yake vizuri kutokana na kuwa na elimu na ujuzi wa masuala ya Sheria ya Ardhi na Utawala hivyo anaamini atayasimamia majukumu yake mapya vizuri.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Nishati na Madini anayesimamia madini Mhe. Charles Kitwanga, ameishukuru Wizara kwa mapokezi aliyoyapata Wizarani hapo ikiwa ni pamoja na kukabidhiwa majukumu yake mapya aliyopewa na hivyo, kuahidi kufanya kazi kwa ushirikiano ili kukamilisha yale ambayo amekabidhiwa.

“Nilipoteuliwa nilistuka kidogo, lakini baada ya kushiriki kongamano la viongozi wa dini lililo jadili masuala ya rasilimali hizi za gesi,mafuta na madini na taarifa mlizonipatia kuhusu nini natakiwa kukisimamia sasa nipo tayari kuanza kazi’’. Alisema Kitwanga.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini Eliakim Maswi, amemkaribisha Waziri huyo na kueleza kuwa, wanatarajia ushirikiano mzuri kwa kuwa anaamini anao uzoefu na uwezo mzuri utakaosaidia kukamilisha majukumu yake aliyokabidhiwa ambayo kwa kiasi kikubwa yanagusa masuala ya msingi yanayohusu maendeleo ya Taifa na Watanzania.
 
© 2012. Design by Ernest James Siwigo Chambasi - Supported By John James Chambasi And Maganza Family