| Hii ni kutoka kwa majirani zetu ambapo
tunaambiwa Wananchi wa Kenya
wameshangazwa na taarifa ya kuzinduka kwa
mwanaume mmoja aliyedhaniwa kuwa amekufa
ambapo alizinduka akiwa kwenye chumba cha
kuhifadhia maiti katika hospitali moja mjini
Naivasha umbali wa kilomita tisini kutoka mji
mkuu wa Kenya Nairobi.
Jamaa huyo anaitwa Paul Mburu ana umri wa
miaka 24 ambapo alipelekwa hospitalini kwa
matibabu baada ya kunywa sumu kwa lengo la
kujitoa uhai kutokana na ugomvi wa kifamilia
na babake ingawa ilisemekana jamaa alifariki
Jumatano usiku wakati akipokea matibabu.
Wafanyakazi wa hospitali hiyo walipigwa na
butwaa na wengine kukimbia walipoona mwili
wa mtu aliyedhaniwa kufariki ukitembea na
kuonyesha dalili za kuwa hai katika chumba
cha kuhifadhia maiti.
Afisa mkuu wa matibabu katika hospitali hiyo
ya wilaya Dokta Joseph Mburu amesema kuwa
dawa iliyotumiwa kumtibu Mburu hufanya
moyo kupiga polepole hali ambayo huenda
ilimfanya muuguzi kudhani kuwa mgonjwa
alikua amefariki.
Raia huyo wa Kenya alisikika akimtaka mmoja
wa wafanyakazi katika chumba cha kuhifadhia
maiti kumsaidia kwani alikuwa anahisi baridi
kali na hapo ndipo mmoja wa wafanyakazi
alipotimua mbio kwa hofu.
Ndugu wa jamaa huyo akiwemo babake
walikuwa wametembelea chumba cha
kuhifadhia maiti siku ya Alhamisi ili kuanza
kwa taratibu za mazishi lakini baadaye mchana
walifahamishwa kuwa Mburu alikuwa hai.
Mgonjwa anaendelea kupokea matibabu katika
hospitali ya Naivasha. |