PICHA:POLISI MAJERUHI ALIYEJERUHIWA KWENYE TUKIO LA UJAMBAZI NEWALA ASAFIRISHWA KWA HELIKOPTA KWENDA HOSPITALI YA MUHIMBILI

ASKARI Polisi aliyejeruhiwa kwenye tukio la ujambazi wilayani Newala alisafirishwa jana kwa ndege ya polisi akipelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa matibabu zaidi.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Zelothe Stephen, askari huyo PC Isaya (34), alijeruhiwa sehemu ya paja ambapo madaktari wa Hospitali ya Newala alikokuwa amelazwa wameshauri atafutwe mtaalamu wa mifupa.
“Tunalazimika kumsafirisha majeruhi wetu kwa ndege ya polisi kwenda Muhimbili kwa ajili ya kufuata mabingwa wa mifupa kwa sababu Hospitali ya Wilaya ya Newala hakuna wataalamu hao.

“Tunawashukuru wauguzi, manesi na madaktari waliomhudimia kwa siku zote alizokaa hospitalini hapo, wameishi vizuri na majeruhi wetu hadi leo tunapomsafirisha,” alisema Kamanda Zelothe.
Katika ujambazi huo watu watatu walifariki dunia kwa kupigwa risasi, wakiwemo askari wawili ambao ni Mkuu wa Upelelezi F. 8106, Nurdun Kassim Sif (38), DC Robert F. 5339 (33) na raia Hamza Msangaluwa, ambao walifariki dunia papo hapo.
Ujambazi na mauaji hayo yalifanyika Januari 12, saa 10 jioni kwenye msitu wa Kijiji cha Kidumi baada ya mtu aliyesadikiwa kuwa jambazi kufika katika kituo cha Camel akitaka kuuziwa mafuta.

Ilidaiwa mtu huyo mwenye galoni alitaka kununua mafuta ya sh 2,500, ambapo baada ya kupimiwa mtu huyo aliingia ndani ya jengo la kituo hicho na kuwaamuru wahudumu wampe fedha za mauzo ya siku mbili.
Baada ya wahudumu kukaidi mtuhumiwa huyo alitoa bunduki yake na kuwaamuru wampe fedha walizokuwa nazo.
 Kwa mujibu wa shuhuda wa tukio hilo, baada ya jambazi huyo kuhisi anacheleweshwa alianza kupekua sehemu mbalimbali na kukuta fedha hizo uvunguni mwa meza ndani ya kituo hicho zinazodaiwa kuwa sh 3,299,180 na kukimbilia vichakani.

Baada ya jambazi huyo kutokomea vichakani wahudumu wa kituo hicho waliomba msaada wa wananchi waliomkimbiza jambazi huyo umbali wa kilometa nane kabla ya kuingia msituni.
Akiwa msituni mtuhumiwa huyo alimuua Hamza kwa risasi kabla ya kufanya hivyo kwa askari polisi wawili na kumjeruhi mmoja kisha kutokomea kusikojulikana.
Hata hivyo Jeshi la Polisi linaendelea kumsaka jambazi huyo.


Baadhi Ya Wananchi Waliokuepo Kumsindikiza Wakiwa Na Huzuni Tele