MAPINDUZI ZANZIBAR YATIMIZA MIAKA 50

Rais wa Zanzibar,Dk.Ali Mohamed Sheni (kulia) akimtunuku Dkt.Salim Ahmed Salim nishani ya Mapinduzi ya Zanzibar jana katika viwanja vya Ikulu ya Zanzibar jana.Picha na Michael Matemanga
Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohammed Shein atawaongoza maelfu ya wananchi wa Zanzibar, kusherehekea miaka 50 ya Mapinduzi ya visiwa hivyo leo.
Sherehe hizo zinatarajiwa kuhudhuriwa pia na Rais Jakaya Kikwete na viongozi wengine kutoka nchi mbalimbali akiwamo Rais Yoweri Museveni wa Uganda, Ikililou Dhoinine wa Comoro na maseneta kutoka miji ya Lamu na Mombasa nchini Kenya, pamoja na mwakilishi maalumu wa Rais wa Jamhuri ya Watu wa China.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Vuga mjini Unguja jana, Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Idd alisema kuwa sherehe hizo ambazo ni kilele zitaanza saa 3.00 asubuhi baada ya viongozi wa kitaifa kuwasili, ambapo pamoja na mambo mengine Dk Shein atalihutubia taifa hilo.
Uchunguzi unaonyesha kuwa, wananchi wa visiwa hivyo wanamtarajia Rais Dk Shein kuzungumzia hali ya kiuchumi, kisiasa na kudumisha usalama wa raia kutokana na vitendo vya watu kumwagiwa tindikali, pia harakati za viongozi wa dini na wanasiasa kutaka Zanzibar kujitenga katika Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
 
© 2012. Design by Ernest James Siwigo Chambasi - Supported By John James Chambasi And Maganza Family