MAJERUHI wa bomu lililolipuliwa katika mgahawa wa Vama Traditional
Indian Cuisine jijini Arusha juzi, wanachunguzwa na Jeshi la Polisi na
Idara ya Uhamiaji.
Taarifa za awali ambazo gazeti hili lilizipata jana, zilidai tukio
hilo la bomu linatokana ugomvi wa kibiashara. Taarifa hizo zilidai kuwa
Jeshi la Polisi lilikuwa linaendesha uchunguzi wa tukio hilo na pamoja
na madai kuwa linatokana na ugomvi wa kibiashara.
Alipohojiwa kwa njia ya simu jana juu ya tukio hilo na madai kuwa
kuna hisia linatokana na ugomvi wa kibiashara, Mkurugenzi wa Idara ya
Habari (MAELEZO), Assah Mwambene alisema, “ni kweli na mimi nimesikia
taarifa hizo, lakini tuviachie vyombo vya ulinzi na usalama, vilifanyie
kazi tukio hilo na vitatoa taarifa kamili vikimaliza uchunguzi wao”.
Kwa upande wake, Kamanda wa Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Arusha, Daniel
Namomba, alisema jana ofisi yake inafanya uchunguzi kuhusu majeruhi wa
tukio hilo, kubaini kama uwepo wao nchini ulikuwa ni wa kihalali.
Namomba alisema wanapitia nyaraka zote za majeruhi hao ili kujua kama
wapo, waliokuwa wanafanya kazi hapa nchini kwa vibali maalumu; na
endapo kulikuwa na watalii kati yao, ambao waliingia nchini kihalali.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana, ofisa huyo alisema,
“Siwezi kuthibitisha kama majeruhi hao walikuwa hapa nchini kihalali au
la, naomba unipe muda kwa kuwa suala hili ofisi yangu inalifanyia kazi
na baada ya uchunguzi kukamilika nitatoa taarifa rasmi”.
Kumekuwepo taarifa jijini hapa kwamba mfanyabiashara mwenye asili ya
Asia (jina tunalo), ndiye aliyekuwa mwenyeji wa majeruhi hao, wanaodaiwa
kuwa watalii, huku taarifa nyingine zikidai ni wafanyabiashara wa
madini.
“Majeruhi hawa wapo ambao ni wafanyakazi hapa (Arusha) kwa zaidi ya
miaka 15, lakini baadhi yao siyo raia na inadaiwa kuwa ni watalii na
wengine wanadai walikuja hapa zaidi ya wiki moja iliyopita kwa lengo la
kufanya biashara ya madini,” alisema mmoja wa watu, ambaye hakutaka jina
lake litajwe gazetini.
Waziri hospitalini
Katika hatua nyingine, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Seif Rashid
alitembelea majeruhi jana katika Hospitali ya Rufaa ya Seliani.
Waziri huyo alilaani vikali kitendo hicho kilichofanywa na watu ambao
wanahatarisha amani ya jiji la Arusha, ambalo ni kitovu cha utalii
nchini.
Alisema hali za majeruhi zinaendelea vizuri. Alisisitiza kwamba
vyombo vya ulinzi na usalama, vinaendelea na uchunguzi kubaini
watuhumiwa hao hatimaye wafikishwe kwenye mkono wa sheria.
Matibabu Nairobi
Waziri alisema endapo wagonjwa watasafirishwa nje ya nchi, serikali
haitahusika katika matibabu yao, kwa kuwa anaamini nchini kuna hospitali
zenye uwezo mkubwa wa kutibu majeruhi.
Akizungumzia hali za majeruhi hao, Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya
Seliani, Dk Mark Jacobson ambaye ni raia wa Marekani, alisema hali za
wagonjwa zinaendelea vizuri.
Lakini, alisema mmoja kati ya wagonjwa hao, ambaye ni mtoto wa miaka
(13), Ritwik Khaalelwa, amepelekwa Nairobi kwa matibabu kutokana na hali
yake kutoridhisha.
Aidha, alisema Deeptak Gupta aliyepoteza mguu wa kushoto, bado yuko
katika chumba cha uangalizi maalumu, kutokana na maumivu makali aliyo
nayo na familia yake inafanya utaratibu wa kumhamishia Nairobi kwa
matibau zaidi.
Jacobson alisema wagonjwa wengine wawili wanaendelea na matibabu
hospitalini hapo. Alisema watatu wameruhusiwa kwenda nyumbani baada ya
majeraha waliyoyapata, kuendelea vizuri.
Mbatia ahofu
Mwenyekiti wa Chama cha NCCR- Mageuzi, James Mbatia ametaka Serikali
kupitia Idara yake ya Ulinzi na Usalama wa Taifa, kurudi kazini na
kufanya uchunguzi wa kina juu ya milipuko ya mabomu, yanayotokea Jijini
Arusha na kutoa majibu sahihi ya matukio hayo.
Mbatia, ambaye ni Mbunge wa Kuteuliwa, alisema hayo jana jijini hapa, alipozungumza na waandishi wa habari.
Alisema mashambulio hayo katika jiji la Arusha lenye vivuto vingi vya
utalii, yanatisha na yanasikitisha na uchumi wa nchi unaweza kuyumba
kwa matukio hayo.
Mbatia alisema Tanzania ni nchi ya pili duniani kwa kuwa na vivutio
vya utalii vingi na uchumi wa nchi katika sekta ya utalii, pato lake ni
sawa na asilimia 17 sawa na Sh trilioni 9.6 kwa mwaka.
Alisema watu na mali zao katika maeneo ya Jiji la Arusha na Zanzibar,
wanapaswa kulindwa kwa nguvu zote.Alisema serikali inapaswa kufuatilia
na kutambua adui wanayepambana naye.
Alishauri serikali na vyombo vyake vya ulinzi na usalama, kukusanya
kila kiashiria cha matukio hayo bila kudharau na kisha kukaa mezani kwa
kushirikisha watu mbalimbali, kuchambua kwa kina kila kimoja kupata
ukweli na kisha kuufanyia kazi.
Viashiria
Alitaja baadhi ya viashiria vilivyowahi kutajwa na makundi mbalimbali
kuwa ni ugomvi wa kisiasa, dini, wivu wa kibiashara ya utalii na
kusherehekea na kushabikia matukio ya uvunjifu wa amani katika nchi
jirani.
Vingine ni ugomvi wa marais na mgogoro wa kutaka kumng’oa Spika wa
Bunge la Afrika Mashariki. Alisema utaratibu wa sasa wa serikali na
vyombo vya usalama, kutoa majibu mepesi kila tukio linapotokea, bila
kutoa majawabu sahihi, ni dalili za kushindwa kutafutia ufumbuzi matukio
hayo, hali inayoendelea kujenga hofu miongoni mwa wananchi.
Alionya kuwa serikali na vyombo vya ulinzi na usalama, haipaswi
kusubiri hadi jambo litokee, ndipo ianze kupambana bali inapaswa
kujipanga, ikizingatiwa tukio hilo la jana si la kwanza, bali ni la sita
ndani ya kipindi cha mwaka na nusu.
Mbatia alisema alitegemea muda huu angeona anga la Arusha likiwa
limefunikwa na helikopta na pia kukiwa na askari wa kutuliza ghasia
mitaani.
Alisema kwa mkoa wa Arusha kuendelea kukumbwa na matukio hayo ya
mabomu, kunaathiri mambo mengi, ikiwemo pato la taifa, ikizingatiwa
utalii unachangia asilimia 33 ya pato la taifa.