
*Lipumba atilia shaka elimu ya waziri wa fedha
*Yeye amjibu kwa kutoa vielelezo lukuki
MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, amelishushia tuhuma nzito Baraza la Mawaziri, baada ya kudai baadhi ya mawaziri walioteuliwa hawana elimu ya kutosha. (HM)
*Yeye amjibu kwa kutoa vielelezo lukuki
MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, amelishushia tuhuma nzito Baraza la Mawaziri, baada ya kudai baadhi ya mawaziri walioteuliwa hawana elimu ya kutosha. (HM)
Profesa Lipumba alisema mmoja wa mawaziri hao ni Waziri wa Fedha, Saada Mkuya.
Alisema chama chake, kina wasiwasi na
elimu ya Waziri Mkuya, kutokana na wasifu wake kutoonyesha vyuo
alivyosoma wakati wa kupata shahada ya kwanza na ya pili katika masuala
ya biashara.
Alisema katika tovuti ya Bunge, wasifu
wa waziri huyo umeonyesha sehemu aliyosoma elimu ya sekondari na
kuhitimu kidato cha sita.
Alisema katika tovuti hiyo, haionyeshi
chuo alichosoma shahada ya kwanza ya biashara, ingawa inaonyesha masomo
aliyochukua jambo ambalo linatia mashaka uhalali wake kuongoza wizara
hiyo nyeti.
"Ukiingia kwenye tovuti ya Bunge,
utaona wasifu wake kuanzia elimu ya msingi hadi kidato cha sita na shule
alizosoma, lakini kuanzia elimu ya shahada imeonyesha masomo
aliyochukua na kupata shahada ya kwanza ya biashara, haionyeshi vyuo,
jambo ambalo linatia mashaka," alisema Lipumba.
Alisema nafasi aliyopewa inahitaji
kiongozi mwenye upeo wa hali ya juu, kuweza kupambanua mambo yanayohusu
uchumi wa nchi kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za kifedha za
ndani na nje ya nchi.
"Napata wasiwasi kama Rais Jakaya
Kikwete, aliangalia wasifu wa waziri wake kwa sababu asingeweza
kumchagua kushika nafasi kubwa kama hii, wakati vyeti vyake vina
mashaka," aliongeza.
Alisema kitendo cha kumuweka mtu
mwenye vyeti vya mashaka, kunaweza kusababisha nchi kuyumba kiuchumi,
kuongezeka kwa deni la taifa, kwa sababu uamuzi wake unatokana na
ufahamu wake.
Alisema kutokana na hali hiyo, uamuzi
wa Serikali wa kuwaondoa mawaziri mizigo hautafanikiwa kwa sababu waziri
huyo anaweza kuongeza mzigo mwingine kwa nchi.
"Mawaziri mizigo, wanaisababishia
Serikali kuwa na viongozi mizigo, hivyo basi tunapaswa kuwa makini kwa
kupinga kuongozwa na viongozi mizigo, kwa sababu wanaweza kutuletea
matatizo," alibainisha.
Akitolea mfano katika kipindi ambacho
Waziri wa Fedha anapaswa kuwa makini na matumizi ya fedha za Serikali,
ni pamoja na kuwepo kwa mchakato wa uboreshaji wa daftari la wapiga
kura, mchakato wa Bunge maalumu la Katiba, vitambulisho vya uraia na
mambo mengine ambayo kwa kiasi kikubwa yanahitaji fedha.
Alisema kutokana na hali hiyo, waziri
huyo anapaswa kusimamia matumizi ya fedha katika shughuli mbalimbali
zikiwemo za halmashauri na safari za Rais, ambapo katika kipindi hiki
cha robo mwaka, safari zake za nje zimemaliza bajeti yake ya mwaka
mzima.
Alisema kutokana na hali hiyo, Rais
Kikwete alipaswa kumchagua mtu makini mwenye sifa stahiki kukalia nafasi
hiyo, ili aweze kutimiza majukumu yake kwa kufuata taratibu za
kisheria.
Alisema chama hicho hakina mashaka na
uteuzi wake, lakini wana mashaka na chuo alichosoma na kupata shahada ya
kwanza na ya pili.
WAZIRI AJIBU
Waziri Mkuya alisema elimu yake wala haina mashaka, kwani alisoma kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari Lumumba mjini Zanzibar.
Baada ya hapo, alijiunga na masomo ya
diploma ya Biashara katika Chuo cha Stamford cha Malaysia, ambapo pia
alichukua diploma nyingine ya biashara nchini Uingereza.
Alisema mbali na masomo hayo, pia
amesoma shahada ya pili ya biashara katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania
(OUT) na kuhitimu mwaka 2009.
"Nimehitimu Shahada ya Uzamili ya Utawala na Biashara (MBA) ya Chuo Kikuu cha WATT kilichopo Edinburgh, Scotland.
"Kwa sasa nachukua Shahada ya Uzamivu
(PhD) ya Utawala wa Biashara Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, tawi la Dar
es Salaam," alisema Mkuya.
Chanzo: MJENGWA