
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya
Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli amesema anawaachia
Watanzania waamue mkweli kati ya kamati yake na Naibu Waziri wa
Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu.Kauli hiyo ya Lembeli inafuatia
taarifa ya gazeti moja la kila siku (Siyo Mwananchi), iliyomnukuu
Nyalandu akisema ripoti ya Operesheni Tokomeza Ujangili iliyowang'oa
mawaziri wanne ilikuwa ya uongo.
Nyalandu anadaiwa kutoa kauli hiyo
alipozungumza na viongozi wa taaluma mbalimbali na Kamati ya Ulinzi na
Usalama Mkoa wa Dodoma na Manyara kuhusu mgogoro wa mipaka kati
wanavijiji na Hifadhi ya Tarangire.
Pia, mgogoro huo unahusisha Pori la Akiba Nkungunero na vijiji vya jirani.
Nyalandu alikaririwa akisema kutokana
na taarifa hiyo kueleza wapo watu waliobakwa wakati siyo kweli. Tanzania
imeonekana kushuka kwa kiwango kikubwa katika utawala bora kutokana na
ukiukwaji haki za binadamu.
Hata hivyo, Lembeli alipoulizwa na
gazeti hili jana kuhusiana na kauli hiyo alijibu: "Sijaisoma hiyo habari
ila nimeisikia tu, kama ni kweli ametoa kauli hiyo (Nyalandu) basi ni
hatari."
Lembeli alisema anawaachia Watanzania kupima mkweli kati yake, kamati yake na Waziri Nyalandu katika jambo hilo